The House of Favourite Newspapers

BreakingNews: IGP Sirro Aanza na Mauaji Rufiji, Kibiti na Ikwiriri Mkuranga, Asema Ubaya Ubaya Tu!

1

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro amesema moja ya majukumu yake makubwa atakayoanza nayo ni kumaliza mauaji yanayofanywa huko Rufiji, Kibiti, Ikwiriri na Mkuranga mkoani Pwani

Sirro alikuwa akizungumza kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku mbili tangu Amiri Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli amuapishe kuwa IGP.

Sirro amesema suala la mauaji kwa viongozi wa serikali za mitaa yanayofanywa na mkoani humo ni jambo la muda mfupi ambalo litapatiwa majibu sahihi karibuni.

“Wanahabari niseme tu kwamba nchi yetu ni shwari, hatuna matukio makubwa ya kutisha, lakini changamoto kubwa ni Mkoa wa Pwani ambako baadhi ya raia wema wameuawa bila sababu, kuna kikundi cha watu wachache wanaodhani wanaweza kuufanya ule mkoa kukosa amani. Lakini haki lazima itatoa majibu.

“Niwahakikishie Watanzania kwamba suala la Ikwiriri, Mkuranga na Rufiji ni la muda mfupi, viongozi wangu wamezungumza; ukianza na Rais (Dkt. John Pombe Magufuli), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (Mwigulu Nchemba) hivyo mimi sina la kuzungumza zaidi ya kufanya kazi kwa weled,” alisema Sirro.

Aidha aliwaonya wanaofanya uhalifu huo kwamba watajibiwa kwa ubaya kwa mujibu wa sheria.

Mkuu huyo wa polisi pia aliwataka raia kutii sheria bila shuruti na kusisitiza kuimarisha vita dhidi ya madawa ya kulevya.

Alisema kwamba utii wa sheria ni pamoja na raia kutochukua sheria mikononi ambapo watu wanaotuhumiwa uhalifu wafikishwe mahakamani.

Kuhusu uadilifu katika jeshi la polisi, alisema askari atakayejihusisha na rushwa hatabaki salama na alisema ametoa maelekezo kwa jeshi polisi kuwa atakayefanikisha kupatikana kwa wala rushwa atapata zawadi.

Sirro pia ameahidi kutoa shilingi milioni 10 kwa raia mwema atakayetoa taarifa sahihi kwa watu wanaofanya mauaji mkoani  Pwani.

 

Akijibu swali kuhusu anavyoweza kukabili uhalifu nchini kutokana na uchache wa askari waliopo, alisema atatumia askari haohao waliopo ambao watafanya kazi kwa weledi mkubwa zaidi.

Kuhusu chanzo cha mauaji hayo ya Pwani, alisema jeshi lake litapita litapita kwa wananchi wa sehemu hisika na kujua iwapo kuna vibaraka miongoni mwao wanaounga mkono mauaji hayo.

“Tutaangalia  jinsi ya kufanya kwa sababu tusipoaminiana kazi itakuwa ni ngumu, si muda mrefu tutapita kuzungumza na wananchi na tunajua kuna vibaraka watakuwepo,” alisema Sirro.

Akijibu swali kuhusu anawapa muda gani wananchi ili kuleta amani sehemu husika na iwapo angeshirikisha Jeshi la Wananchi katika shughuli zake, alisema jeshi lako lina mipango thabiti ya kukabili hali hiyo.

“Kuzungumza habari ya kushirikisha jeshi mimi sio mzungumzaji wa Jeshi la Wananchi lakini ninachosema, vyombo vyote tunafanya kazi kwa pamoja. Sisi wote amiri jeshi mkuu ni mmoja na mimi nazungumzia Jeshi la Polisi, habari ya kushughulisha jeshi la wananchi muulize CDF atalieleza,|” alisema Sirro.

TAZAMA VIDEO AKIZUNGUMZA

1 Comment
  1. […] BreakingNews: IGP Sirro Aanza na Mauaji Rufiji, Kibiti na Ikwiriri Mkuranga, Asema Ubaya Ubaya Tu! […]

Leave A Reply