The House of Favourite Newspapers

Mil 300 Zatengwa Kumung’oa Mwakifwamba Urais Bongo Muvi

0
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba.

Na Gladness Mallya | AMANI |Dar es Salaam

Wakati mambo yakizidi kupamba moto kutokana na maandamano yaliyofanywa hivi karibuni na baadhi ya wasanii wa Bongo Muvi wakipinga uuzwaji wa filamu za nje hapa nchini, habari mpya kwa sasa ni milioni 300 zinazodaiwa kutengwa kwa ajili ya kumng’oa kwenye nafasi ya Urais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba.

Chanzo makini kililiambia gazeti hili kuwa, suala la filamu za nje kupigwa marufuku limewagawa wasanii wa filamu kwani kuna wanaokubali na wengine hawakubali ambapo kwa upande wa wasiokubali yumo pia Mwakifwamba hivyo kuonekana kuwa msaliti kwani mwanzoni wakati wa kuandika barua kuomba serikali iwasaidie, yeye ndiye aliyeongoza harakati hizo.

Chanzo hicho kilieleza kuwa, baada ya baadhi ya wasanii kupanga maandamano, Mwakifwamba alikataa kushiriki na kuwataka na wao waachane nayo kwa sababu ishu hiyo ilionekana ni ya kisiasa, jambo ambalo liliwakasirisha wasanii hao na sasa kuna milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya kumuondoa kwenye uongozi.

“Kuna mtu nyuma ya wasanii walioandamana ametenga shilingi milioni 300 kuhakikisha wanamtoa madarakani Mwakifwamba. Chama cha Waigizaji Tanzania kimemwandikia Mwakifwamba barua na kumpa siku 30 awe ameshaitisha mkutano mkuu wa dharura ili ajieleze, vinginevyo wanamtoa kwenye nafasi hiyo,” kilisema chanzo hicho.

Baada ya kupata habari hizo, gazeti hili lilimtafuta Mwakifwamba ambaye alikiri kwamba kuna wasanii wawili ambao wamepewa viwanja Mbweni, nje kidogo ya Jiji la Dar (hakuwataja) ili wahakikishe wanamuondoa madarakani. Pia Mwakifwamba alikiri kutengwa kwa shilingi milioni 300 ili kuhakikisha anaondoka.

“Najiuliza kwa nini hizo fedha za kuniondoa wasizitumie kwa ajili ya kuwasaidia wasanii ili filamu isonge mbele? Mimi nasema hivi, siwezi kuona tasnia ikifa kwa sababu ya watu wachache wanaotetea masilahi yao binafsi.

“Kuna mgawanyiko mkubwa sana kwenye tasnia ya filamu, wapo wanaotaka maendeleo, wapo wapiga dili wenye mitazamo ya kisiasa, ninachosema ni hivi, tasnia hii siyo sehemu ya kuwasafisha watu waliopoteza mvuto, hatuwezi kuona filamu inakufa kwa ajili ya wanasiasa, tutapambana mpaka mwisho,” alisema Mwakifwamba.

Kuhusu kuandikiwa barua ya kuitisha mkutano wa dharura ili ajieleze, Mwakifwamba alisema: “Wao wameandika barua, basi wasubiri huo mkutano, kama kunitoa sawa, wao si wanaijua katiba vizuri, sitaki kuzungumza sana.”

 MSIKIE MWENYEKITI WA CHAMA CHA WAIGIZAJI TANZANIA

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania, Elia Mjata alikiri chama chake kumwandikia Mwakifwamba barua ya kuitisha mkutano mkuu wa dharura wa wanachama ili akaeleze kwa nini aliwageuka kwenye mapambano hayo.

“Mwakifwamba tumeshamwandikia barua kuwa ndani ya siku 30 awe ameitisha mkutano wa dharura ili atueleze ilikuwaje akatugeuka wakati yeye ndiye aliyetoa ruhusa ya kuandika barua tusaidiwe na serikali lakini baadaye akaja kukataa.

“Tunasubiri, asipofanya huo mkutano tutaenda Basata (Baraza la Sanaa la Taifa) maana ndicho chombo chetu kikuu ili waitishe mkutano baada ya hapo akishindwa kueleza kwa nini, ni bora ajiuzulu mwenyewe na asipofanya hivyo tutamwondoa katika nafasi hiyo ya urais kwa nguvu.

“Sisi tunapigania haki ya kazi zetu, yeye anataka kuturudisha nyuma kwa kukataa kuungana na sisi kwa madai eti kuna siasa ndani yake, je, kupinga filamu za nje zisiuzwe kuna siasa gani hapo? Yaani asipoacha hiyo nafasi mimi nitajiuzulu nafasi hii ya uenyekiti maana hatuwezi kufanya kazi na mtu anayepinga mambo ya maana kwenye tasnia yetu,” alisema Mjata.

 

Mwakifwamba Ayatumbua Makundi 2 ya Siri Yanayoitafuna Bongo Movie

Leave A Reply