×

JPM Hajambeba Augustino Mrema

1Kwanza kabisa nimshukuru Mungu kwa kuweza kunipa uhai leo pia kukuwezesha wewe msomaji kusoma makala haya.

Nianze kwa kusema kwamba kitendo cha Rais Dk. John Pombe Magufuli kumteua mtu kutoka chama cha upinzani ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Lyatonga Mrema (pichani) kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Tanzania ni cha kupongezwa.

Ni mara ya kwanza tangu mfumo wa vyama vingi nchini kuanza mwaka 1992 kuona rais akiteua mtu kutoka upinzani kuongoza bodi ya taifa ya kitu fulani nchini.

Baada ya Rais Magufuli, kumteua Mrema watu wanasema amemkumbuka kiongozi huyo mkongwe nchini kutokana na uchapakazi wake.

Hii ilitokana na taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa, ambayo ilionesha uteuzi huo wa Mrema, umefanyika sambamba na uteuzi wa viongozi na watendaji wa taasisi mbalimbali za serikali.

Kuteuliwa kwa Mrema ndiyo gumzo la mjini kwa sasa kwani ni jambo ambalo siyo la kawaida kwa kiongozi wa nchi wa chama tawala kuchukua viongozi wa vyma vya upinzani kuwapa nafasi ya kuongoza.

Huko nyuma tuliwahi kushuhudia Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa akimteua Hamad Rashid kutoka Chama Cha Wananchi (CUF) kuwa mbunge na Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akimteua James Mbatia ambaye ni Mwenykiti wa NCCR- Mageuzi kuwa mbunge katika Bunge la Jamhuri.

Wote hao walioteuliwa walifanya kazi vizuri na kwa weledi wa hali ya juu. Hivyo basi uteuzi wa Mrema kuongoza Bodi ya Parole ambayo inashughulikia misamaha ya wafungwa ni jambo zuri.

Nasema ni jambo zuri kwa sababu bodi hiyo ipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo Mrema aliwahi kuwa waziri na akafanya kazi nzuri sana kiasi cha kumfanya rais aliyekuwa akiongoza kipindi hicho, Ali Hassan Mwinyi kumfanya naibu waziri mkuu.

Siyo siri, Mrema alikuwa ni mchapakazi na alikuwa akifanya kazi yake usiku na mchana, hivyo ni imani ya kila Mtanzania kwamba atafanya kazi vizuri kwa kushirikiana na viongozi wa wizara ambayo waziri wake ni Mwigulu Nchemba.

Naamini Mrema ataisaidia sana wizara hiyo na pia kusaidia Idara ya Magereza kupunguza wafungwa waliorundikana katika magereza mbalimbali nchini.

Waswahili au wahenga walisema ‘Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni’, ukweli ni kwamba Mrema ana aliyoyafanya mazuri akiwa anaongoza wizara ya mambo ya ndani ambayo hadi sasa yanakumbukwa kama vile kujenga vituo vidogo vya polisi nchi nzima, hili lilikuwa jambo jema sana kwani alisaidia kupunguza mirundikano ya watu kwenye vituo vikubwa vya polisi.

Niseme kifupi tu kwamba tukiweka siasa pembeni, Mrema hakubebwa kama watu wengine wanavyodhani lakini historia yake ya utendaji kazi serikalini imembeba.

Kitendo cha Rais Magufuli kumteua Mrema kushika wadhifa huo kiwe changamoto kwa viongozi wengine kufanya kazi kwa weledi ili mazuri yao yaendelee kuenziwa daima kama ilivyotokea kwa mkongwe huyo wa siasa nchini.

Naamini kwa uchapakazi wa Mrema  ataitendea haki nafasi aliyopewa ya kuiongoza  Bodi ya Parole na kila mmoja wetu atasema rais hakukosea.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave a Comment