IRINGA: Baada ya wananchi wa Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa kutoa kero yao ya kutengenezewa madawi ya wanafunzi wa shule yasiyo na kiwango, hatimaye kilio chao kimesikika.
Wananchi hao walilalamika na kumfikishia kilio chao Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto, kwamba madawati yanayotengenezwa wilayani humo ni chini ya kiwango kwani hupakwa rangi ya kuyang’arisha bila kupigwa randa.
Wananchi hao walisema madawati hayo yakitumika yatachana sare za wanafunzi, hivyo kuna kila dalili kwamba kuna baadhi ya watu ‘wamepiga fedha’.
Kero hiyo ilifika hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza akafanya safari ya kushitukiza akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na viongozi wa Wilaya ya Kilolo hivi karibuni ili kukagua madawati yanayolalamikiwa wilayani humo.
Akizungumza baada ya kukagua madawati hayo, mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa hajafurahishwa hata kidogo na ubora wa madawati hayo zaidi ya 600 ambayo yametengenezwa kwa fedha za Mfuko wa Jimbo la Kilolo na nyingine kutoka vyanzo vya ndani vya Halmashauri ya Kilolo.
“Baada kupata malalamiko hayo nimelazimika kufika nikiwa nimeambatana na kamati yangu ya ulinzi na usalama ya mkoa na nimejiridhisha kuwa ni kweli madawati haya yapo chini ya kiwango hayafai kwa matumizi ya wanafunzi.
“Ninaelekeza kuwa Wilaya ya Kilolo waende wakakae na kuangalia na namna gani wanaweza kutatua changamoto hii ya madawati pia naelekeza haya madawati marufuku kuyasambaza mashuleni na yale waliyosambaza yarudishwe karakana,” aliamuru mkuu huyo wa mkoa.
Alisema alishangazwa kuona madawati yanafikia zaidi ya 600 bila afisa yeyote kupita kuyakagua hadi wananchi kupaza sauti na kuona kero hiyo. Aliwalaumu watendaji wa wilaya kuanzia ngazi ya kata kwa kumdanganya kutokana na taarifa waliyokuwa wakimpa na akasema kitakachofuata baada ya kugundua kuwa yametengenezwa chini ya kiwango, kitawashangaza wengi.
Alimwambia mkurugenzi wa wilaya hiyo asicheze na kazi yake na akamuagiza akamwambie hivyo mkuu wa wilaya pia. Alisema wahusika ni lazima watazirejesha fedha walizotengenezea madawi hayo yasiyo na kiwango na katika hilo, hakutakuwa na kubembelezana.
Alimwagiza mkuu mpya wa Wilaya ya Kilolo, Asia Juma Abdallah kuhakikisha anasimamia utengenezaji wa madawati hayo 600 yenye thamani ya shilingi milioni 25.1 kwa ubora unaohitajika ndani ya mwezi mmoja.
