Freeman Mbowe Afungua Mkutano Mkuu Chadema, Akemea Matusi, Asema Uchaguzi Huo sio Vita

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amewasihi viongozi watakaoshika nyazifa mbalimbali katika Chama hicho ni lazima wakijenge chama katika misingi ya maadili na Nidhamu.
Ameyasema hayo leo Januari 21, 2025 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa chama hicho unapendelea Mlimani City jijini Dar es Salaam.
“Mtakaopewa mikoba ya chama hiki ni lazima mkarekebishe, inawezekana tukavumilia matusi kipindi hiki cha chaguzi lakini msingi wa Chadema sio matusi watakaokabidhiwa mikoba leo wakasafishe”
“Hiki chama tunawajibu wote wa kukilinda kwa gharama yoyote ile na chama hiki tutakilinda”. Ameongeza.
Amesema kuwa Chadema kitamaliza uchaguzi wakiwa wamoja na kwamba uchaguzi huo sio vita.
“Uchaguzi huu haupaswi kuwa vita unapaswa kuwa ujenzi ya Demokrasia, Wapo watabiri wengi walisema kuhusu Chadema , Mheshimiwa Mbowe mnakwenda kukipasua Chadema ” amesema Mbowe.
Amesema kuwa Chadema kimebeba Ndoto ya Taifa sio Ndoto ya kiongozi mmoja mmoja na wataendelea kupita katika mabonde na milima lakini kila mmoja awe na wajibu wa kukilinda Chadema na njia ya kukilinda ni kuwa na hekima na Nidhamu.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)- Bara Tundu Lissu amesema pamoja na kutofautiana na Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe kwa misimamo lakini hawajawahi kugombana.
Hayo ameyasema leo wakati akitoa Salamu zake kabla ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa chama hicho, ambapo amesema wanaweza kuwa wametofautiana kimsimamo lakini hawajawahi kugombana.
Amesema uamuzi wowote utakaofanywa na wajumbe wa chama hicho ni sehemu ya ujenzi wa chama naye ni muumini wa ujenzi wa chama hicho . “vyovyote itakavyokuwa leo nitakuwa mmoja wa kujenga chama chetu.”