Meneja wa mwanamuziki, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, Hamis Tale maarufu kwa jina la ‘Babu Tale’ akiwa na Diamond Platnumz.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MENEJA wa mwanamuziki, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, Hamis Tale maarufu kwa jina la ‘Babu Tale’ jana alitiwa mikononi na Polisi kisha kupandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Tale alifikishwa mahakamani hapo jana asubuhi chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi akitokea Kituo cha Polisi cha Ilala, Dar ambapo alilala hapo tangu juzi.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Tale alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kujieleza kwa nini asifungwe kwa kushindwa kutekeleza hukumu ya mahakama iliyomwamuru alipe fidia ya Sh milioni 250 kwa makosa ya kuvunja Sheria ya Hakimiliki.
Tale anatakiwa alipe fedha hizo kutokana na kuvunja mkataba kati yake na Shehe Mbonde, kwa kuuza na kusambaza nakala za mawaidha (DVD) bila ridhaa ya shehe huyo, jambo ambalo ni kinyume na hakimiliki.
Hata hivyo, baada ya kufikishwa tena mahakamani, Tale alikuwa ameandaa mawakili wanne kwa ajili ya kutengua hukumu ya mahakama.
Lakini baada ya shauri hilo kusikilizwa kwa zaidi ya dakika 45 mawakili wake waliomba muda wa kwenda kupitia tena shauri zima mwanzo mwisho jambo lililopelekea kesi kuahirishwa mpaka Ijumaa hii (keshokutwa). Tale yupo nje kwa masharti hadi Ijumaa ambapo atatakiwa tena kwenda mahakamani hapo.
