Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.
Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.
Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni Mombasa, Kenya ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.
Grace anasafiri kuelekea Israel kikazi na Magesa anaitumia nafasi hiyo kumpekua mwanamke huyo akitaka kuujua ukweli wa maisha yake. Anachokutana nacho kinamshangaza sana. Hatimaye Grace anarejea na Magesa anambana kwa maswali magumu, hali inayosababisha mwanamke huyo apasue jipu na kueleza ukweli.
Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi na viongozi wa juu wa usalama, wamepeana saa 72 kuhakikisha ukweli unafahamika kuhusu kilichojificha nyuma ya mauaji hayo na tayari kuna kila dalili ya siri kufichuka.
Grace na Magesa waliokuwa mafichoni Mombasa nchini Kenya, wanajiandaa kwa safari ya kuelekea sehemu ambayo Magesa haijui, kwa kutumia mbinu za hali ya juu, wanafanikiwa kupita salama uwanja wa ndege na hatimaye wanaondoka.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Baada ya saa 72 kupita, vigogo watatu wa juu wa usalama wa nchi, Inspekta Jordan Ngai, Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi, Ephraim Mandiba, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa na Pius Kasekwa, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali walikutana kujadiliana kuhusu majukumu waliyopeana siku tatu zilizopita.
Katika uwasilishaji wao, ilibainika kwamba kifo cha CAG Mwampashi hakikuwa kifo cha kawaida bali mpango maalum uliopangwa kwa lengo la kuficha jambo zito lililokuwa linawahusu watumishi wa serikali.
Kilichozidi kuwashangaza wote, ni kugundua kwamba kumbe kulikuwa na uhusiano wa karibu kati ya Mwampashi na Magesa na kwamba yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kufahamu kilichokuwa ndani ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Kingine kilichobainika katika uchunguzi huo wa kina, ni kwamba hakukuwa na ripoti zozote za kidaktari zilizoonesha kwamba mapafu ya marehemu Magesa yalikutwa na moshi, kama inavyotokea kwa watu wote wanaokufa kwa ajali za moto.
“Una maana gani kusema mapafu yake hayakuwa na moshi?”
“Inafahamika kwamba mtu anayekufa kwa moto, lazima avute moshi mwingi wakati akihangaika kujiokoa na moshi huo huenda kujaa kwenye mapafu lakini ripoti ya daktari haioneshi kwamba kulikuwa na moshi kwenye mapafu ya marehemu. Kwa tafsiri nyepesi, Magesa aliuawa kabla kisha ndiyo ajali ikatengenezwa.”
“Tuna uhakika gani kwamba aliyekufa kweli ni Magesa?” Mandiba alihoji swali lililowafumbua wote vichwa vyao.
“We must request an exhumation order and then cross examine deoxyribonucleic acid of his body to be sure exactly who was burried in Magesa’s grave.” (Lazima tuombe kibali cha kuufukua mwili wa marehemu kisha tuuchunguze kwa kipimo cha DNA kuwa na uhakika ni nani hasa aliyezikwa kwenye kaburi la Magesa,” Pius Kasekwa alisema, wazo lililoungwa mkono na wenzake.
Hata hivyo, walikubaliana kwamba suala hilo liwe la mwisho, waendelee kujadiliana kuhusu mambo mengine mengi yaliyobainika katika uchunguzi wao wa saa 72.
“Risasi zilizotumika kumuua Mwampashi zinaonekana zimetoka kwenye bunduki zinazotumiwa na askari wa jeshi letu la polisi, kuna jambo zito litakuwa limejificha hapa.”
“Ni jukumu letu kufichua kila kilichojificha, lazima ukweli upatikane na kwa kuanzia, inabidi wahusika wote waliotajwa kwenye ripoti ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali, wakamatwe na kuwekwa chini ya ulinzi, lazima tutawapata wahusika wa mauaji miongoni mwao,” alisema Kasekwa.
Wakaendelea kujadiliana mambo mengi yaliyobainika katika uchunguzi na mwisho ikaamriwa kwamba ripoti ya CAG isomwe hadharani na nakala yake ipelekwe kwa mheshimiwa rais ili wote waliohusika katika ubadhirifu mkubwa wa mali za umma, wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria kujibu mashtaka yanayowakabili.
Pia wakakubaliana kwenda kufukua kaburi la Magesa ili kuhakikisha ni nani aliyekuwa amezikwa kwenye kaburi hilo. Baada ya makubaliano hayo, kikao hicho cha siri na cha dharura kilichochukua zaidi ya saa nne, kilihitimishwa kwa kila mmoja kukabidhiwa majukumu mapya.
Tofauti na awali, safari hii zilitengwa saa ishirini na nne tu uchunguzi uwe umeshakamilika. Wote wakatawanyika huku kila mmoja akaanza utekelezaji wa majukumu yake.
Saa chache baadaye, taarifa zilianza kusambaa kwenye vyombo vya habari kuhusu kutoka kwa ripoti ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali, ikiwa imesheheni kashfa nyingi za ufisadi, hasa katika wizara za fedha, nishati na madini na kwenye wizara ya maliasili na utalii.
Ripoti hiyo ilimshangaza karibu kila aliyeisikia kwani japokuwa ripoti za miaka mingine ya nyuma zilikuwa zikionesha ubadhirifu mkubwa wa mali za umma, hiyo ilionesha kuvunja rekodi. Watu wakaanza kukusanyika makundi kwa makundi kuijadili, huku wakiishinikiza serikali kuwachukulia hatua kali wote waliokuwa wakihusika.
Wapo waliounganisha matukio na kueleza kuwa upo uwezekano mkubwa kwamba waliomuua Mwampashi, walikuwa na lengo la kuficha uozo huo. Ndani ya muda mfupi tu tangu kutangazwa hadharani kwa ripoti hiyo, nchi ilikuwa ‘ikiwaka moto’ huku shinikizo la wananchi la kutaka wahusika wote wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria likizidi kuwa kubwa.
* * *
Wakati zogo likiendelea miongoni mwa wananchi, maafisa wa ngazi za juu wa usalama serikalini waliendelea na majukumu yao kama walivyokubaliana. Kibali maalum cha kufukua mwili wa Magesa (Exhumation Order) kikatolewa ambapo wanafamilia walijulishwa juu ya kilichokuwa kinaendelea.
Mtoto mkubwa wa marehemu, Ivan Magesa akawa miongoni mwa watu wachache walioshuhudia wakati kaburi la Magesa likifukuliwa na sampuli za mwili wake kuchukuliwa kwa ajili ya kwenda kufanya vipimo vya vinasaba (DNA) kutambua kama aliyezikwa alikuwa Magesa kweli.
“Naamini haki itatendeka kuhusu kifo cha baba yangu kama ambavyo siku zote nimekuwa nikiomba itokee,” Ivan alisema huku akitokwa na machozi wakati akishuhudia sampuli za mwili wa baba yake zikiondolewa makaburini hapo na kupelekwa hospitalini chini ya ulinzi mkali.
Japokuwa tukio hilo lilifanywa kwa usiri mkubwa, taarifa zilivuja na kusambaa kama moto wa nyika miongoni mwa wananchi, hali ikazidi kuwa tete kwani kwa ilivyoonekana, kulikuwa na mambo mengi nyuma ya pazia.
Taratibu zote zilifuatwa na majibu ya vipimo hivyo yakatoka haraka kuliko kawaida. Kila mtu akawa na shauku kubwa ya kutaka kujua majibu hayo yapoje.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye gazeti hilihili.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/