Ajibu Awatetemesha Chama, Kahata

KUTUA kwa aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu Simba kutawapa ugumu wa namba viungo wenzake Mkenya, Francis Kahata na Mzambia, Clatous Chama kwenye timu hiyo.

 

Ajibu na Kahata wote walijiunga kwa pamoja kwenye msimu huu wa ligi kama wachezaji huru baada ya kumaliza mikataba na klabu zao walizokuwa wanazichezea.

 

Kutua kwa Ajibu kutaleta ushindani mkubwa kutokana na wote kucheza nafasi sawa za viungo washambuliaji namba 7, 11, pia 10 ambayo ni ngumu kwa viungo kutoka na na ujio wa mshambuliaji wa TP Mazembe, Deo Kanda.

Kwa mujibu wa mfumo anaoutumia Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems viungo hao mmoja wapo kati ya hao watatu ni lazima aanzie benchi kutokana na aina zao za uchezaji kuendana. Mfumo ambao anapenda kuutumia Aussems ni 4-5-1 huku akiwatumia viungo wawili wakabaji na siyo wachezeshaji kama ilivyokuwa msimu uliopita alikuwa akimtumia Mghana, James Kotei kucheza namba 6 na Jonas Mkude 8 huku mawinga wa pembeni wakiwa ni Chama na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima aliyetimkia AS Kigali ya Rwanda.

 

Hivyo, kocha huyo atakutana na changamoto ya kupanga kikosi kwa kuamua nani aanze katika kikosi cha kwanza, licha ya Chama kuwa na nafasi kubwa ya kuanza kutokana na kuwepo kwenye msimu uliopita uhakika huo aliokuwa nao Chama, bado anahitajika kuonyesha kitu cha tofauti kwani Ajibu na Kahata wataleta kitu kipya katika timu hiyo inayoundwa na mafundi wengi wenye uwezo wa kupiga pasi, kumiliki mpira na kutengeneza nafasi za mabao. Ajibu huenda rekodi yake aliyotoka nayo Yanga ya kupiga asisti 17 huku akifunga mabao 6 ikambeba na kocha kumuamini na kumpa nafasi ya kuanza katika kikosi cha
kwanza.

 

Kocha na mchezaji wa zamani, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ hivi karibu alisema kuwa “Hakuna mchezaji wa kumuweka benchi Ajibu Simba, licha ya usajili wa wachezaji wengi wa kigeni wenye uwezo.

 

“Labda Ajibu mwenyewe asitake kucheza, lakini kama akiamua kucheza, basi atacheza hadi atakapochoka mwenyewe, kwani huyo ni kati ya viungo wenye ubora hapa nchini,” alisema Julio. Tofauti na viungo hao watatu ndani ya Simba wengine watano wanaotarajiwa kukutana na ushindani ni Mzamiru Yassin, Jonas Mkude, Sharaf Eldin Shiboub, Said Ndemla na Hassani Dilunga.


Loading...

Toa comment