The House of Favourite Newspapers

Sababu 7 Mauaji ya watu 8 Tanga

0

mauaji tanga (1)      

Na Dege Masoli, UWAZI

TANGA: Mauaji ya watu nane katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima, nje kidogo ya Jiji  la Tanga yamefichua mengi ambapo wiki iliyopita, gazeti hili lilitinga eneo la tukio na kuchimbua kisha kuibuka na sababu 7 za watu hao 8 kuchinjwa, Uwazi linakupa zaidi.

TUKUMBUKE KIDOGO

Saa 7 usiku wa Mei 30, mwaka huu, watu wanaodhaniwa kuwa magaidi, walivamia kijiji hicho na kuwakusanya watu nane, wakiwemo viongozi wa kijiji hicho na kuwachinja kwa kuwatenganisha vichwa na viwiliwili.

mauaji tanga (2)Waliokumbwa na unyama huo ni  Mjumbe wa Serikali ya Kijiji, Issa Hussein (50), Mkola Hussein (40), Hamisi Issa (20), Mikidadi Hassan (70), Mahmoud (raia wa Kenya), anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 na 40, Issa Ramadhani (25) na wachunga ng’ombe wawili waliofahamika kwa jina mojamoja la Kadiri na Salum.

Watu hao walikusanywa kutoka nyumba tofauti za Kata ya Kibatini na kupelekwa sehemu moja ambako walichinjwa kikatili na watu hao waliokuwa wameficha sura zao.

mauaji tanga (4)SABABU ZA KUCHINJWA KWAO

 Kwa mujibu wa shuhuda mmoja ambaye ni mwanakijiji aliyekuwa miongoni mwa watu walioamka na kuwafuatilia watu hao kwa karibu mpaka sehemu walipochinjiwa, alisema:

“Nilivyowasikia wale watu wakati wanawapeleka eneo walipowachinjia, walikuwa wakiwalaumu waliochinjwa kwamba walitelekeza kiapo walichowekeana

nao cha kulinda siri ya mpango wa kimkakati wa kunusuru kundi lao ambalo limekusudia kuwatoa wenzao walio kwenye magereza mbalimbali nchini.”

mauaji tanga (5)SABABU YA PILI

“Lakini pia, wale jamaa walisikika wakisema kuwa marehemu waliwachongea vijana wao hadi wakakamatwa na polisi huku wakijua ni watoto wao, kwa maana hiyo marehemu waliamua kuwasaliti. Kwa hiyo wakaona adhabu yao ni kuwaua kwa njia ile.”

mauaji tanga (6)SABABU YA TATU

“Mimi mwenyewe nilijua wakiniona wataniua maana walikuwa wakisema maneno mengi ya kuwalaumu wale. Lakini sababu nyingine niliwasikia wakisema wanawatoa uhai ili mtandao wao usije ukajulikana. Kwa maelezo yao ni kama marehemu waliujua mtandao wao, ndiyo maana wakaamua kuwafuta.”

SABABU YA NNE

“Wakati wanawatoa marehemu majumbani mwao, mmoja alisema kwa vile wao wanajua wanakopatikana (maskani au kijiwe) wanaamini watawaambia polisi ili waende kuwakamata kama walivyowachongea vijana wao.”

mauaji tanga (7)SABABU YA TANO

“Kuna mmoja wa watu waliochinjwa alisikika akisema kwamba, wao hawakujua kama wale vijana waliokamatwa na polisi wanahusiana na wao (hakukuwa na mawasiliano) kwa hiyo walifanya kwa bahati mbaya, ndipo wale wachinjaji, mmoja akasema hakuna kitu kama hicho,” alisema mwanakijiji huyo ambaye aliongeza kuwa mpango wake ulikuwa ni kukihama kijiji hicho baada ya mauaji hayo.

mauaji tanga (3)SABABU YA SITA

Habari za ndani zaidi zinasema kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya watu waliofanya mauaji hayo na wale waliovamia Msikiti wa Mkolani jijini Mwanza katika tukio la  Mei 19, mwaka huu na kuwachinja watu watatu ambao walikuwa wakiswali.

Kwa mujibu wa habari hizo, watu hao waliovamia Kijiji cha Kibatini, Tanga,  mbali na kulipa kisasi lakini sababu yao nyingine ni kuitisha serikali iliyopo madarakani kuhusu wenzao wanaoshikiliwa kwenye magereza mbalimbali nchini wakijihusisha na vitendo vya kigaidi, kwamba wanataka waachiwe mara moja.

mauaji tanga (8)SABABU YA SABA

Aidha, taarifa nyingine zinadai kwamba makundi hayo yanayochinja raia wasio na hatia (Mwanza na Tanga), yamekuwa yakifanya hivyo ili kuongeza hofu katika jamii ya Watanzania popote walipo.

“Wanatumia kutoa roho kwa njia ya kuchinja ili jamii iingiwe na hofu kuhusu wao hivyo watu wawe wanaishi roho mkononi kila siku. Maana sasa hata watu mitaani, majumbani na kwenye nyumba za ibada hawajui nini kitawatokea siku husika,” alisema kiongozi mmoja wa dini ya Kiislam akiomba asitajwe jina gazetini.

MWINGINE ALISEMA HAYA

Akizungumza na gazeti hili huku akikataa kutaja jina lake, mwanakijiji mmoja aliwataja wauaji hao kuwa ni watu waliojitoa maisha yao na

wanaoweza kufanya lolote  kwa kile wanachokiamini kuwa, wanatetea mkakati wao wa kuwakomboa wenzao.

“Unajua  marehemu walikuwa miongoni mwa watu walio kwenye mpango wa kuwakomboa wenzao walio gerezani. Ilikuwa ni siri ya ndani sana, lakini kukamatwa kwa

vijana wao kumewapa hisia za kuvuja kwa siri hiyo.

“Waliamua kuwachinja akina Issa kwa lengo la kuzima kubainika kwa mipango yao hatimaye kuvunjwa mtandao huo kwa vile walikuwa wakiwafahamu,” alisema mwanakijiji huyo.

mauaji tanga (9)MKE SHUHUDA

“Watu hawa walivamia nyumbani na kutuamuru tutoke nje kwa kusema; `toka nje au tunavunja mlango’. Baada ya kugonga sana ndipo mume wangu alipoamua kutoka nje, wakamkamata na kumlaza chini huku wakimkanyagakanyaga tumboni kisha wakamwambia waende naye kwa kaka yake Issa,” alisema Asha ambaye ni mke wa Mkola.

Asha alisema wauaji hao walimchukua mume wake  mpaka kwa kaka yake ambaye pia aliuawa kwenye tukio hilo. Alisema walipofikishwa huko, walianza kuwaulizia vijana wao saba ambao walikuwa wamekamatwa na polisi kwenye eneo la Kibatini hivi karibuni.

Vijana hao walikamatwa na polisi baada ya watu wa eneo la Kibatini kuwashuku nyendo zao na kuamua kuvitaarifu vyombo vya dola.

Asha alieleza kuwa, baada ya kukosa ushirikiano kutoka kwa Mkola na Issa, waliwachinja mbele ya watu waliokuwa wanaishi karibu na Issa.

“Waliwakusanya wote sehemu moja na kuwachinja pamoja lakini kubwa walikuwa wanataka kujua walikopelekwa vijana wao waliokamatwa,” aliongeza Asha.

KAULI YA POLISI, MKUU WA MKOA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa

Tanga, ACP Leonard Paul amekuwa akisema watu wanaofanya matukio ya uhalifu maeneo hayo ni wahamiaji haramu huku Mkuu wa Mkoa, Martin Shigella akisema ni majambazi.

Naye Diwani wa Kata ya Mzizima, Fedrick Chiluba aliliambia gazeti hili kuwa, kuna taarifa kwamba, wahalifu hao wanatoka kwenye Mapango ya Amboni

wakiwa ni wahamiaji haramu na majambazi ambao wamekuwa wakiendesha vitendo vya uhalifu kwa wananchi.

Kwa upande wa tukio hilo, Chiluba alisema usiku huo, watu waliofanya unyama huo walipita nyumba hadi nyumba kuwagongea watu

waliowataka na kuwatoa nje kabla ya kuwapeleka msituni walikowafanyia unyama wa kuwachinja baada ya kuwapanga kwa mstari.

Juzi, gazeti hili lilimpigia simu Kamanda Leonard ili kumsikia anasemaje kuhusu tukio hilo lakini iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

Tayari wakazi wa kijiji hicho wameyahama makazi yao na kwenda kuishi kwa ufadhili maeneo mbalimbali.

MAREHEMU WAZIKWA

Marehemu hao walizikwa katika maeneo mbalimbali

ambapo wawili wamezikwa jijini Tanga, wanne wamezikwa kijijini hapo na wawili walisafirishwa kwenda kuzikwa Kondoa mkoani Dodoma.

WATATU WALIOUAWA MWANZA, WANANCHI WALALA KWA AMANI

Wakati huohuo, polisi mkoani Mwanza wamefanikiwa kuwaua majambazi wawili baada ya kushambuliana kwa risasi na polisi katika mapango ya Mlima Utemini.

 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, SACP Ahmed Msangi aliwataja majambazi waliouawa kuwa ni  Saidi Khamisi Mbuli na mwingine jina lake halikuweza kujulikana mara moja waliopigwa risasi na polisi wakati wa majibizano.

Omari Francis Kitaleti yeye aliuawa na majambazi wenzake hao wakati anakwenda kuonesha walipo.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyipita, walisema kuwa kuuawa kwa majambazo hao kumewapa ahueni ya kulala kwa amani kwani wanaamini juhudi za polisi za kuwatokeza majambazi mkoani humo ndiyo kuwepo kwa amani katika jamii husika.

Leave A Reply