ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA:
“Yes! Hakuna mtu anayepita eneo hili muda huu,” alisema mama Pilima hali iliyomfanya baba Pili aamini kwamba huenda wanakwenda kutimiza ndoto yake…
“Egemea kiti,” alisema mama Pilima…
JIRUSHE MWENYEWE…
Baba Pili aliegemea kiti kwa haraka sana, akatumbua macho kusubiri hatua nyingine akiamini ataambiwa au ataelekezwa…
“Mmm! Baba Pili acha mi niende bwana. Muda umekwenda kwelikweli, si ajabu nyumbani wameanza kuingiwa na wasiwasi,” alisema mama Pilima akiwa tayari ameshika kitasa cha mlango ili kushuka…
“Kha! Yaani mbona haifanani?” alihoji baba Pili…
“Nini?”
“Kuniambia nilale mpaka kuaga kwamba unawahi nyumbani…”
“Teh! Teh! Ulidhani nini kitafuata baba Pili? Mbona mimi nimeshaongea mengi na wewe?” alisema mama Pili akiwa ameshafungua mlango wa gari na kushuka.
Mama Pilima alisimama mlangoni, akamwangalia baba Pili kwa sura yenye umakini wa hali ya juu…
“Bai baba Pili, usiku mwema, nafurahia kampani yako,” alisema mama Pilima akaanza kutembea.
Baba Pili akiwa bado ameegemea kiti, alishindwa kujifahamu. Kwa kutumia mwanga hafifu uliokuwa ukitoka kwenye taa za madukani, alimwangalia mama Pilima anavyotembea kuelekea mitaa ya kwake kisha akatingisha kichwa akisema…
“Da! Ameniweza kweli! Yaani kuegemea kiti na kuaga maana yake nini? Yule nadhani kuna kitu ameshtuka, si hivihivi tu.”
Aliwasha gari na kugeuza kurudi kwake.
***
Alipofika nyumbani kwake, mama Pilima alimtumia meseji baba Pili ya kumjulisha amefika salama na kumtakia usiku mwema…
“Nimefika baba Pili, usiku mwema kwako na kwa familia pia, tudumishe upendo wetu.”
“Mh!” aliguna baba Pili.
***
Kulikucha, mama Pilima alikwenda kwenye shughuli zake kama kawaida. Akiwa kwenye pilikapilika alishtuka maeneo f’lani, akaita…
“Baba Pili…baba Pili,” aligeuka mwanaume huyo, akamkazia macho mama Pilima, lakini hakuonesha kumchangamkia.
Mama Pilima alimsogelea huku akiachia tabasamu na kumkazia macho…
“Vipi? Uko sawa baba Pili?” alihoji mama Pilima baada ya kumwona mwanaume huyo akiwa hana uso wa bashasha. Yeye kwa akili zake aliamini hiyo ilisababishwa na kitendo alichomfanyia jana yake, cha kumlaza kwenye kiti cha gari kisha kumwacha…
“Niko sawa, sijakuelewa lakini,” alijibu mwanaume huyo…
“Utanielewa tu baba Pili. Unajua nilishakwambia mimi siwezi kusaliti. Kwa nini usinielewe jamani? Kwani tukiendelea kwa urafiki wetu kuna nini?” alisema mama Pili huku mwanaume huyo akiendelea kumkazia macho…
“Oke, basi tufanye hivi…leo tukutane hotelini, tupeane raha. Lakini iwe leo tu, tusirudie tena. Haya niambie tutakutana saa ngapi na wapi?” alisema mama Pilima na kuuliza swali.
Mwanaume huyo aliwaza sana, akamshangaa mama Pilima lakini hakutaka kumwambia jambo lolote. Ila alimtamani kwa namna mwanamke huyo alivyo mzuri wa umbo mpaka sura. Akaona ile ni bahati ya mtende kwake, kuota jangwani…
“Panga wewe,” alisema…
“Mimi napanga saa kumi, nitakuwa nimemaliza kazi zangu, lakini kuhusu hoteli gani, panga wewe sasa,” alisema mama Pilima.
“Nitakwambia, simu yangu ile nimeiacha, imeharibika kidogo, natumia nyingine hii na namba pia ni nyingine, nitajie upya namba zako,” alisema mwanaume huyo.
Mama Pilima alimtajia namba mwanaume huyo lakini huku akiona kama bado hajachangamka…
“Vipi jana ulifika salama? Nilikutumia meseji hukunijibu. Gari umepaki wapi?” mama Pilima aliuliza maswali mawili kwa mpigo…
“Si ndiyo maana nimekwambia simu ina matatizo kidogo, gari liko kule Mnazi Mmoja kwa mbele.”
Kidogo mwanaume huyo amuulize mama Pilima amsevu kwa jina gani, akashtuka…
“Basi baadaye.”
“Poa baba Pili, utanicheki. Lakini kama nilivyosema, iwe leo tu. Mara moja tu halafu basi, sawa baba Pili?”
“Sawa, nimekuelewa,” alijibu mwanaume huyo akianza kuondoka ili kukwepa maswali zaidi.
Mama Pili alikuwa na mawazo. Aliamini bado hajamridhisha mwanaume huyo kwani hata majibu yake yalionesha hivyo…
“Bado hayuko sawa. Kaniambia ‘basi baadaye’. Angekuwa sawa angeniambia ‘basi baadaye mama Pilima’. Nimemwambia atanicheki, akanijibu sawa, nimekuelewa’. Angekuwa sawa, angenijibu ‘sawa, nimekuelewa mama Pilima’. Nadhani hayupo sawa.”
***
Mbele ya safari, yule mwanaume alimuwaza mama Pilima…
“Kuna wanawake wameumbwa jamani! Yaani yule mwanamke ameumbwa! Nimepata bahati kubwa. Siwezi kumwacha hivihivi tu. Mi amenivutia yale macho yake bwana,” alisema moyoni mwanaume huyo.
***
Saa kumi juu ya alama, mama Pilima alipokea simu kwa namba asiyoijua, akajua ni baba Pili…
“Haloo…niambie baba Pili…wapi? Ooo…napajua…oke… we umeshafika? Haya nakuja sasa hivi mpenzi wangu…”