Stori: Musa Mateja na Imelda Mtema, Ijumaa
Dar es Salaam: Tumbua majipu inazidi kushamiri kila kona na sasa imemdondokea jamaa aliyejitambulisha kwa jina moja la Samwel aliyekuwa akijidai kuwa ni Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kujikuta akichezea kichapo ‘hevi’ baada ya kutumia mwanya huo kutapeli dukani.
Tukio hilo la aina yake lilijiri Machi Mosi, mwaka huu kwenye duka la Hamza Shopping Center lililopo Sinza-Madukani jijini Dar baada ya kuwekewa mtego naye kuingia mkenge mzimamzima.
Ilidaiwa kwamba, mmiliki wa duka hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Hamza alimshtukia Samwel kuwa si Afisa wa TRA na kwamba, alitaka kujipatia fedha na mali zake kwenye duka hilo kwani awamu ya kwanza, jamaa huyo na mwenzake walifanikiwa kumtapeli zaidi ya Sh. milioni 2 kwa gia hiyo ya kujifanya Maafisa wa TRA.
Kwa mujibu wa mashuhuda, muda mfupi kabla ya tukio hilo, mmoja wa watu walioshtukia mchongo huo aliwatonya Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global Publishers ili kusaidia kuweka mtego ambapo mara moja vijana hao wa OFM walitinga na kufanya kama walivyopokea mafunzo yao wakihakikisha kuwa jamaa huyo anatiwa mbaroni.
Ili kuweka mambo kiserikali, Polisi wa Kituo cha Urafiki, Ubungo walipewa taarifa ambao nao walifika eneo la tukio na kufanya kazi yao sawia huku OFM wakichukua picha za tukio hatua kwa hatua.
Akizungumzia tukio hilo, Hamza alidai kuwa, jamaa huyo na mwenzake wamekuwa wakimtapeli mara kwa mara, jambo ambalo lilikuwa kero kwake hivyo alilitafutia ufumbuzi na kwa
kuwatega akiwakubalia kuwapatia kiasi cha Sh. milioni 4 hivyo akawaomba wafike dukani hapo wakazichukue ndipo Samwel akanaswa huku mwenzake akifanikiwa kutoka nduki.
“Jamaa wameshanitia hasara sana. Mara ya kwanza walikuja dukani wakawakuta wadogo zangu, wakaanza kukagua vitu wakiwaambia mashine zetu za risiti ni mbovu hivyo watoe fedha ya faini ambapo walichukua zaidi ya shilingi laki mbili.
“Hali hiyo haikukoma, juzikati tena wakaja ndiyo nikaamua kuwatega kwa kuwakubalia na leo nimemkamata mmoja wao, nashukuru Mungu kwani jamaa mwenyewe amesema kuwa siyo afisa wa TRA.
“Wakati wamekuja, huyu jamaa (Samwel) alikuwa anapiga mkwara mzito kuwa ni afisa wa TRA, kusema kweli nimejaribu sana kumlinda lakini kutokana na mwenzake kukimbia, amejikuta akipokea kichapo cha wananchi hivyo nikamfungia dukani hadi polisi walipofika na kumchukua kwenda naye Kituo cha Polisi cha Urafiki, Ubungo.
“Nimefika kituoni hapo tumeambiwa huyu jamaa atashikiliwa kwa ajili ya kuwezesha uchunguzi na upelelezi kwani polisi wanajipanga kuwakamata wenzake,” alisema Hamza.