Irene Sanga Sikumpenda JK Lakini JPM Kanishika

Msanii wa muziki ambaye alivuma sana baada ya Wimbo wa Salamu kwa Mjomba,  Irene Sanga.

 NA HAMIDA HASSANI | IJUMAA | MAKALA

KWA wafuatiliaji wa masuala ya burudani Bongo, jina la Irene Sanga litakuwa siyo geni masikioni mwao. Huyu ni msanii wa muziki ambaye alivuma sana baada ya Wimbo wa Salamu kwa Mjomba wa Mrisho Mpoto kutoka. Alivuma kwa kuwa yeye ndiye mtunzi wa wimbo huo.

Mdada huyu ni msanii wa maana halisi ya msanii lakini hapo katikati akajiweka pembeni kidogo na kufanya mambo mengine.

Rais wa sasa, Dk. John Pombe Magufuli.

Hivi karibuni mwandishi wetu alipata bahati ya kumnasa, akazungumza naye mambo mengi anayofanya kwa sasa lakini kubwa aligusia tofauti kubwa iliyopo kati ya rais wa sasa, Dk. John Pombe Magufuli na aliyepita, Jakaya Mrisho Kikwete na kufikia hatua ya kuanzisha kundi la WhatsApp alilolipa jina la Viva Magufuli. Kuhusu Kikwete hebu msikie anachosema; “Kiukweli sikuwahi kumpenda, hili nalisema kutoka moyoni mwangu. Alikuwa mpole sana na ikawafanya wengine kumchukulia poa.

Msanii Mrisho Mpoto.

Utakumbuka pale ikulu wasanii walikuwa wakienda kwa sana, mimi sikuwa nikipenda ile. Kwa hiyo kuna mambo ambayo alikuwa akiyafanya yalikuwa hayanipendezi ndiyo maana sikutokea kumpenda. “Si kwamba nina chuki binafsi, hapana! Na utakumbuka hata nyumbani kwake wengi walikuwa huru kwenda, aliongea na kila mtu, mcheshi. Hicho ndicho kilinifanya nikamtungia ule Wimbo wa Salamu kwa Mjomba baada ya yeye kuingia madarakani na nyimbo nyingine mbili za kuikosoa serikali yake ambazo baadhi ya media ziliogopa kuzipiga.

“Kiongozi mzuri anatakiwa kuwa ‘nyutro’, yaani usiwe dikteta, wala mtu wa demokrasia sana. Hiyo sikuipata kwa Kikwete. Hata hivyo, sikupata tatizo lolote kipindi cha utawala wake, maisha yaliendelea kama kawaida.”

AMKUBALI MAGUFULI

“Kwa sasa namkubali sana Magufuli, nilimpenda Magufuli toka alipokuwa Waziri wa Ujenzi kutokana na utendaji wake. Alipoingia kwenye kinyang’anyiro cha urais ndipo na mimi nikajipanga kupiga kura. “Na kwa kweli siku ya uchaguzi nikaenda kupanga foleni, lengo likiwa ni kumpigia kura yeye na hatimaye akaingia madarakani. “Anachokifanya sasa kinanifanya niendelee kumkubali. Namkubali na namuelewa kwa kila hatua anayopiga kuelekea kuinyooshanchi.

Rais aliyepita, Jakaya Mrisho.

MAGUFULI AKISEMWA ANAKONDA

Irene anaeleza kuwa, kwa namna anavyoona Magufuli anapiga kazi, akisikia baadhi ya watu wanamsema vibaya anakonda. Na kutokana na kumuelewa vizuri kiongozi huyo, alijiwa na wazo la kuanzisha kundi la wanaomuelewa Magafuli na kulipa jina la Viva Magufuli.

LENGO LA VIVA MAGUFULI

Msanii huyo ambaye kwa sasa ni mwanafunzi katika Chuo cha Afya Muhimbili jijini Dar akisomea masuala ya Ustawi wa Jamii anaeleza kuwa, aliamua kuanzisha grupu hilo baada ya kuona kuwa, huenda wapo wengi wanaomuelewa Magufuli na ni vyema wakajuana ili kumpa sapoti katika kupambana kwake.

WAZO LILIKUJAJE?

“Siku moja nikiwa na Mrisho Mpoto tukijadiliana mambo mbalimbali ya kisiasa, aliniuliza; Hivi ni mimi na wewe tu tunaomuelewa Magufuli?’ Tulihisi tuko wengi na ndipo nikaanzisha grupu hilo kwenye Mtandao
wa WhatsApp na leo hii tuko wengi kiasi kwamba inatupa nguvu ya kuendelea kumuunga mkono.

WANACHOFANYA KWA SASA

“Tumeamua kukutana kutambuana kwanza kisha tumepanga mikakati ya namna tunavyoweza kumsapoti rais wetu na tuna mpango wa kufanya jitihada za kuwafikia wale ambao bado hawamuelewi. “Tutakuwa tunaendesha mijadala kila mkoa hasa kwa wale wanaoonekana kupinga anachokifanya na tutawaelewesha kwa ‘facts’ na kila atakayekuwa anapinga akija na ‘facts’ zake na sisi tunamuelewesha kwa ‘facts’.

“Lengo si kutukana, wale watakaokuwa na nia ya kutukana tutaachana nao kwani katika grupu hili hakuna siasa wala chama, wewe kama upo Chadema, upo CUF ilimradi unamuelewa Magufuli basi unaruhusiwa kujiunga. “Mimi nimeamua kujichagua kuwa kiongozi kwenye hili, nitahakikisha nafanya kazi ya kujitolea ili watu wamuelewe. Wewe umeona ameweza kufanya mambo makubwa kwa muda mfupi kama vile kutumbua majipu mbalimbali serikalini moja likiwa ni mfano kwa wenye vyeti feki, kuimarisha utawala bora, rushwa imepungua na mengineyo ambayo huko nyuma hayakuwahi kufanywa.

VIVA MAGUFULI NI AKINA NANI?

Kundi hili linajumuisha watu wa kawaida na baadhi ya mastaa. Mastaa waliomo ni pamoja na Steven Jacob ‘JB’, Chiki Mchoma, Mrisho Mpoto, Kelvina John, Masoud Kaftan, Faiza Omary ‘Sister Fay’, Luckiness Mokiwa, Vanitha Omary na wengineo.

IRENE SANGA NI NANI?

Ni msanii wa muziki anayeandika na kuimba, amewahi kutunga nyimbo kama Pangisheni, Utandawazi na Salamu kwa Mjomba. Ana albamu yake yenye nyimbo saba. Mbali na nyimbo pia ni mwandishi wa filamu ambapo amewahi kupata tuzo mbalimbali za Zanzibar International Filim Festival ‘Ziff’ kupitia filamu alizoandika za Mikono Salama, Utakapokucha na Chungu cha Tatu.

Loading...

Toa comment