The House of Favourite Newspapers

MKE AJIJENGEA KABURI AKIWA HAI!

DAR ES SALAAM: Uchuro? Mwanamke mmoja, mkazi wa Tabata-Kinyerezi jijini Dar ambaye jina halikupatikana mara moja amesababisha watu kupigwa na butwaa baada ya kudaiwa kufanya kitu kinachoweza kuitwa uchuro baada ya kujijengea kaburi akiwa hai ili akifa azikwe jirani na alipozikwa marehemu mumewe.

 

Katika tukio hilo lililojiri wiki iliyopita kwenye Makaburi ya Zimbiri yaliyopo Tabata- Kinyerezi, Dar, mama huyo aliwaeleza watu kuwa alifanya hivyo akihofia kukosa eneo hilo ambalo limeshajaa na Serikali ya mtaa huo imeshawekwa matangazo ya kupiga marufuku kuendelea kuzika hapo.

 

Kitendo hicho kilizua mtafaruku mkubwa kati yake na Serikali ya mtaa huo ambayo ilishazuia kuendelea kuzika katika makaburi hayo huku wakazi wengine wakilalamika kwa nini mwenzao amepata nafasi hiyo wakati wao walishazuiliwa tangu miezi mitatu iliyopita.

 

Kwa mujibu wa chanzo chetu kilichokuwa miongoni mwa mashuhuda wa tukio hilo, wakazi wa eneo hilo walishapigwa marufuku kuendelea kuzika kwenye makaburi hayo, lakini mama huyo alitumia nguvu kujichimbia na kujenga kaburi hilo kwa kuwatumia mafundi wake aliofuatana nao makaburini.

 

Kilidai kwamba, mwanamke huyo alionekana akiwasimamia mafundi waliokuwa wakimuandalia kaburi hilo ambapo alikuwa akiwaelekeza jinsi alivyokuwa akitaka lifanane. Baada ya kuelezwa juu ya jambo hilo, Uwazi lilifika kwenye makaburi hayo na kujionea kaburi hilo huku mhusika akiwa ameshaondoka na mafundi wake.

 

Baada ya kushuhudia hali hiyo, wanahabari wetu walikwenda kwenye ofisi za Serikali ya mtaa huo na kuonana na Mjumbe wa Serikali ya Mtaa, Deogratius Malima ambaye baada ya kuulizwa taarifa za kaburi hilo alianza kwa kukataa kuwa hakuna kaburi linalochimbwa eneo hilo.

 

Aliposisitiziwa na wanahabari wetu kuwa maandalizi ya kaburi hilo yanaendelea sehemu hiyo ambayo wakazi wengine wa eneo hilo wamepigwa marufuku kuendelea kuzikia, Malima aliwaambia waongozane wakajionee.

 

Walipofika kwenye makaburi hayo, mjumbe huyo na wanahabari waliwakuta vijana wanaofanya kazi mbalimbali kama kusafisha makaburi na kuyajengea, walimwambia Malima kuwa mwanamke huyo na waliokuwa wakimchimbia kaburi hilo walishaondoka.

 

“Hili kaburi alikuja mwanamke mmoja na wachimbaji wake, wakalichimba wakisema huyo mwanamke anataka azikwe pembezoni mwa kaburi la mumewe na alikuwa akiwaelekeza hao wachimbaji wake jinsi alivyokuwa akitaka,” alisema mmoja wa vijana waliokutwa kwenye makaburi hayo.

 

Akizungumza na wanahabari wetu, Malima alisema kuwa, uongozi wa Serikali ya mtaa huo ulishapiga marufuku kuzika eneo hilo na hakuna mtu yeyote anayeweza kupata nafasi hiyo kwa njia ya kinyemela na hana taarifa za mwanamke huyo aliyejiandalia kaburi hilo.

 

“Huyo mwanamke sina taarifa zake ndiyo naambiwa hapa na hawa vijana, lakini nitamsaka na ikiwezekana hili kaburi tutalifukia kwa kuwa tumeshapiga marufuku kuzika na tumeshaweka vibao kila kona vya kupiga marufuku kuzika hapa.

 

Hata hivyo, Malima aliwasiliana na mwenyekiti wake kwa njia ya simu ambaye alikuwa safarini ili kujua kama anazo taarifa za mwanamke huyo ambapo katika maongezi yao, mwenyekiti alisema hana taarifa za mwanamke huyo hivyo ikiwezekana kaburi hilo lifukiwe.

STORI: RICHARD BUKOS NA ZAINA MALOGO, UWAZI

Comments are closed.