×

Kidoa hongera; kuna maisha baada ya ushindi, jipange!

KIDOA (6)
KWAKO Mshindi wa Shindano la Ijumaa Sexiest Girl, Asha Salum ‘Kidoa’. Mambo vipi, ‘kiraruraru’ cha ushindi kimepungua? Unajisikiaje kuwa mshindi wa shindano hilo maarufu linaloendeshwa kila mwaka na Gazeti la Ijumaa?

Ukitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima, naendelea na mishemishe zangu za kila siku. Suala la kukuandikia wewe barua ni moja kati ya majukumu yangu. Nimekuwa nikifanya hivyo kwa mastaa mbalimbali, leo ni zamu yako.

Nasema ni zamu yako kwani nawe sasa ni staa. Kabla ya kuibuka kidedea katika shindano hilo, umaarufu wako ulianza kujionesha katika video ya Akadumba ya Msanii wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ lakini sasa umeongezeka zaidi.

Dhumuni la kukuandikia barua hii, kwanza ni kukupongeza. Nakupongeza kwani katika shindano hilo ulichuana na mastaa mbalimbali waliokuwa na majina makubwa lakini hatimaye wote uliwagaragaza na kutangazwa mshindi katika Ukumbi wa Dar Live, Mbagala-Zakhem jijini Dar.

Ushindi wako ni nafasi yako kujulikana. Watanzania watazidi kukufuatilia katika vyombo vya habari. Watataka kujua nini kinafuata kwako baada ya kukuona kwenye video ya Nay wa Mitego na ushindi wa Ijumaa Sexiest Girl.

Baada ya pongezi hizo, nikutake sasa uwe makini maana kipindi hiki ndicho ambacho wengi huwa wanafeli. Wanakuwa washindi lakini wanashindwa ‘ku-mantain’ huo ushindi. Mifano ipo mingi tu ya watu walioshinda mashindano mbalimbali lakini sasa wamepotea.

Usikubali kuwa sehemu yao. Maisha baada ya ushindi wako unayapanga mwenyewe kwa kujipanga nini cha kufanya ili umaarufu wako usipotee. Nini unatakiwa kufanya na kwa wakati gani. Hakikisha kila uchwao unajaribu kubuni kitu, unakifanya na vyombo vya habari vinaendelea kuripoti kazi zako.

Weka njaa ya maendeleo. Usiishie tu katika kuonekana kwenye video za wasanii. Weka mikakati mbalimbali ya kukuingizia kipato katika nyanja za burudani. Kama unaweza kuigiza, kuimba anza kufanya hivyo na ukomae kwa nguvu zote.

Wote waliofanikiwa walijiwekea malengo. Weka malengo kwa mwaka huu unaoanza, ujue utafanya nini kitakachokuongezea fedha na umaarufu. Waoneshe wale walioshinda mashindano mbalimbali kwamba inawezekana kushinda na kuendelea kuwa juu.

Ni matumaini yangu utayafanyia kazi hayo niliyokueleza na kwa ushauri zaidi, unakaribishwa Global Publishers muda wowote ili uweze kujifunza zaidi mbinu za mafanikio maana mjengo huu umesheheni wataalamu wa hayo mambo.
Mimi kaka yako,
……………….
Erick Evarist

Leave a Comment