Mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib (katikati) akishangilia na wachezaji wenzake.
BAADA ya kuifungia timu yake bao la kusawazisha katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting na kuiwezesha kupata ushindi wa mabao 2-1, juzi kwenye Uwanja wa Uhuru, mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib ametoa kauli ambayo moja kwa moja inawalenga wapinzani wao wakuu, Yanga na Azam FC.
Ajib ambaye msimu uliopita alifunga mabao 9 katika Ligi Kuu Bara, amedai kuwa anataka kufunga katika kila mechi ya ligi hiyo na nyingine ambazo timu yake itashiriki, japokuwa akazuga kuwa eti hana mpango wa kuwa mfungaji bora.
Msimu uliopita Yanga ndiyo ilikuwa bingwa na ikitoa mfungaji bora, Amissi Tambwe aliyefunga mabao 21, hivyo kauli hiyo itakuwa inamaanisha kuwa Ajib anataka vita dhidi ya wapinzani wake hao, Simba iipindue Yanga kuwa bingwa na kama atafunga kila mechi basi anaweza kuwa mfungaji bora na kuchukua tuzo ambayo inashikiliwa na Tambwe kwa sasa.
Kutokana na ushindi wa Simba, sasa imeshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba sawa na Azam FC na Mbeya City ambapo timu zote zimecheza michezo mitatu.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Ajib alisema kuwa hafikirii suala la kuibuka mfungaji bora wa ligi kuu zaidi ya kuhakikisha anafunga katika kila mchezo kwa lengo la kuipa ushindi timu yake ili iweze kufikia malengo waliyojiwekea msimu huu.
“Kiukweli sifikiri kitu chochote kuhusu suala la ufungaji bora kwa sababu nataka kuisaidia timu yangu ifikie malengo, huo ufungaji bora unaweza kuja tu kama ziada lakini zaidi nataka kuhakikisha nafunga katika kila mchezo nitakaocheza ili kutimiza hilo.
“Ushindani upo, hilo lipo wazi kwa sababu kila timu inacheza kwa kujituma kwa ajili ya kutafuta matokeo halafu ukiangalia ligi ndiyo kwanza imeanza, huwezi kusema fulani atakuwa bingwa wakati huu labda itakapofika katikati hapo bingwa anaweza kujulikana ila kwangu naona kufunga mabao ndiyo kitu muhimu,” alisema Ajib.
Alipotafutwa Tambwe kuzungumzia ushindani huo wa mabao na mbio za kuelekea kwenye ubingwa alisema: “Sipo sehemu nzuri siwezi kulizungumzia hilo, nitakutafuta baadaye.”
