Kuna msomaji wetu mmoja ameamua kupasua jipu wiki hii kuhusu mjadala wa simu feki kufungwa. Kwa kuheshimu mchango wake tunawaletea kile alichotaka jamii ifahamu; fuatana naye:
Shirika la Kimataifa la Mawasiliano Duniani, International Telecommunication Union (ITU), lilitoa agizo kwa nchi wanachama kuwa ifikapo Juni 17, 2015 iwe mwisho wa kurusha na kutumia mawimbi na vifaa vya analogia kwa televisheni.
Tanzania kama mwanachama wa shirika hilo, iliitikia wito na kuzima mitambo yote ya analogia katika urushaji wa matangazo ya televisheni. Ukurasa mpya ukafunguliwa kwenye urushaji wa matangazo ya televisheni Tanzania.
Katika siku za karibuni shirika letu la umma linaloratibu shughuli za mawasiliano, yaani Tanzania Communication Regulatory Authority (TCRA) wametoa angalizo kuwa ifikapo Juni 2016 mwaka huu, watazima au kuzuia utumiaji wa simu za mkononi zote feki.
Yaani ambazo watengenezaji wake wamezisajili ITU kwa vitambulishi maalum vya kimataifa viitwavyo kwa lugha ya kigeni, International Mobile Equipment Identity (IMEI) na tayari shirika hilo la umma limeshatuma ujumbe mfupi kwa watumiaji namna ya kuzijua IMEI za simu zao na kisha kutambua kama ni halisi au feki.
Nafikiri nayo ni kuitikia wito wa shirika hilo la ITU. Inawezekana pia ni katika kuhakikisha kuwa Watanzania wanatumia bidhaa za mawasiliano zilizo bora na halisi au wengi wanapenda kuziita genuine.
Au pia inawezekana ni katika kuongeza kasi na ufanisi kwa shirika letu la umma katika kwenda sawa na kipindi hiki cha kufanya kazi kwa nguvu zote cha Rais Dkt. John Magufuli, hivyo basi kutafuta na kufukua kila linaloonekana katika nafasi yao TCRA kulifanyia kazi kwa kuliboresha.
Tukiangalia katika upande mwingine wa shilingi naona kuna tatizo la msingi tu nafikiri wapanga sera wataliona pia. Afrika ya Kusini ilichelewa kuzima mitambo yake ya analogia mwaka jana kama walivyotakiwa na ITU.
Walikataa kutii tarehe ya mwisho, Juni 17, 2015 kwa sababu za msingi kuwa wazalishaji wake wa ndani hawakuwa na uwezo kwa wakati huo wa kutengeneza ving’amuzi (decoders), vya kunasa mawimbi ya digitali katika upokeaji wa mawimbi hayo ya televisheni.
Hapa Tanzania ilionekana dhahiri tu kuwa tulipozima mitambo yetu ya analogia basi tulifungua mwanya kwa kampuni za nje kutuletea ving’amuzi maana sisi hatuna kampuni zetu zinazotengeneza vifaa hivi. Inajulikana tu kuwa China ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kutuletea teknolojia zao katika kila kitu kinachohusiana na maisha yetu.
Afrika Kusini kwa kujua hili walikataa kuzima mitambo yao hadi pale kampuni zao za ndani zitakapoweza kuzalisha angalau asilimia 60 ya ving’amuzi hivyo. Hivyo kuleta ajira, kuongeza kipato kwa wananchi na kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi zitakazotozwa kwenye bidhaa hizi.
Hili ni suala la sera za nchi husika ambazo wazalendo wa nchi husika hupanga na kutekeleza kwa maendeleo ya nchi yao. Je, sisi tulifikiria mbadala huu au tulikuwa tunakubali tu wanachotaka wakubwa wa Ulaya? Maana si lazima tuwe na kampuni za kizalendo kwa asilimia mia moja, hata kampuni za wageni waliowekeza hapa zingekidhi haja hii.
Wawekezaji waliowekeza na kujenga viwanda hapa Tanzania lazima wangeliajiri watu wetu na wangetumia rasilimali zetu kuongeza tija katika uzalishaji wao.
Itaendelea wiki ijayo.
Hata Kenya iliongeza muda wa kutumia analojia!