Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.
Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.
Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni Mombasa, Kenya ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.
Grace anasafiri kuelekea Israel kikazi na Magesa anaitumia nafasi hiyo kumpekua mwanamke huyo akitaka kuujua ukweli wa maisha yake. Anachokutana nacho kinamshangaza sana. Hatimaye Grace anarejea na Magesa anambana kwa maswali magumu, hali inayosababisha mwanamke huyo apasue jipu na kueleza ukweli.
Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi. Tayari baadhi ya mambo yameanza kufichuka ambapo inaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kifo cha Mwampashi na Magesa.
Kaburi ambalo kila mtu anaamini kwamba ndipo alipozikwa Magesa, linafukuliwa na sampuli zinachukuliwa kwa ajili ya vipimo vya DNA.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Japokuwa tukio hilo lilifanywa kwa usiri mkubwa, taarifa zilivuja na kusambaa kama moto wa nyika miongoni mwa wananchi, hali ikazidi kuwa tete kwani kwa ilivyoonekana, kulikuwa na mambo mengi nyuma ya pazia. Taratibu zote zilifuatwa na majibu ya vipimo hivyo yakatoka haraka kuliko kawaida. Kila mtu akawa na shauku kubwa ya kutaka kujua majibu hayo yapoje.
“Nilijua tu.”
“Ulijua nini kiongozi?”
“Kwamba majibu yatatoka hivi. Hili suala ni gumu kuliko tulivyotegemea,” Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa, Ephraim Mandiba aliwaambia wenzake, Inspekta Jordan Ngai, Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi na Pius Kasekwa, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali wakati wakijadiliana kuhusu majibu ya DNA yaliyotoka.
Katika majibu hayo, ilibainika kwamba mwili uliokuwa umezikwa kwenye kaburi la Magesa, haukuwa wa Magesa kama watu wote walivyokuwa wanaamini bali mtu mwingine tofauti kabisa.
“Sasa kama siyo yeye, huyu aliyezikwa kwenye kaburi lake ni nani na yeye mwenyewe yuko hai au amekufa? Na kama yupo hai, amejificha wapi na kwa nini alidanganya kuhusu kifo chake?”
“Kuna maswali mengi hapa ambayo hakuna anayeweza kuwa na majibu. Inaonesha nyuma ya pazia kuna siri kubwa pengine kuliko hata tulivyokuwa tunafikiria,” alisema Kasekwa, kila mtu akawa anatingisha kichwa kukubaliana na kilichokuwa kinasemwa.
“Lakini kabla ya tukio hili la mwisho, kulikuwa na matukio mengine kadhaa ya kujaribu kuyakatisha maisha ya Magesa. Sijui hilo tunalizungumzia vipi.”
“Inavyoonekana, matukio yote hayo yalianza kutokea baada ya Magesa kuwasiliana na marehemu Mwampashi na kumtumia ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali. Kwa hiyo tutakuwa hatukosei kusema kwamba waliomuua Mwampashi ndiyo haohao waliofanya kila kinachowezekana kutaka kumuua pia Magesa.”
“Inabidi tuingie tena kazini kufuatilia kwa kina kilichotokea kwa Magesa. Lazima mwisho wa siku ukweli ufahamike, hatuwezi kujiita viongozi wa juu wa usalama wakati kuna matukio kama haya yatokea halafu wahusika wasipatikane. Kama tukishindwa kuufahamu ukweli, hatuna haja ya kuendelea na kazi, ni bora tujiuzulu,” alisema Mandiba, ukimya ukatawala kati yao.
Walichokubaliana, ilikuwa ni kuanza kuchimba kwa kina kufuatilia kila kitu kilichotokea kwenye maisha ya Magesa, yakiwemo majaribio kadhaa ya kutaka kuyakatisha maisha yake mpaka ajali ambayo kila mmoja alikuwa akiamini kwamba ndiyo iliyoyakatisha maisha yake.
Bila kupoteza muda, kazi ilianza ambapo mtu wa kwanza aliyetafutwa, alikuwa ni mke wa Magesa, Vivian. Kazi ya kumtafuta mwanamke huyo haikuwa nyepesi kwani vijana waliotumwa kumtafuta, walipofika nyumbani kwake waliambiwa kwamba kwa wiki nzima mwanamke huyo hakuwa amerejea nyumbani.
“Mpigieni simu mwambie tunamhitaji.”
“Simu zake zote hazipatikani hewani.”
“Sasa mnajuaje kama huko aliko yupo salama.”
“Yupo salama, ni kawaida yake, atakuja tu mwenyewe,” msichana wa kazi aliwajibu wale watu. Ikabidi waondoke na kurudisha taarifa kwa mabosi wao.
“Mnakumbuka siku zile ilipokuja taarifa kwamba mumewe amefariki kwenye ajali mlimkuta wapi?”
“Bagamoyo.”
“Anaweza kuwa yuko huko, mfuateni haraka. Hakikisheni anapatikana leoleo.”
“Sawa mkuu,” walijibu vijana hao na bila kupoteza muda, safari ya kuelekea Bagamoyo ikaanza.
Baada ya takribani dakika arobaini, tayari walikuwa wamewasili, wakaenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya Kitalii ya Mangrove Swamp iliyopo ufukweni mwa Bahari ya Hindi.
Walichokuwa wamekihisi ndicho kilichotokea kwani ni kweli walimkuta mwanamke huyo akiwa amejichimbia kwenye hoteli hiyo ya kitalii. Kama ilivyokuwa mara ya kwanza, walimkuta mwanamke huyo akiwa amelewa chakari, akiwa amevaa nguo za kuogelea zilizoyaanika wazi maungo yake muhimu.
Mbaya zaidi, alikuwa sambamba na mheshimiwa waziri mkuu, ambaye naye alionekana kulewa chakari, wakawa wanafanyiana vituko vya kimahaba vya hapa na pale. Hata bila kuuliza, kwa jinsi walivyokuwa wamekaa, walionesha kwamba wana uhusiano wa kimapenzi.
“Unajisikiaje kuwa na mimi Vivian.”
“Nakupenda sana tena sana, umenisahaulisha maumivu yote niliyosababishiwa na mume wangu, bora hata alivyokufa mshenzi yule.”
“Usimchukie marehemu, amepata alichokistahili,” alisema waziri mkuu na kumvutia Vivian kifuani kwake, wakagusanisha ndimi zao huku wakionesha kuwa kwenye hisia nzito za kimapenzi.
“Samahani kwa kuwaingilia, heshima yako mkuu. Tafadhali tunaomba kuongea na mama mara moja.”
“Nyie ni akina nani mnaoingilia starehe za mabosi wenu?” alisema mheshimiwa waziri mkuu kwa sauti ya kilevi.
“Samahani, sisi ni askari kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam. Tumeagizwa na Mandiba kuja kumchukua Vivian, kuna mambo muhimu anatakiwa kwenda kutusaidia,” alisema mmoja kati ya wale vijana.
Licha ya ufafanuzi huo, haikuwa kazi nyepesi kuondoka na Vivian, ikabidi wampigie simu Mandiba ambaye kwanza alionesha kushangazwa sana na kitendo cha mheshimiwa waziri mkuu kukutwa na mwanamke huyo, tena akiwa amelewa wakati ulikuwa ni muda wa kazi. Ikabidi ampigie simu na kumuomba awaruhusu vijana wake wamchukue Vivian, jambo ambalo alikubaliana nalo kwa shingo upande.
Tayari taa nyekundu ilishawaka kwenye kichwa chake kuhusu uhusiano kati ya mheshimiwa waziri mkuu na Vivian. Baada ya kuzungumza naye kwa simu, Vivian alichukuliwa na kurejeshwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano ya kina.
“Tumefukua kaburi ambalo kila mtu alikuwa akiamini kwamba ndiko alikozikwa mumeo lakini baada ya kufanya kipimo cha DNA imebainika kwamba aliyezikwa si mumeo.”
“Mimi hayo mambo hayanihusu, kwanza bora alikufa, mwanaume mshenzi sana yule.”
“Kwa sababu gani unazungumza hivyo Vivian? Yule si alikuwa mumeo?”
“Hata kama ungekuwa ni wewe ungeweza kumpenda mtu anayefanya ushenzi kama huu?” alisema mwanamke huyo kilevi huku akitoa simu yake na kufungua upande wa picha. Akaifungua picha moja ambayo Magesa alikuwa akionekana akiwa mtupu ndani ya hoteli, tena akiwa na mwanamke mwingine kitandani.
“Hii picha wewe umeipata wapi?”
“Wala haina haja ya kujua nimeipata wapi lakini kama hiyo haitoshi, mume wangu amempa mwanamke mwingine ujauzito nje ya ndoa. Kweli unaweza kumpenda mtu wa aina hiyo? Bora amekufa, mshenzi sana yule.
“Una uhusiano gani na mheshimiwa waziri mkuu?”
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye gazeti hilihili.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/