×

Mtumishi wa bandari ajinyonga

 ajinyongaLucas Kazimoto enzi za uhai wake.

Waandishi wetu, Amani

DAR ES SALAAM: Mtumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Lucas Kazimoto (33), anadaiwa kujinyonga nyumbani kwao, Sinza-Mugabe jijini hapa kwa kisa ambacho hakijajulikana, Amani lina stori kamili.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, tukio hilo lililoacha majonzi na simanzi nzito lilitokea mchana wa Julai 14, mwaka huu nyumbani hapo ambapo inasemekana marehemu kabla ya kujinyonga, alikuwa akizungumza mwenyewe maneno ambayo tafsiri yake pia aliijua mwenyewe.

HAKUWA AKIISHI ALIPOJINYONGEA

Chanzo kilitiririka kuwa, kipindi chote, Lucas alikuwa akiishi Mtoni Mtongani jijini Dar na hakuwa na familia lakini mara kwa mara alikuwa akionekana Sinza walipokuwa wakiishi wazazi wake.

“Marehemu alizaliwa na kulelewa hapa (Sinza) lakini pia alikuwa akiishi Mtoni. Siku aliyojinyonga, baba yake mzazi ambaye naye pia ni mtumishi wa umma, alikuwa kikazi mkoani na mama yake alikuwa nchini India akimuuguza mjukuu wao.

“Siku hiyo pale nyumbani alikuwepo mdogo wake (jina halikupatikana) ambapo alimsikia marehemu mara kwa mara akisema kuwa ni bora afe kuliko kupoteza kazi, lakini pia alikuwa akipigiwa sana simu kutoka kazini kwake zikizungumzia funguo, sijui funguo za nini?” kilisema chanzo hicho.

AFUTA NAMBA ZOTE ZA SIMU

Chanzo kikaongeza kuwa, muda mfupi kabla Lucas hajajinyonga, alifuta namba zote za kwenye simu yake sambamba na meseji, akaacha moja tu aliyomtumia mtu akisema; unamjua Neema? Amefariki dunia.

Ilidaiwa kuwa, baada ya kusema hayo, marehemu alimpa mdogo wake shilingi elfu ishirini akimwambia ashike kwanza na ndipo baadaye alipogundulika kuwa ananing’inia.

Hata hivyo, kuna madai kwamba kifo cha Lucas kina maswali mengi baada ya mazingira ya kujinyonga kutotoa ushirikiano kuwa, alijining’iniza mwenyewe.

Marehemu Lucas alizikwa Jumapili iliyopita kwenye Makaburi ya Sinza jijini hapa katika mazishi yaliyokusanya mamia ya wakazi kutoka pande zote za jiji.

KAMANDA ANASEMAJE?

Juzi, Amani lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Christopher Fuime kuthibitisha tukio hilo kama amelipata na kusema kuwa, bado halijamfikia kwa vile matukio ya kujinyonga mengi huanzia vituo vidogo.

“Tukio hilo bado sijalipata ila inawezekana likawepo lakini nafuatilia kujua zaidi,” alisema Fuime.

MWENYEKITI WA MTAA ANENA

Amani pia lilimtafuta Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sinza C, Amour A. Amour ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

“Taarifa za Lucas kujinyonga ni za kweli na niliongea na baba wa marehemu ambaye alinithibitishia kuwa mwanaye kajinyonga ila sababu hawajui ni ipi,” alisema Amour.

Leave a Comment