Waliosema kwamba ukiona giza linaongezeka ujue mapambazuko yamekaribia hawakukosea. Msemo huo wa wahenga unaonekana kuanza kutimia kwa Jafet Lubongeja na msichana aliyekuwa anampenda kuliko kitu chochote, Anna.
Baada ya kupitia kwenye misukosuko mingi, penzi lao likitawaliwa na machozi, maumivu ndani ya moyo, usaliti na kukataliwa, hatimaye mapambazuko yameanza kuonekana.
Wawili hao walikutana wakiwa bado wadogo, Jafet akiwa ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Mtakatifu Paulo iliyopo Kwimba, Mwanza huku Anna akiwa ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bwiru.
Penzi zito likachanua kati yao kiasi cha kumfanya Jafet afikie hatua ya kutoa figo yake moja na kumpa Anna aliyekuwa anasumbuliwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi.
Hata hivyo, licha ya wema mkubwa alioufanya Jafet, baadaye wazazi wa Anna wanaanza kumchukia Jafet baada ya Anna kupona kabisa. Sababu kubwa ya kumchukia ni baada ya kugundua ukweli kwamba kijana huyo alikuwa akitokea kwenye familia maskini sana, wakaona hana hadhi ya kuwa mkwe wao.
Wakafanya kila kilichowezekana na hatimaye wakafanikiwa kuwatenganisha wawili hao. Hata hivyo, baadaye mambo yanaanza kumwendea kombo Anna, anapewa ujauzito na mwanaume mwingine na wazazi wake wanapoamua kuutoa, maradhi yake ya figo yanarudi upya.
Mtu pekee anayekuja kusaidia kumrudishia Anna furaha, akiwa hoi kitandani ni Jafet. Uwepo wake unasababisha msichana huyo apone maradhi yote yaliyokuwa yanamsumbua, jambo linalomshangaza kila mmoja. Mwisho wazazi wa Anna wanaamua kuwatafutia chuo kimoja nchini Marekani ili wapate muda wa kuwa karibu zaidi.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Baada ya safari ndefu angani, hatimaye baba yake Anna, Jafet na Anna waliwasili jijini New York, Marekani kwenye Uwanja wa Ndege wa JFK, wakakamilisha taratibu zote za kiusalama uwanjani hapo ambapo baadaye walitoka na kukodi teksi iliyowapeleka mpaka kwenye kituo cha treni za kasi almaarufu New York Subways.
Baba yake Anna ndiye aliyekuwa kiongozi wa kila kitu kwa sababu hata Anna naye hakuwahi kupanda treni ziendazo kasi, wakakamilisha taratibu zote na muda mfupi baadaye, tayari walikuwa ndani ya treni kuelekea Manhattan.
Baada ya safari iliyowachukua takribani dakika 45, wakisimama kwenye vituo vingine vingi katikati ya safari, hatimaye waliwasili Manhattan, wakateremka na kuchukua teksi iliyowapeleka mpaka kwenye jengo kubwa lililokuwa na maandishi makubwa ya vioo yaliyosomeka: The Icahn School of Medicine at Mount Sinai (ISMMS).
“Hiki ndiyo chuo mtakachokuwa mnasoma, zamani kilikuwa kinaitwa Mount Sinai School of Medicine. Kinatoa madaktari bingwa duniani kote, naamini mtakuwa hodari sana mkihitimu.
“Anna, naamini ndoto zako za kuja kuwa daktari mashuhuri wa figo zitatimia sasa,” alisema baba yake Anna wakati wakitembea taratibu kuelekea kwenye jengo hilo, kila mmoja akiburuza begi kubwa pamoja na mizigo mingine.
Kwa kuwa tayari baba yake Anna alishafanya taratibu zote za Jafet na Anna kujiunga na chuo hicho, walipofika walielekea moja kwa moja kwenye ofisi za usajili ambako walikamilisha taratibu ndogondogo, wawili hao wakapokelewa rasmi chuoni hapo.
Baada ya hapo walielekea kwenye ofisi ya mkuu wa chuo ambako nako walikamilisha taratibu chache kisha wakapelekwa na viongozi wa serikali ya wanafunzi mpaka kwenye hosteli zilizokuwa chuoni hapohapo.
Baada ya kukabidhiwa vyumba vyao, Jafet akichanganywa na wanachuo wenzake wa kiume kutoka mataifa mbalimbali, Anna akipelekwa upande wa wasichana, walirejea pale mapokezi walipomuacha baba yao kwa ajili ya kuagana.
“Nataka muishi kwa upendo na amani, kukitokea matatizo yoyote naomba sisi wazazi tuwe wa kwanza kujua, tupigieni simu wakati wowote. Kubwa zaidi nawasisitiza, najua mnapendana sana lakini chondechonde msifanye mapenzi mpaka mtakapokuwa mmeoana,” alisema baba yake Anna kwa msisitizo, Jafet na Anna wakatazamana kisha wote wakajiinamia chini kwa aibu.
Baba yake Anna aliendelea kuwapa nasaha na kuwataka wawe mfano bora chuoni hapo kwa tabia njema na kuelekeza nguvu zao kwenye masomo. Mwisho alitoa fedha za matumizi na kuwakabidhi, kila mmoja akapewa zake na kuahidi kuendelea kuwatumia kila wanapoishiwa.
Baada ya mazungumzo yaliyochukua karibu dakika arobaini, baba yake Anna aliinuka, tayari kwa kuanza mchakato wa safari ya kurejea Tanzania. Wakamsindikiza mpaka kwenye kituo cha teksi kilichokuwa jirani na chuo hicho cha kisasa, akaondoka na kuwaacha wawili hao wakimpungia mikono mpaka alipopotea kwenye upeo wa macho yao.
Huo ukawa mwanzo wa wawili hao kufungua ukurasa mpya, mawazo yote juu ya Suleikha yalifutika kabisa kwenye kichwa cha Jafet, mapenzi yake kwa Anna yakazidi kuongezeka maradufu.
Kila alipokuwepo Anna, Jafet alikuwa pembeni yake, mapenzi yao hayakuwa siri tena, kila mtu chuoni hapo aliwafahamu. Ndani ya muda mfupi tu, wakawa maarufu sana wengi wakiwapachika jina la African Couple (Wapenzi wa Kiafrika)! Kingine kilichofanya wazidi kuwa maarufu, ni uwezo wao darasani.
Japokuwa Anna hakuwa na kichwa chepesi kama Jafet, kitendo cha kushirikiana kwa kila kitu, kuanzia kusoma, kujadili kwa makundi na kufanya mazoezi ya vitendo, kilizidi kumuongezea uwezo wa kuelewa. Ikafika kipindi wakawa wanafukuzana kwenye matokeo ya mitihani na majaribio ya chuoni.
Ikawa kama Jafet ameshika nafasi ya kwanza, basi Anna anashika nafasi ya pili au ya tatu, wakatokea kuwa kipenzi cha kila mmoja. Siku zilizidi kusonga mbele, wakazidi kuelekeza nguvu kwenye masomo huku pia afya ya Anna ikiendelea vizuri kwani kwa kipindi chote hicho, hakuwahi kulalamikia kuumwa wala kusikia maumivu ya kitu chochote.
Mara kwa mara walikuwa wakizungumza na wazazi wao kwa simu, baba yake Anna akawa anamueleza jinsi alivyomalizana na Suleikha.
“Nilitenga siku maalum na kufunga safari mpaka chuoni kwao, nikajitambulisha kwamba mimi ndiyo baba yako na kumueleza kwamba nafahamu kuhusu uhusiano wenu wa kimapenzi kwa sababu umeshaniambia,” alisema baba yake Anna jioni moja wakati akizungumza na Jafet kwa simu.
Kijana huyo akawa na shauku kubwa ya kutaka kusikia nini kilichofuatia, baba yake Anna akaendelea:
“Nilimueleza kwamba kwa bahati mbaya, baba yako mkubwa anayeishi nchini Marekani amekuja kukuchukua wewe na mama yako na kwamba amewahamishia huko. Nikamwambia kwamba uliondoka haraka mno kiasi cha kukosa hata nafasi ya kuja kumuaga na kumuomba radhi kwamba hutaweza tena kuwa naye kwa sababu hutegemei kurejea Tanzania.
“Nikamtaka aendelee na maisha yake tu kuliko kuendelea kusubiri kitu ambacho hakiwezi kutimia. Alilia sana na kunitia huruma, inaonesha alikuwa anakupenda sana. Sijui una damu gani ya kupenda kiasi hicho,” alisema baba yake Jafet na kusababisha wote wawili wacheke. Aliendelea kumueleza kila kitu na mwisho akamtaka kuwa na msimamo kama mwanaume kwa sababu anaweza kuja kuyumbishwa tena na kushindwa kuamua nini cha kufanya.
“Msimamo wangu ni kwamba nampenda sana Anna na sipo tayari kumpoteza. Yeye ndiye mke wangu,” alisema Jafet kwa kujiamini, wakaendelea kuzungumza mambo mengi mpaka baba yake Anna alipokata simu.
MIAKA MITATU BAADAYE
Jafet na Anna waliendelea vizuri na masomo yao na hatimaye wote wakaingia mwaka wa mwisho wa masomo yao, huku uwezo wao darasani ukizidi kuwa gumzo kila sehemu. Kila aliyewafahamu aliwatabiria makubwa kwenye maisha yao ya baadaye.
Hatimaye walibakiza miezi michache kabla ya kumaliza masomo na kama ulivyokuwa utaratibu wa chuo hicho, baada tu ya kumaliza mitihani ya mwisho, kilichofuatia ilikuwa ni mahafali kwa sababu wanachuo wengi walikuwa wakitoka nchi mbalimbali, jambo ambalo lingefanya iwe vigumu kuondoka na kisha kurejea baadaye kwa ajili ya mahafali.
Maandalizi ya mitihani ya kuhitimu chuo yalienda sambamba na maandalizi ya mahafali, wazazi wa pande zote mbili nao kwa upande wao wakaanza kujipanga kwa ajili ya kufanikisha mahafali ya watoto wao. Mara kwa mara walikuwa wakiwasiliana na Jafet na Anna na kupeana utaratibu wa jinsi mahafali hayo yatakavyokuwa.
Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia sehemu ya mwisho ya hadithi hii Jumatano kwenye Risasi Mchanganyiko. Jiandae pia kusoma hadithi nyingine nzuri itakayofuata baada ya hii kumalizika.
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/
Enock Kaaya hadithi bado haijaisha so huwezi sema mapenzi kati ya jafeth na sulekhia yameisha kuwa mpole mpaka mwisho wa hadhithi utajua maana ya mapenzi yasiyo isha
Your Comment kaka wewe ni nouma
yes mapenzi mazito aisee
huzuni kwako suleka umedandia gari kwa mbele
Hadithi nzuri sana……inaelimisha kuwa upendo wa kweli haufi.