Katika makala iliyopita tumeona mengi kuhusu magonjwa haya hasa makundi ya watu walio hatarini kuyapata.
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani ya mwaka 2002, ilichambua na kubainisha baadhi ya hatari zinazoweza kusababisha mtu kupata magonjwa yasiyoambikiza ambayo ni: –
Kuongezeka kwa shinikizo la damu mara kwa mara, kuongezeka kwa lehemu kwenye damu, matumizi ya sigara, unywaji wa pombe na uzito mkubwa.
Mambo mengine yanayohusiana na hayo katika kusababisha mtu apate magonjwa haya yasiyoambukiza ni hali ya kiuchumi na kijamii, uwe unao uwezo kifedha au huna uwezo inategemea mpangilio wako wa maisha ukoje.
Sababu zote hizo zinaweza kusababisha mtu akaathirika kiafya kama vile kupata magonjwa ya moyo, kiharusi na kisukari.
Kwa hiyo suala kubwa hapa ni kujipanga kwa kula mlo mzuri na kufanya mazoezi. Sababu za kimazingira husababisha athari kubwa kiafya. Kwa hiyo magonjwa haya yasiyoambukiza husababishwa zaidi na sababu zilizo nje ya mwili lakini zinaathiri mwili, mfano; mionzi ya jua, lishe isiyo ya afya yaani inaweza kukufanya unenepe sana au uwe na uzito mkubwa, uchafuzi wa mazingira na utaratibu usiofaa kimaisha.
Magonjwa yatokanayo na vyanzo hivi ni magonjwa mbalimbali ya moyo, magonjwa ya mfumo wa hewa hasa kwa wavuta sigara, kisukari, maumivu sugu ya kiuno na haya huwapata zaidi watu wasiofanya mazoezi.
Pia utapiamlo kama hupati lishe ya kutosha, saratani ya ngozi kutokana na mionzi ya jua, uzito mkubwa wa mwili.
Lipo kundi lingine la magonjwa haya yasiyoambukiza ambalo husababishwa na sababu za kurithi. Magonjwa haya hutokana na makosa katika vinasaba, ambapo hutokea athari mbalimbali katika vinasaba na viasili mwilini hivyo kusababisha magonjwa kama mtindio wa ubongo.
Magonjwa yasiyoambukiza yanayoendana na mabadiliko ya mfumo wa maisha huwa yanatibika au yanazuilika endapo kila mmoja atazingatia kanuni bora za maisha ambazo ni kula chakula bora na kufanya mazoezi, kuepuka vihatarishi kama uvutaji sigara, unywaji wa pombe, kulala usingizi wa kutosha na kuishi katika mazingira salama.
NINI CHA KUFANYA?
Ili kuepuka magonjwa haya ni vyema kuendelea na mipango madhubuti wewe mwenyewe kuhakikisha unabadili mtindo wa maisha na unaepuka vihatarishi tulivyokwishaeleza.
Magonjwa haya huchangia sana katika kupunguza umri wa kuishi. Magonjwa mengi huanza kujitokeza katika umri kuanzia miaka 40 na ukichunguza wagonjwa wengi wanaojaza kliniki ni kati ya umri wa miaka 40 na 70.
Kwa hiyo ni vema kujiwekea mpango mahususi kama mtu binafsi, familia na jamii kwa ujumla.