×

Mbaroni kwa Ubakaji wa Mtoto na Kumsababishia Kifo!

CHUGAKamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji

Na Stephano Mango, Risasi

Ruvuma: Jeshi la Polisi mkoani hapa limemtia mbaroni kijana Dickson Nchimbi (29), mkazi wa Kijiji cha Matiri wilayani Mbinga kwa tuhuma za ubakaji wa mtoto (jina linahifadhiwa), mwenye umri wa miaka minne ambaye naye ni mkazi wa kijiji hicho na kukutwa porini akiwa amefariki dunia baada ya kufanyiwa kitendo hicho cha kinyama.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji  aliliambia gazeti hili kuwa tukio hilo lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita majira ya saa 12:00 jioni kwenye kijiji hicho.

Alisema kuwa, siku ya tukio, mtoto huyo alikutwa porini akiwa amefariki dunia huku akiwa ameingiliwa na sehemu zake za siri kuharibiwa na mtu aliyetajwa kwa jina la Dickson Nchimbi, mkazi wa kijiji hicho.

Alifafanua kuwa, ilidaiwa siku hiyo ya tukio, mtoto huyo alikuwa nyumbani kwa wazazi wake, akiwa peke yake wakati wazazi wake wakiwa shambani ndipo mtuhumiwa Nchimbi akapata nafasi ya kumchukua na kwenda naye hadi porini ambako inadaiwa alimfanyia kitendo hicho kilichomsababishia kifo.

Kamanda Mwombeji alifafanua kuwa mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa baada ya kuingiliwa alinyongwa kwa kuvunjwa shingo.

Hata hivyo, kamanda huyo alisema upelelezi kuhusiana na tukio unaendelea ikiwa ni pamoja na kumpima akili mtuhumiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Leave a Comment