×

Wakali hawa walikubali Bongo kuhamia Dodoma

Mbaraka-studioMakala: Boniphace Ngumije

HIVI karibuni gumzo nchini ni juu ya kauli aliyoitoa mkuu wa nchi hii Dk.  John Magufuli kuwa serikali inahamia Dodoma. Hata hivyo, gumzo hilo si tu juu ya kauli ya mkuu huyo bali ni uwezekano wa jambo hilo ukizingatia limesemwa na wakuu wa nchi karibia wote waliopita kuanzia Mwalimu Julius Nyerere lakini halikuwezekana.

Uwezekano wa zoezi hilo kwa sasa tumuachie Rais Magufuli na timu yake,  kikubwa hapa ninakumbusha juu ya wasanii wa muziki ambao waliunga mkono kupitia kazi yao ya muziki, makao makuu ya nchi kuhamia Dodoma.

Mbaraka MwiNsheHeMbaraka Mwinshehe

Mkongwe huyu aliyefariki dunia mwaka 1979 kwa ajali ya gari nchini Kenya, enzi za uhai wake akiwa na Bendi ya Super Volcano aliachia Wimbo uitwao Makao Makuu Dodoma na hiyo ilikuwa ni baada ya Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Julius Kambarage Nyerere kutangaza nia ya kuyahamishia makao makuu ya Tanzania, kutoka Dar kwenda Dodoma.

Mbaraka alitoa kibao hicho akiwa na Kulwa Salum aliyepiga mdomo wa bata ‘Saxophone,’ Lazaro Bonzo huyu alisimama na tarumbeta, Samson Gumbo akizicharaza nyuzi za gitaa wakati Coco Billy akisapoti kwa kuimba.

king kikiiKing Kiki

Kikumbi Mwanza Mpango, huyu ni maarufu kwa jina la King Kiki au Mzee wa Kitambaa Cheupe. Naye hakuwa nyuma, akiwa na bendi yake ya Double O pia alipiga wimbo wa kusapoti juu ya nchi kuhamishia makao yake makuu Dodoma uliojipatia umaarufu sana ulioitwa Dodoma Capital.

remmy-02bcDk Remmy Ongala

Mkali katika gemu la Muziki wa Dansi nchini ambaye ni vigumu kusahaulika, Ramazan Mtoro  Ongala ‘Dk Remmy’ naye hakupenda  kubaki nyuma katika kuonesha kuunga mkono idea ya kuhamishia makao makuu ya nchi hii mkoani Dodoma.

Akiwa na vijana wenzake wa wakati huo waliokuwa wanaunda Bendi ya Super Matimila akiwemo Cosmas Chidumule aliyekuwa mwimbaji pia walitoa ngoma yenye mahadhi hayo. Hata hivyo, suala hilo wakati huo halikuweza kufanikiwa,  pengine wakati huu inawezekana kutokana na Rais Magufuli kuwa ‘siriasi’ kulifanikisha.

Leave a Comment