ILIPOISHIA WIKIENDA
Nilipofika hapo hoteli nikakutana na rafiki yangu mmoja ambaye si tu nilisoma naye Chuo Kikuu cha Mlimani bali pia tulitoka mkoa mmoja. Yeye alikuwa mfanyabiashara.
Tukazungumza sana. Yule bwana aliagiza chakula akaniagizia na mimi. Nikapata hapohapo mlo wa usiku tena wa bure.
SASA ENDELEA…
Baada ya chakula aliniambia kama ninataka kinywaji chochote niagize. Niliagiza maji tu ya kunywa. Yeye mwenyewe ndiyo aliagiza chupa tatu za bia.
Nilipoondoka hapo hotelini ilikuwa karibu saa tatu usiku, nikarudi nyumbani kulala. Asubuhi nilipoamka nilioga nikavaa. Dereva wangu aliponifuata nikamwambia mke wangu alikuwa amejifungua, hivyo nilihitaji anipeleke hospitali nikawajulie hali.
Dereva wangu akanipeleka Mikocheni. Nilikaa kidogo tu nikampa jina mtoto wetu. Nilimuita Mkanga, jina la kikwetu ambalo babu yangu aliniambia alimpa baba yangu kabla ya kupata jina la ubatizo.
Siku tatu zikapita. Mke wangu akaruhusiwa kurudi nyumbani. Kilikuwa kipindi cha furaha sana kwangu. Mtoto wetu aliyezaliwa alikuwa kama ishara ya matumaini na kuingia katika majukumu ya kikubwa.
Nilikuwa nikirudi nyumbani mapema ili kumsaidia mke wangu kulea mtoto wetu ambaye alikuwa kama tunu iliyotupa ishara njema katika ndoa yetu.
Kutokana na furaha ya kupata mtoto nilikuwa na maelewano mazuri na mke wangu ambapo wakati wote tulikuwa tunazungumza kwa furaha na kucheka.
Jina la Mkanga ndilo lililokuwa limetawala nyumba kwani kila wakati lilikuwa linatajwa; “Mkanga…Mkanga…”
Baada ya kukaa na sisi kwa miezi miwili, mama mkwe wangu akaondoka kurudi kwake. Tukabaki na mtumishi wa ndani aliyekuwa akitusaidia.
Ilipokamilika miezi mitatu, likizo ya uzazi ya mke wangu nayo iliisha. Mke wangu akaanza kazi. Mtoto akabaki na mtumishi mchana kutwa hadi mama yake anaporudi kazini.
Niseme tu kuwa yule mtumishi alikuwa hodari wa kazi na alikuwa akijua kulea mtoto kiasi kwamba tuliweza kumuachia mtoto na tunaporudi jioni tunamkuta yupo salama na amepatiwa mahitaji yote.
Kulikuwa na siku moja niliporudi kazini mchana nikakuta kesi nyumbani. Yule mtumishi alifanya usafi chini ya mvungu wa kitanda chumbani mwetu akakuta ule mkoba wangu wa uchawi. Kwa umbeya wake aliufungua ndani.
Alipoona vitu vya ajabuajabu akamuita mke wangu na kumuonesha.
“Nini hivi?” mke wangu akauliza akiwa amekunja uso.
“Sijui ni nini, vilikuwa ndani ya huu mkoba.”
“Huo mkoba ulikuwa wapi?”
“Niliukuta mvunguni. Nilikuwa nafanya usafi nikauona.”
“Huu utakuwa ni wa baba yake Mkanga, Sijui ni kwa nini mtu huyu anakuwa na vitu vya ajabuajabu. Kuna siku hivyo hivyo niliamka usiku nikamkuta uani na mkoba wake huo.”
Mwanamke akanisubiri, nilipoingia ndani tu akaniuliza:
“Vile vitu ulivyoviweka mvunguni ndani ya ule mkoba ni vya nini?”
Kwa kweli aliponiuliza swali hilo alinishtua kwani sikutegemea kuulizwa swali kama hilo.
Nilibabaika kidogo kabla ya kumjibu:
“Havina neno. Ule ulikuwa mkoba wa babu yangu, alinipa.”
“Alikupa wa nini?”
“Si unajua wazee wa zamani…”
“Mume wangu mbona unakuwa kama hukusoma! Unaweka vile vitu mvunguni kwa kazi gani?”
“Kwani uko wapi huo mkoba?”
“Nimeuacha hukohuko mvunguni ulikouweka mwenyewe. Wakati mwingine ukilala unajisikia kubanwa, kumbe ni hayo madude yako. Si yanatufyonzaga damu hayo?”
Nikajidai kucheka.
“Hapana. Mke wangu usiwe muoga kiasi hicho. Vile ni vitu tu vya kiasili, babu yangu alinipa nikae navyo.”
“Alikupa ukae navyo kwa kazi gani. Mbona hujibu hili swali?”
Hapo nikanyamza kimya. Sikuwa na jibu.
“Basi kama hutaki kusema nakuomba uende ukaviondoe ukatafute mahali pengine pa kuviweka, tena siyo humu nyumbani. Kaviweke ofisini kwako.”
“Mbona siku zote vipo mke wangu.”
“Nilikuwa sijaviona. Kwa vile nimeshaviona sitalala kwa amani humu chumbani, mwanangu bado mchanga.”
“Mke wangu havina madhara, viache tu.”
Niliposema hivyo ndiyo nilimpandisha.
“Kama ule ndiyo uchawi wa kwenu, hutaki viondoke mle chumbani, nakwenda kuutupa ule mkoba kwenye pipa la takataka!”
Akainuka na kuchanganya mwendo kuelekea chumbani. Na mimi nikanyanyuka na kumfuata.
“Hebu subiri,” nikamwambia tulipoingia chumbani.
Mwanamke akasimama na kunitazama.