Barnaba Afunguka Mama Steve Kuolewa!

KWENYE listi ya wanamuziki wazuri wa Bongo Fleva wanaojua kuimba, kutunga, kutumia vyombo na kuzalisha (produce) ngoma kali, huwezi kuacha kutaja jina la Elias Barnabas, muite Barnaba Boy ‘Classic’.

 

Barnaba ni zao la Tanzania House of Talent (THT). Amesikika kwenye midundo na melodi tamu za Ngoma za Washa, Tuachane Mdogomdogo, Sichomoi, Lover Boy, Mapenzi Jeneza, Tunafanana, Nyang’anyang’a, Milele Daima, Bembeleza, Ngoma akiwa na Aslay na nyingine kibao. Mwenyewe anasema ana miaka 17 kwenye gemu la Bongo Fleva.

 

Barnaba anasema aliyegundua kipaji chake kwenye muziki ni mama yake mzazi.

Lakini baada ya hapo, alikwenda THT (Tanzania House of Talent) ambapo alipokelewa na marehemu Ruge Mutahaba. Huyo ndiye mtu ambaye alimpokea na kumlea tangu akiwa mdogo. Anasema Ruge alimsainisha THT kisha akaanza masomo ya muziki.

 

Barnaba anasema THT ina mchango mkubwa kwake ambao hauelezeki wala hauhesabiki maana safari yake ya muziki ilianzia pale. Alifika pale akiwa hajui kitu kuhusiana na muziki, alianza kusoma, kuandika nyimbo kisha alijifunza kucheza na vyombo vya muziki, leo ni mwanamuziki mkubwa Afrika Mashariki.

 

Katika mahojiano maalum (exclusive) na IJUMAA SHOWBIZ, Barnaba anafunguka mengi, kubwa zaidi

ni kuhusiana na kitendo cha mzazi mwenzake, Mama Steve kuolewa na mwanaume mwingine, dondoka nayo;

 

IJUMAA SHOWBIZ: Ghafla tu ngoma yako mpya ya Sichomoi imekuwa gumzo, nini siri ya mafanikio?

Barnaba: Ni ngoma nzuri, mapokeo ni mazuri na ninamshukuru Mungu kwa hilo.

IJUMAA SHOWBIZ: Ukweli ni kwamba, janga la Virusi vya Corona limeathiri mambo mengi hasa kwenye sanaa, kwa upande wako unalizumgumziaje?

 

Barnaba: Corona imemuathiri kila mtu. Janga hili limesababisha anguko la uchumi na kwa upande wa wasanii hali ni mbaya baada ya shoo kuzuiliwa. Cha muhimu ni kumuomba Mungu atuepushe na janga hili.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa sasa tunaona wasanii wengi wamekuwa na mtindo wa kutoa album au EP (albam fupi), kwa upande wako hii imekaaje?

BARNABA: Muda ukifika nitatoa, lakini siyo kwa sasa. Bado sina mpango huo.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Wakati ukiendelea kufanya vizuri kwenye gemu, tumeona mzazi mwenzako (Mama Steve au Zubeda) ameolewa jijini Arusha. Je, unalizungumziaje hilo?

Barnaba: Silijui suala hilo na wala siwezi kuzungumzia kwa sababu halinihusu.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, kwa upande wako mipango ya ndoa imekaaje na mpenzi wako wa sasa?

Barnaba: Mungu akijaalia tutafunga ndoa kwa sababu kuoa ni jambo la baraka, hivyo lazima na mimi nitalifanya tu!

 

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa sasa tunaona wasanii wengi wamejikita kwenye biashara nyingine nje ya muziki ili kuweza kujikimu kimaisha hasa kwa kipindi kama hiki cha Corona. Je, kwa upande wako umebuni biashara gani ya kukuingizia kipato nje ya muziki?

BARN-ABA: Mungu akijaalia nadhani nitawaambia watu kwa sababu nina plani nyingi sana za kufanya.

IJUMAA SHOWBIZ: Vipi kuhusiana na shoo na kolabo za kimataifa?

 

Barnaba: Hakuna shoo wala kolabo za kimataifa kwa sasa kutokana na janga hili la Corona. Cha msingi ni kumuomba Mungu atuepushe na suala hili kwanza ndipo mambo mengine yatakaa sawa.

IJUMAA SHOWBIZ: Kufuatia janga hili la Corona wasanii wengi lazima watapoteza mashabiki, kwa upande wako umejipanga vipi kuhakikisha hupotezi mashabiki au kushuka kisanaa?

 

BARNABA: Cha muhimu ni kufanya muziki mzuri. Pia mimi huwa nafanya Insta Live, naongea na mashabiki wangu na tunaongea mambo mengi hivyo hiyo ni njia moja ya kulinda mashabiki zangu. Pia nina studio yangu nyumbani, ninafanya mambo yangu nyumbani, naposti YouTube, naamini bado wananifuatilia.

 

IJUMAA SHOWBIZ: Muziki wa sasa una ushindani mkubwa, je, unafanyaje kuhakikisha hushuki?

BARNABA: Kwa mimi wala ushindani haunishtui kwa sababu najua ninachokifanya. Pia mashabiki wangu wanainjoi kwa kile ninachowapa.

IJUMAA SHOWBIZ: Una lipi la kuwaambia mashabiki wako?

BARNABA: Ninawashukuru, naomba tuendelee kusali sana kipindi hiki, tufanye maombi sana na kingine nawapenda mno hivyo wazidi kunisapoti maana bila wao, Barnaba siyo kitu.

MAKALA: KHADIJA BAKARI

 

 

Toa comment