The House of Favourite Newspapers

Kisa sare, Yondani ajifungia aangua kilio

WACHEZAJI wa Yanga wakiongozwa na beki mkongwe, Kelvin Yondani, juzi walijikuta wakimwaga machozi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo. Tukio hilo la aina yake lilitokea mara baada ya mchezo
wa Ligi Kuu Bara kumalizika kwa Yanga kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Polisi Tanzania.

 

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Yanga ndiyo waliosawazisha baada ya kuwa nyuma kwa mabao 3-1 na mwisho matokeo kuwa 3-3.

 

Mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Ditram Nchimbi alipiga hat trick huku mabao ya Yanga yakifungwa
na Mrisho Ngassa na David Molinga aliyefunga mawili.

 

Taarifa ambazo Championi Jumamosi limezipata, baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ndiyo walimwaga machozi kufuatia matokeo hayo. Mtoa taarifa huyo alisema, wachezaji hao walikasirishwa na matokeo hayo ambayo hawakuyatarajia.

 

Aliwataja baadhi ya wachezaji waliomwaga machozi ni Yondani, Juma Abdul na Ngassa.
“Ujue wachezaji wamelia kwa mengi sana, moja ni kutoka sare ya mabao 3-3 na timu ya kawaida, tena nyumbani.

 

“Kingine ni kitendo cha timu yao kupata matokeo mabaya kunasababisha wao wasipate zile posho kutoka kwa mashabiki wa Yanga na viongozi, hivyo katika mchezo huo walitarajia matokeo mazuri ya ushindi ambayo kwao hawakuyapokea vizuri na ndiyo sababu ya wao kuanza kulia,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Ngassa alizungumzia hilo kwa kusema: “Wote tulitarajia ushindi na ndiyo sababu ya wachezaji kupata uchungu na kufikia hatua hiyo.

 

“Kama wachezaji tumeumia lakini tunajipanga kwa ajili ya michezo ijayo na kikubwa ni kupata matokeo mazuri ya ushindi na siyo kitu kingine,” alisema Ngassa.

Comments are closed.