The House of Favourite Newspapers

Mwigizaji Huyu Bilionea Ana Neno la Utajiri Kwako

Johnny Depp

Na NYEMO CHILONGANI & MTANDAO| IJUMAA WIKIENDA| MAKALA

KATIKA ulimwengu wa sasa, unapozungumzia watu walioingiza kiasi kikubwa cha fedha kupitia vipaji vyao, Johnny Depp ni miongoni mwao. Jamaa amekuwa kivutio kikubwa katika filamu zake. Depp amezaliwa mwaka 1963 huko Owensboro, Kentucky nchini Marekani.   

Mbali na umaarufu, Depp ana utajiri mkubwa pamoja na kwamba ametoka kwenye familia ya kawaida sana. Mama yake, Betty Sue alikuwa mhudumu katika hoteli moja huko Kentucky na baba yake alikuwa injinia ambaye hakulipwa kiasi kikubwa cha fedha.

Depp alipenda sana muziki na alipokuwa na umri wa miaka 15, mama yake alimnunulia gitaa na kumwambia afanye muziki, kitu alichokuwa akikipenda sana hivyo alijiunga na vijana wenzake na kuunda bendi ya muziki wa Rocky waliyoipa jina la The Kids.

Miaka ilisonga Depp akiwa na bendi hiyo, hawakuwa na mafanikio makubwa mpaka pale bendi hiyo ilipovunjika. Alichokifanya ni kumuoa dada wa rafiki yake waliyekuwa kwenye bendi moja, msichana mrembo aitwaye Lori Anne Allison.

Johnny Depp

Huyo ndiye mtu aliyeyabadilisha maisha yake na kuingia kwenye uigizaji kwani alimwambia wazi kwamba, muziki waliokuwa wakiufanya haukuwa ukilipa na lingekuwa jambo jema kama angeachana nao na kuwa muigizaji. Hivyo alichokifanya mkewe ni kumtambulisha kwa Muigizaji Nicolaus Cage aliyemchukua na kuanza kumfanyia mipango ya uigizaji.

Hakutegemea kwamba huko ndipo angetokea kwani kabla ya hapo aliamini muziki ndicho kilikuwa kipaji chake. Lakini baada ya kuingia kwenye filamu, alifanya vizuri mno na kujikuta akiwa bilionea mkubwa. Filamu yake ya kwanza kuigiza ilikwenda kwa jina la A Nightmare On Elm Street ya mwaka 1984.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa Depp uliompa umaarufu na kuonekana anafaa kuwa muigizaji hivyo waongozaji wengi kumchukua na kufanya naye kazi mbalimbali ambazo zilimpa fedha na kuwa bilionea mkubwa. Anapokuwa akiitwa katika vipindi mbalimbali vya televisheni kuzungumza kuhusu mafanikio, huwa anazungumza maneno mengi lakini yale makubwa zaidi huyaweka wazi ambayo huamini kwamba kama k ijana unayetafuta mafanikio ni lazima uyafuate;

JIAMINI Depp anasema kwamba watu wengi wame- kuwa hawajiamini. Wana uwezo mkubwa wa kufika sehemu f’lani kama watu wengine lakini tatizo ni kwamba hawataki kujiamini kama wanaweza. Kuna watu wengi wana vipaji mitaani, wengine waigizaji, wengine wanamuziki lakini wamekuwa hawajiamini kama wanaweza.

Yeye alikuwa mwanamuziki, aliamini kwamba ndicho kilikuwa kipaji chake, alipoambiwa kuhusu kuigiza filamu, kitu cha kwanza kabisa alijiamini, akaona kwamba angeweza kwani haikuwa kazi kubwa sana, kweli akaweza, sasa kwa nini wewe usijiamini na kufanya kitu unachohisi huwezi kukifanya?

HAKUNA MKUBWA ZAIDI YAKO

Depp anasema kwamba kitu kingine ambacho unatakiwa kufanya ni kujiona mkubwa zaidi ya wengine. Hutakiwi kusema kwenye maisha f’lani ni mkubwa zaidi yako, jione wewe ni mkubwa na unaweza kufanya mambo mengi makubwa, ukifanya hivyo, utafanikiwa kwani utahisi dunia nzima inakuangalia wewe kwa kuwa ni mkubwa zaidi ya wengine.

Johnny Depp

HAKUNA ATAKAYEBADILISHA MAISHA YAKO

Depp anafunguka kuwa usimtegemee mtu flani kuyabadilisha maisha yako. Ukitaka kumfahamu mtu atakayeyabadilisha maisha yako, hebu kifuate kioo, kiangalie, yule utakayemuona ndiye mtu pekee atakayeweza kuyabadilisha maisha yako. Usimsubiri mtu mwingine akufuate na kukuambia kwamba unatakiwa kufanya hivi na vile ili ufanikiwe, acha watu hao wakupe njia za mafanikio, ila kwenye utendaji, usitake wakusaidie.

KUWA MBUNIFU

Depp anaendelea kusema kwamba amekuwa kwenye chati kwa kipindi kirefu kwenye filamu kwa sababu yeye ni mbunifu. Katika filamu nyingi alizocheza, amekuwa na muonekano tofauti. Filamu kama Pirates of Carrebean, The Lone Ranger, Black Mass, Dark Shadows, Alice in Wonderland, Public Enemies, In The Woods na nyingine nyingi, amefanya ubunifu wa hali ya juu ambao umependwa na kumfanya kupendwa zaidi. Leo hii jamaa ana utajiri wa zaidi ya shilingi bilioni 800.

Bado anaendelea kuigiza, si maskini kama alivyokuwa kipindi cha nyuma, alipambana, anaendelea kupambana kila siku.

Yeye amefanikiwa kwa kuwa alifanya vitu hivyo ambavyo amevisema hapo juu. Kama yeye alifanikiwa, kwa nini na wewe usianze kufanya ili ufanikiwe? Kwa nini usifanye ubunifu katika kazi yako inayokuingizia fedha? Kwa nini hutaki kuamini kama mtu pekee anayeweza kuyabadilisha maisha yako ni wewe pekee? Unatakiwa kupambana na kujiamini, kila kitu unachokiona mbele yako kione kuwa kidogo na unaweza kukifanya, usitake kuamini kwamba maisha yako yatabadilishwa na mtu f’lani, chukua njia hizo na zifanyie kazi, usisubiri mtu aje na akuambie sasa tuanze kufanya.

Comments are closed.