×

Mabao ya Bocco Yaweka Rekodi

WAKATI juzi Jumamosi Simba ikiibuka na ushindi mnono wa mabao 0-7 dhidi ya Coastal Union, nahodha wa kikosi hicho, John Bocco aliweka rekodi ya kipekee kupitia mabao yake matatu. Simba juzi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, iliibuka na ushindi huo ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara.

 

 

Katika mchezo huo, Bocco aliweka rekodi ya kufunga mabao matatu ʻhat trickʼ akitumia dakika 13 tu ikiwa ndiyo hat trick ya mapema zaidi msimu huu. Bocco alifunga dakika ya 24, 28 na 37.

 

Ikiwa hiyo ni hat trick ya pili msimu huu kupatikana baada ya ile ya Adam Adam wa JKT Tanzania, lakini ya Bocco ndiyo ya mapema zaidi na kumfanya kuweka rekodi. Oktoba 25, mwaka huu, Adam alifunga hat trick katika ushindi wa 6-1 walioupata dhidi ya Mwadui huku akitumia dakika 58 kuikamilisha. Alifunga dakika ya 24, 48 na 82.

 

 

MCHEZO ULIVYOKUWA

Kiungo wa Simba, Hasan Dilunga, alikuwa wa kwanza kufunga bao dakika ya saba. Bao hilo lilionekana kulalamikiwa na wachezaji wa Coastal Union wakidai kuwa aliotea. Bocco akafunga dakika ya 24, 28 na 37 na kumfanya kuwa na mabao saba ndani ya ligi akiwa kinara. Katika mabao hayo, Ibrahim Ajibu alitoa asisti moja ikiwa ni ya kwanza kwake ndani ya ligi hiyo msimu huu.

 

Mabao mengine yalifungwa na Bernard Morrison dakika ya 45+2 na Clatous Chama dakika ya 59 na 85 ambaye sasa ana jumla ya mabao manne kwenye ligi hiyo.

 

Morrison alirejea ndani ya uwanja na utamu wake baada ya kufungiwa mechi tatu pamoja na adhabu ya 500,000 kutokana na kitendo cha kumpiga beki wa Ruvu Shooting, Juma Nyosso.

 

Kiungo huyo juzi alianza kwenye kikosi cha kwanza na kuifanya Simba kuwa timu ya kwanza kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi kwa msimu wa 2020/21. Mbali na kufunga, alitoa pasi ya bao.

 

 

Kabla ya Simba kuibuka na ushindi huo wa juzi, JKT Tanzania ilikuwa ya kwanza msimu huu kupata ushindi mnono wa mabao 1-6 dhidi ya Mwadui katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Mwadui, Shinyanga.

 

Baada ya mchezo, Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda, alisema: “Tumefanya makosa yametugharimu, hatuna wa kumlaumu ingawa kikosi changu baada ya kuondokewa na wachezaji takribani sita, kimekuwa dhaifu.”

 

SALAMU KWA WANIGERIA

Ushindi huo wa Simba ni kama salamu kwa wapinzani wao, Plateau United ya Nigeria ambayo watapambana nayo mwishoni mwa wiki ijayo katika mechi ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayochezwa nchini Nigeria kabla ya kurudiana jijini Dar kati ya Desemba 4-6, mwaka huu. Simba inatarajiwa kwenda Nigeria Jumatano ijayo. Matokeo ya mechi zingine juzi; Polisi TZ 0-0 Ihefu, KMC 1-0 Azam, JKT TZ 0-2 Gwambina.

 

MUSA MATEJA, Arusha

Leave a Comment