ILIPOISHIA
Mwanamke huyo aliniambia na kuongeza.
“Kingine nilichotaka kukueleza ni kuwa kama vile ambavyo baba yako alimtoa kafara mke wake na wewe utatakiwa umtoe kafara mke wako ili mama yako aweze kufa kwa sababu muda wake umekwisha.”
SASA ENDELEA
Loh! Yalikuwa maneno yaliyonitisha sana. Nimtoe kafara mke wangu awe dondocha? Na ni kwa sababu gani hasa? Kama ni pesa za majini aliyezitaka ni baba yangu ambaye ameshakufa, mimi zinanihusu nini?
Hapo nikatikisa kichwa kukataa.
“Sikubaliani na masharti hayo. Mimi siwezi kumtoa kafara mke wangu, siwezi kufanya ukatili huo.”
“Huwezi nini, wakati hayo ni makubaliano ya sisi na baba yako. Baba yako alituambia wewe utarithi pesa zile na utatimiza masharti tutakayokupa,” mwanamke huyo akaniambia kwa mkazo.
Nikaendelea kutikisa kichwa.
“Huwezi kukataa kitu hapa. Kama umerithi zile pesa lazima utimize masharti hayo. Kama utakataa tutamchukua wenyewe mke wako. Sasa nenda kawape chakula wale madondocha, hawajakula tangu baba yako alipokufa.”
Hapo hapo nikashituka usingizini… Nikatazama huku na kule, sikumuona yule mwanamke aliyekuwa akiniambia maneno hayo.
Jasho lilikuwa limenisambaa mwili mzima. Nikanyanyuka na kuketi kitandani.
Nikagundua kuwa nilikuwa ninaota lakini huenda ndoto yenyewe ilikuwa na ukweli unaotisha.
Kwa ndoto ile niligundua marehemu baba yangu alikuwa akiishi na yule jini mwanamke ambaye alitaka nimrithi.
Pia niligundua kuwa baba yangu alikwenda eneo la Kisima cha Giningi huko Zanzibar kutafuta pesa za majini ndipo alipokutana na Habib Sultan ambaye alimmilikisha yule jini pamoja na kumpa masharti ya kupata utajiri.
Kumbe baba yangu alikuwa akimiliki pesa za majini! Na pia alikuwa akiishi na mke wa kijini! Ndiyo maana baada ya kufa mama yangu, baba hakuoa mke mwingine hadi mwenyewe alipofariki.
Lakini habari nyingine iliyonishitua ni kuhusu kuwa hai kwa mama yangu na mwanangu Abdul. Nilichokuwa ninakifahamu na kila mtu anakifahamu ni kuwa mama yangu alikufa, tena alikufa baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Na kuhusu mwanangu ni hivyo hivyo. Nilichokuwa ninakifahamu ni kuwa mwanangu alikufa.
Sasa ile habari kuwa watu hao wako hai wamegeuzwa madondocha, ilinishitua sana.
Lakini wakati nafikiria zile pesa, nikakumbuka kwamba mke wangu naye alikuwa kwenye hatari ya kufanywa dondocha bila kutaka mimi mwenyewe.
Pesa zilikuwa tamu lakini masharti yake yalikuwa magumu. Sikuweza kujua marehemu baba yangu aliupata wapi ujasiri wa kuyakubali masharti yale.
Kusema kweli baada ya kuamka sikulala tena hadi asubuhi kulipokucha. Baada ya kuoga na kuvaa nilichukua sime nikatoka kuelekea kule kwenye pango ambako niliambiwa mama yangu na mwanangu walikuwa wamewekwa.
Nilifika hadi pale mahali ambapo baba yangu alianguka na kufa nikaendelea kwenda hadi nikaona ule mti ambao baba yangu aliniambia. Nikakata kushoto. Baada ya mwendo mfupi nikakuta kichaka ambacho nilishuku ndiyo kile nilichoambiwa kuwa ndani yake kuna pango.
Kitu kilichonipa moyo na kuona kuwa mahali hapo palikuwa na watu nilisikia sauti za watu wanaolalamika. Nikaingia ndani ya kile kichaka, nikaona pango lililokuwa limezibwa kwa jiwe kubwa. Sauti nilizokuwa ninazisikia zilikuwa zinatoka ndani ya pango hilo.
Nikaliondoa lile jiwe na kulisukuma kando. Mlango wa pango ukawa wazi. Nikashika sime yangu mkononi na kuingia. Mwanga wa jua ulikuwa umejipenyeza hadi ndani ya pango hilo na hivyo niliweza kuona vyema.
Vile naingia tu, zile sauti zikazidi. Nikamuona mama yangu na mwanangu wamewekwa chini kama walemavu wakilia njaa. Walikuwa weusi kama waliopakwa lami na walikuwa wamekonda sana kiasi kwamba walikuwa wanatisha na kuonekana kama vinyago.
Walikuwa wamenikodolea macho huku wamefungua midomo yao kuashiria kuwa walikuwa wanataka kula. Kwa kweli walinitia huruma sana. Mambo yale yalifanywa na baba yangu aliyekuwa ameshakufa lakini kama angekuwa hai ningekwenda kumkata na sime nikamuua kwa hasira.
Baada ya kumuona mama yangu na mwanangu wanavyolalamikia njaa, nikakumbuka kwamba nilikwenda kizembe mahali hapo. Sikuwachukulia chakula chao nilichoagizwa. Nikageuka na kutoka mbio.
Nilirudi nyumbani nikawatayarishia uji wa mapumba ya mahindi kama nilivyoagiwa kisha nikautia uji huo asali. Sikuona vibaya kuwapelekea uji wa mapumba ya mahindi kwa sababu ni mzuri na mimi mwenyewe niliwahi kuunywa mara nyingi.
Uji ulipoiva niliutia kwenye chupa ya chai nikachukua vikombe viwili na kutoka mbio kurudi kule pangoni.
Niliingia kwenye lile pango nikawamiminia uji kwenye vile vikombe na kuwapa. Walikuwa hawawezi kunywa wenyewe. Walikuwa kama watu waliopooza. Ilibidi niwanyweshe. Uji ulikuwa moto lakini walikunywa hivyo hivyo kwa sababu ya njaa.
Kila mmoja alikunywa vikombe vinne.
Itaendelea wiki ijayo