Mbwana Samatta na Leon Bailey waibeba kwa mara nyingine KRC Genk kuipeleka kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Europa baada ya kuifunga Lokomotiva Zagreb ya Croatia mabao 2-0.
Mchezo huo ulifanyika kwenye uwanja wa Cristal Arena unaomilikiwa na Genk na Samatta ndiye alikuwa wa kwanza kuifungia goli timu yake hiyo kwenye dakika ya kwanza ya mchezo huo naye Leon Bailey alifunga ukurasa huo wa mabao kwa kufunga goli la pili kwenye dakika ya 50.
Kwenya mchezo wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita huko Croatia timu hizo zilitoka sare a kufungana mabao 2-2 huku magoli ya Genk yakifungwa na wachezaji wake Mbwana Samatta na Leon Bailey na mabao ya Lokomotiva yalifungwa na Mirko Marić na Ivan Fiolić.
Hatua hiyo imeifanya timu ya Genk kufuzu kwenye hatua ya makundi kwa jumla ya mabao 4-2 na sasa inaungana na timu nyingine kubwa kwenye hatua hiyo kama Manchester United, Ajax, Shakhtar Donetsk, Internazionale Milano na timu nyingine nyingi.