The House of Favourite Newspapers
gunners X

Polisi Yaonya Mikakati ya Vurugu na Uhalifu Mtandaoni Kuelekea Desemba 9 -Video

0


Jeshi la Polisi Tanzania limesema linachukua hatua madhubuti kukabiliana na wimbi la uhalifu wa kimtandao na mipango ya vurugu inayodaiwa kuhamasishwa kupitia mitandao ya kijamii kuelekea Desemba 9, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Desemba 3, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, DCP David Misime, jeshi hilo limesema limeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda maisha ya wananchi na mali zao, huku likihakikisha amani na utulivu vinaendelea kuimarika nchini.

“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vimekuwa vikifuatilia kwa karibu sana yanayoendelea katika mitandao ya kijamii na kwenye makundi sogozi wakihamasisha wanayoyaita maandamano ya amani yasiyo na kikomo tarehe 9 Disemba 2025”, imeeleza taarifa hiyo.

Polisi imesema wanaohamasishana mtandaoni wamekuwa wakitoa maelekezo hatarishi, ikiwemo kuwaelekeza wanaodaiwa kuwa na mafunzo ya silaha kushika majukumu maalum siku hiyo, kutaka shughuli zote nchini zisimame, kuharibu na kuchoma minara ya mawasiliano ili taifa likose huduma, kufunga barabara zote kuingia na kutoka bandarini Dar es Salaam, kufunga mipaka yote ya nchi, kupora mali za watu kwa kisingizio cha njaa, kuzuia huduma hospitalini, kuwafuatilia watumishi wa serikali na kuwadhuru, kutishia kuwanyonga au kuwakata vichwa watakaoonekana wakishiriki maandamano.

“Huu ni uhalifu mkubwa unaoendelea kuhamasishwa. Hali kama hii kwa nchi yeyote ile dunia ni tishio kubwa la maisha ya watu, uchumi wa nchi na masuala yote ya Kijamii.

Hivyo, Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kwa nafasi zao kuanzia ngazi za familia wawakatae watu kama hawa pamoja na wanayoyahamasisha kwani malengo yao ni kuharibu taifa letu na kuturudisha kwenye machungu na madhara tuliyoyapata tarehe 29/10/2025 na siku zilizofuata”, imeeleza taarifa hiyo.

Leave A Reply