Mwanzilishi na Mkurugenzi wa taasisi ya Impact Afya, Bhakti Shah (katikati) akizungumza na wanahabari.
Mshauri wa Masuala ya Afya Impact Dkt. Samuel Mwenda (wa pili kushoto) akifafanua jambo baada ya mkurugenzi wa taasisi hiyo kuzungumza. Pembeni mwake ni baadhi ya mabalozi wa taasisi hiyo.
TAASISI ya ImpactAfya ya jijini Dar es Salaam inayojihusisha na masuala ya kusimamia na kufuatilia watu kufanya mazoezi chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Bhakti Shah, imewaasa Watanzania kuwa na uzalendo wa kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa hatari kama shinikizo la damu.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na mkurugenzi huyo alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusiana na tamasha lao waliloliandaa la kufanya mazoezi litakalofanyika Oktoba 8 mwaka huu kwenye viwanja vya Golden Tulip Oyster Bay kuanzia saa kumi hadi saa moja usiku Dar.
Alisema katika ripoti iliyochapishwa hivi karibuni kupitia Shirika la Moyo la Marekani lilieleza kwamba mabadiliko ya kiuchumi yaani teknolojia na watu kuhamia mijini, ustawi wa viwanda na kuenea kwa biashara za kimataifa huleta mabadiliko katika mitindo ya maisha ambayo huchangia watu wengi kukumbwa na ugonjwa wa moyo.
Aliongeza kwamba ripoti hiyo inaeleza sababu kubwa kuwa ni kutokana na idadi kubwa ya watu kutofanya mazoezi ya mwili na kula vyakula visivyofaa.
Alieleza kuwa njia nyingine inayoweza kuchangia mtu kupatwa na shinikizo la damu ni pale mtu anapokaa kwenye kompyuta kwa muda wa zaidi ya saa tano akifanya kazi na baada ya hapo kuelekea nyumbani pasipo kufanya mazoezi.
Amewaomba Watanzania, mashirika na makampuni kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika mazoezi hayo yanayojulikana kama ‘Movement to Fitness’ ili kuliokoa taifa ambapo kiingilio kitakuwa shilingi elfu ishirini. Pia kutakuwa na huduma mbalimbali ikiwemo ushauri.
Na Denis Mtima/Gpl.