Stori: Hashim Aziz, UWAZI
Dar es Salaam: Wakati Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli akihimiza wananchi wote kufanya shughuli zao kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria, imebainika kwamba makanisa mengi nchini yanaendesha shughuli zake bila kuwa na usajili unaotambulika na serikali.
Akizungumza katika mahojiano na Uwazi ofisini kwake, Afisa Habari wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Isaac Mwintanga (picha Uk. 4), alisema makanisa mengi nchini, huwa yanaanza kwa mtu mmoja au kikundi cha watu kuanza kuhubiri sehemu ndogo, baadaye wakipata waumini wengi, hufungua makanisa kiholela bila kufuata taratibu za kisheria zinazowataka kujisajili.
“Unajua kuhubiri neno la Mungu siyo makosa kwa sababu unahubiri amani lakini unapowakusanya waumini wengi bila kufuata taratibu, unakuwa unavunja sheria,” alisema Mwintanga na kuongeza kuwa hawana ugomvi na watu wanaotoa huduma ya neno la Mungu mitaani lakini ni muhimu wafuate sheria kwa kujisajili.
Mwintanga aliongeza kwa kuwaonya waumini kwamba nao wanapaswa kuwa makini na sehemu wanazoabudia ili kujua kama zimesajiliwa na zinatambulika kisheria kwa sababu ni makosa kufanya mkusanyiko bila kuwa na kibali na inapotokea hivyo, wote waliokusanyika wanaweza kuwa na hatia.
Aliongeza kuwa taratibu za usajili wa taasisi za dini zinafanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani inayoongozwa na Waziri Charles Kitwanga, kupitia kitengo cha usajili na kwamba viongozi wote wa makanisa ambao hawajajisajili, waende ofisini hapo ili kutimiza hitaji hilo la kisheria.
Juhudi za gazeti hili kumpata Waziri Kitwanga ili aongee chochote kuhusu suala hilo ziligonga mwamba kutokana na kuwa visiwani Zanzibar kikazi. Uwazi linaendelea na uchunguzi ili kubaini orodha ya makanisa ambayo hayajasajiliwa na uchunguzi utakapokamilika, itawekwa hadharani kupitia gazeti hili.