×

Rigwaride Ra afande- 7

ILIPOISHIA RISASI JUMAMOSI:
“Ni pale mama, tumefika,” nilimwambia nikimwonesha nyumba nyingine nikijua mlango umefungwa lakini kumbe wenyewe walikuwepo maana ile tunakaribia tu, wakatoka wanawake watatu.

“Ndiyo pale wanapotoka wale wanawake?” aliniuliza mama.
“Hapana, kwa nyuma.”
Na kweli, kwa nyuma ndiyo nyumba ya akina afande Mwira ilipo, tukafika sasa…
SHUKA NAYO…

“Ni wapi?” mama aliniuliza kwa ukali…
“Hapa mama,” nilimwonesha mama ile nyumba. Cha ajabu sasa, mlango ulifungwa kwa kufuli jambo ambalo lilinishangaza sana mi mwenyewe…

“Mbona pamefungwa na kufuli?” mama aliniuliza swali ambalo si langu. Sasa mimi ningejibu nini kwa huyu mama, kwani mimi ndiye nilifunga kufuli?
“Mama hata mimi sijui kwa nini kuna kufuli,” nilimjibu tukiwa tumesimama.
Mara tukasikia mtu akitembea kwa ndani na kutokea mlango wa uani ambao ulisikika sawasawa.

Kutembea kule kukawa kunakuja mbele tuliposimama sisi, yaani mimi na mama.
“Karibuni,” mwanaume mmoja, mrefu sana, mweusi tii, alitukaribisha huku uso wake ukionesha dalili zote za kutoka kulala…
“Huyu alikuja hapa?” mama aliuliza bila salamu.

“Kuja kufanya nini?”
“Nimeuliza alikuja hakuja?” mama alikuja juu.
“We mama…una akili kweli? Huna salamu…huna maneno mazuri unauliza huyu alikuja hapa…alikuja kwa nani na kufanya nini?”
Mama alinigeukia mimi…

“Kumbe unanidanganya siyo?”
“Mama ni hapa, siwezi kukudanganya mama,” nilimjibu mama nikijua hashindwi kuniachia kichapo mbele ya yule mtu mweusi tii!
“Kwani binti unamtafuta nani au ulikuja kwa nani?” yule mtu mweusi tii aliniuliza…
“Namtafuta afande Mwira na wenzake.”

“Unawajua?”
“Nawajua.”
“Muda huu wameshakwenda kwenye lindo. Kurudi hapa ni saa kumi usiku. Mimi ndiyo nimerudi muda si mrefu,” alisema yule mtu.

Mama alikunja sura, akamwangalia yule mtu, akamuuliza…
“Huyu hujawahi kumwona hapa baba?”
“Hapana…”
“Hapana mama…”
Mimi na yule afande, wote tulikataa kwa pamoja ila sema mimi niliongezea na neno ‘mama.’

Mama alisimama akijifikiria kwa muda kisha akafyatuka…
“Sasa huyo afande Mwira sijui, nataka umjulishe kwamba namwachia mzigo huu. Akija hiyo saa ngapi sijui, atamkuta. Hawezi kumchezea mwanangu hivihivi naona. Kama alimwona anafaa angejitokeza nyumbani.”

“Mama…mama punguza jazba, nimekwambia afande Mwira na wenzake wanarudi saa kumi usiku, utamwachaje mwanao hapa? Kwanza mbona anaonekana ni binti mkubwa, ina maana hawezi kujichunga mwenyewe?”

“We unaangalia mwili, ana ukubwa gani huyu? Amejaa tu manyamanyama…mtu ana miaka 22 ndiyo mkubwa?” alisema mama huku mate yakimtoka kinywani kama mvua za kushtukiza…

“Huyu ana miaka 22?” aliuliza yule mtu kwa sauti yenye mshangao…
“Mimi ndiyo mama yake, namwacha hapa. Akija huyo afande Mwira mkabidhi, nitamfuatilia kesho,” alisema mama akiondoka.

Nilitamani kumfuata mama kwa nyuma lakini nikajua nikifanya vile kwa wakati ule, moto utawaka. Nikaamua kusubiri baadaye sana.

Lakini moyoni nilisema, ‘mama ungejua…si afande Mwira tu, na wenzake. Sasa kama kubaki au kukabidhiwa nije kukabidhiwa kwa nani?’
Sasa tukabaki mimi na yule mtu tunaangaliana…
“Unaitwa nani wewe?” aliniuliza kwa sauti ya chini huku akiniangalia kwa macho ya mlegezo…

“Rhoda…”
“Unaishi wapi?”
“Kule Wailes…”
“Unaishi na baba yako?”
“Ndiyo, lakini kasafiri…”

“Sasa huyo afande Mwira mlikutana wapi?”
“Kule barabarani.”
“Akaja na wewe hapa?”
“Ndiyo.”

“Kwa ajili ya nini?”
Eti hilo nalo lilikuwa swali jamani? Mtu anajua afande Mwira ni mwanaume, mimi ni mwanamke. Sasa anadhani pale nitakuwa nilifuata nini?!
“Kwani we unamzungumza afande Mwira gani?” nilimuuliza swali badala ya kumjibu…
“Si huyu wa chumba cha kati…”

“Mwanaume?” nilimuuliza kwa kebehi…
“Ndiyo,” alijibu…
“Huyohuyo,” nilimjibu.

Akaniambia basi karibu ndani ukae umsubiri afande Mwira tuone inakuaje?
Wakati anasema hivyo alikuwa akitembea kuelekea ndani nikamfuata kwa nyuma mpaka ndani kwake, yaani chumbani kwake. Nilichobaini ni kwamba, ile nyumba kila mtu alikuwa ana chumba tu. Na chumba hicho ndiyo kilikuwa sebule na chumba cha kulala…

“Kaa hapo,” aliniambia akinionesha kochi kubwa. Nikakaa pwaa! Maana mimi naye, wowowo peke yake ni shughuli nzito…
Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma kwenye Risasi Jumamosi ijayo.

Leave a Comment