The House of Favourite Newspapers

TFF hakikisheni ligi ya msimu ujao inapata udhamini!

LIGI Kuu Bara inaelekea ukingoni, timu nyingi zimebakiza wastani wa michezo miwili kabla ya kufi kia tamati mwishoni mwa mwezi huu.

 

Msimu huu ligi imeendeshwa bila mdhamini mkuu ambaye ndiye anayekuwa mhusika mkuu katika utoaji zawadi mbalimbali kwa bingwa na washindi wengine wa ligi hiyo.

 

Mpaka sasa zawadi ya bingwa haijatangazwa na ukiangalia ligi inakaribia kuisha, hii imekuwa ikishangaza sana kwani haijawahi kutokea miaka ya karibuni kwa ligi kuenda ukingoni huku zawadi za bingwa na washindi wengine zikiwa hazijatangazwa. Hii inaweza kushusha hata morali kwa namna moja au nyingine.

 

Mshindani huingia uwanjani huku akijua wazi anakwenda kugombania nini lakini mpaka sasa kwenye ligi yetu hii hakuna tamko la zawadi ya bingwa au wale watakaoshika nafasi ya pili na ya tatu.

 

Ni vyema Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ na Bodi la Ligi likaliangalia hili kwa upana zaidi hasa msimu ujao kwa kuhakikisha wadhamini wanapatikana ili timu shiriki zifahamu mapema bingwa atapata nini ukitoa zawadi ya kombe na medali kwa mshindi wa kwanza na wa pili.

 

Pia timu kupewa fedha ambazo zitawasaidia katika mambo mbalimbali ya kimalazi. Msimu huu tulishuhudia baadhi ya timu zikikwama kutoka kituo Fulani kwenda kingine, hii ni kutokana na ukata.

 

Pia hivi karibuni kuna timu ilichelewa na kufi ka kwenye kituo muda mfupi kabla ya mechi yao haijaanza na baada ya hapo ilifungwa mabao mengi sana hii ni kutokana na kukosa usafiri kwa wakati.

 

Hali hii inasababisha timu zionekane kama zinauza mechi kumbe hali ya kiuchumi inasababisha wachezaji washindwe kupambana uwanjani.

 

Msimu uliopita kulikuwa na mdhamini ambaye alikuwa anasaidia mambo mbalimbali kwa timu shiriki kama nauli na vitu vingine lakini msimu huu mambo yamekuwa tofauti hakuna tena vitu hivyo.

 

Kama hali hii iliyopo msimu huu itaendelea tena msimu ujao basi tutegemee kuiona ligi ya timu chache zilizobahatika kupata udhamini wa uhakika zikiendelea kupambana na zile ambazo zinategemea michango ya wanachama zikipambana kivyao.

 

Championi tunaamini TFF na Bodi ya Ligi imejifunza kwa yaliyotokea msimu huu hivyo ule ujao utakuwa na mabadiliko makubwa ya kuhakikisha mdhamini anapatikana ili vitu viende kama ilivyokuwa misimu kadhaa iliyopita.

Comments are closed.