The House of Favourite Newspapers

UNAHANGAIKA KUTAFUTA ‘WIFE MATERIAL?’ SOMA HAPA (2)

WIFE MATERIAL

 

NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa, nakukaribisha tena jamvini, leo tukiwa tunaendelea na mada tuliyoianza wiki iliyopita ya namna ya kumpata mke bora. Nilikueleza kwamba watu wengi wana kasumba ya kusubiri mwanamke aliyekamilika kwa kila kitu ndiyo watangaze ndoa, jambo ambalo siku hizi ni gumu sana kutokea.

 

Ukiweka vigezo vingi kwamba mke unayetaka kumuoa lazima awe na sifa unazotaka wewe, utashangaa muda unaenda, miaka inayoyoma bado unaishi maisha ya kibachela. Jambo ambalo kila mmoja anapaswa kulitambua ni kwamba hakuna mwanamke aliyekamilika, kama ambavyo hakuna mwanaume aliyekamilika. Hii ni kawaida kwa sababu hiyo ni hulka ya kibinadamu, hakuna aliyekamilika. Kwa hiyo ukishakubali kwamba wewe hujakamilika, huwezi kuweka masharti magumu ya mwenza ambaye amekamilika. Kama wewe hujakamilika, unafikiri yeye atawezaje kukamilika?

 

Kwa hiyo jambo la msingi, unapoamua kuanzisha uhusiano wa kimapenzi, ni kuwa tayari kukubaliana na mapungufu ya mwenzi wako. Inapotokea umempenda mwanamke fulani, hutakiwi kuanza kuchunguza hata mambo mengine yasiyo na msingi kwa sababu wahenga wanasema bata ukimchunguza sana huwezi kumla. Utakuwa mtu ametokea kumpenda mwanamke fulani na anaamini kabisa wakiishi pamoja, wanaweza kujenga familia bora.

 

Badala ya kufuatilia mambo ya msingi, ataanza kupeleleza kabla yake alikuwa anatoka na nani, ameshakuwa na wanaume wangapi, nani anampenda na mambo mengine ambayo siyo ya msingi. Matokeo yake, katika uchunguzi, anakutana na mambo ambayo yanamkatisha tamaa na kuona kwamba hawezi tena kuwa naye!

 

Historia ya mtu haina maana yoyote kwenye maisha yake ya baadaye, yawezekana amewahi kuwa na wanaume kadhaa  katika uhusiano lakini kila mmoja kwa wakati wake akamtenda na kusababisha asiyatamani mapenzi, wewe ukija kumhukumu kwa sababu amewahi kutoka na fulani na fulani, unakuwa hutendi haki kwa sababu hujui nini kilitokea mpaka akaachana nao. Jambo kubwa unalopaswa kulizingatia unapotafuta mwenzi wa kuwa naye, ni je, unampenda?

 

Na yeye anakupenda kwa dhati? Hilo ndiyo kubwa, hayo mambo mengine achana nayo. Kwa kawaida, wanawake walivyoumbwa, huwa ni wagumu sana kujionesha wazi kwamba anakupenda, ni mpaka wewe utakapoanzisha mada hiyo.

 

Kwa hiyo kama umepata bahati ya kuwa naye karibu, ukamueleza malengo yako kwake na yeye akaonesha kukuelewa, safari inatakiwa kuanzia hapo. Wewe ndiye unayeweza kumfanya akaja kuwa mke bora, akapendeza, akawa na tabia njema na kuwa mfano wa kuigwa, hata kama alishawahi kuwa na historia isiyovutia. Yawezekana anaonekana hajatulia kwa sababu hakuna mtu wa uhakika wa kumtimizia mahitaji yake ya msingi.

 

Hakuna mtu wa kumuongoza, anayeweza kumwambia kwamba hili ni baya na hili ni sawa na namna maisha yanavyotakiwa kuwa. Yawezekana unamuona hana maana kwa sababu hajasoma na hana kazi yoyote, kwani yeye anapenda kuwa golikipa asiye na ujuzi wowote kichwani?

 

Unaweza kumbadilisha akiwa kwenye himaya yako, akasoma na kupata ujuzi anaoutaka au akawa na kazi nzuri na mkaendelea na maisha. Achana na woga kwamba mwanamke ukimsomesha atatukimbia, ukiona amefanya hivyo jua hakuwa amekupenda kwa dhati.

 

Upo ushahidi wa watu wengi tu waliowaendeleza wake zao, wakawabadilisha na kuwa watu wanaoheshimika kwenye jamii hata kama huko nyuma walikuwa wakidharaulika. Uamuzi ni wako. Mwanaume mzuri ni yule anayemrekebisha anayempenda taratibu, hatua kwa hatua mpaka akafikia viwango anavyovitaka yeye.

 

Na ukweli wasioujua wengi, hakuna kitu chenye nguvu kama mapenzi. Ukimuonesha mapenzi ya dhati, ukamtimizia anachokitana halafu ukamueleza wewe unachokitaka, hata kama alikuwa na tabia mbovu kiasi gani, atakusikiliza na kubadilika. Kwa leo ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.

 

NA: HASHIM AZIZ| IJUMAA

Comments are closed.