The House of Favourite Newspapers

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (9)

0

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (9)

Nilivuka barabara. Gari dogo likakosa kunigonga. Katika harakati za kukwepa kadhia hiyo, nikaparamia mkokoteni wa takataka. Mwenye mkokoteni japo mimi ndiye nilimkosea, akaamua kuwatukana wazazi wangu ambao hawakuwa mahali pale. Sikujali, lengo lilikuwa kujiokoa. Niliendelea kukimbia.

 

Kila nilipogeuka nyuma, nilimuona mtu wa ajabu akizidi kunikaribia. Nikaongeza mbio ili kujiweka salama. Hata hivyo, kwa sababu ya kukimbia kupita kiasi, mapafu yakashindwa kufanya kazi yake. Nikadondoka kwa kishindo kama furushi, “Puuuh!” fahamu zikapotea.

 

Nilishtuka asubuhi  nikajikuta nikiwa chumbani kwangu. Haya yalikuwa maajabu mengine kwani sikutambua ni nani aliniweka mule ilhali muda uliopita nilikuwa katika tukio la kufukuzwa na yule adui yangu.

 

Sikutaka kubaki mjini tena, nikaamua liwalo na liwe, lazima niende Kigoma kumtafuta Mzee Samike. Nililisogelea kabati chakavu lililojaa vumbi. Panya mkubwa akakimbia kuelekea juu zaidi ukutani ambako alifahamu nisingeweza kumfikia. Sikupata muda wa kumtafakari, nikafungua zipu ndogo ya begi nikatoa kiasi cha fedha ambacho niliamini kingeweza kunifikisha Kigoma na kunisadia katika gharama ndogondogo.

 

Nilimaliza kujiandaa. Nikatoka nikiwa na fulana nyeusi, suruali ya jinsi, viatu vikubwa na kiasi cha fedha kufanikisha safari ya kusaka tiba.

 

Jua halikuonyesha dalili ya kuchomoza, lilipakatwa na mawingu mazito yaliyoifunika dunia. Wingu lile nililiona kama turubai lililoweka matanga. Kama si msiba wangu, ulikuwa msiba wa nani? Sikupata jibu.

 

Nilitembea kwa hatua za kuruta wa jeshi, ‘chap chap’ mpaka nikafika stendi. Hapo nilipokelewa na wapiga debe wengi ambao kila mmoja alinivutia kwake kama ilivyo kwa mwamba ngoma.

 

Sikumsikiliza yeyote. Nilikwenda mpaka ndani ya ofisi ya basi nililotaka, nikakata tiketi, kisha nikazama ndani ya chombo cha usafiri.

 

Nilipokaa juu ya siti, nikapitiwa na usingizi mzito. Kwa muda wa siku kadhaa sikulala vya kutosha. Asili ya maumbile ikanikwapua mzima-mzima. Nikalala kama dume la konokono.

 

Nilishtuka gari likiwa Dodoma. Nikajinyoosha kinyonge tayari kuendelea na safari. Gari ilikwenda kwa mwendo wa kistaarabu. Dereva alikuwa mzee na alizishika sheria zote za barabarani. Kweli utu uzima dawa!

 

Nini hatma ya safari hii ya kusaka tiba? Tukutane kesho…

Leave A Reply