×

Upandikizaji wa Kwanza wa Uso na Mikono

MMAREKANI Joe DiMeo (22), alifanyiwa upasuaji wa kwanza wa uso na mikono wa saa 23 huko New York, NYU Langone, uliofanywa na timu ya zaidi ya wahudumu wa afya 140 mwezi Agosti, mwaka jana (2020).

 

 

Ajali ya gari mwaka 2018 ilimwacha DiMeo na majeraha ya kuungua kwa kiwango cha zaidi ya 80% ya mwili wake. Vidole vyake vilikatwa na alipoteza midomo na vigubiko vya macho.

 

 

Yeye mwenyewe alisema operesheni hiyo ilimpa “nafasi ya pili maishani”.

 

 

Siku ya tukio, DiMeo alikuwa akirejea nyumbani kutoka zamu ya usiku alipolala kwenye usukani. Gari lake liliacha njia likapinduka na  likawaka moto.

 

 

Alikaa miezi minne katika kitengo kinachoshughulika na wagonjwa walioungua moto, ambacho kilijumuisha wakati alipokuwa hana fahamu. Kisha alifanyiwa upasuaji zaidi ya mara 20 wa kuurekebisha mwili wake.

 

 

Mwaka 2019, alipelekwa kwenye kituo cha matibabu cha kitaalamu  ambapo alifanyiwa upasuaji wa upandikizaji wa ngozi mwezi Agosti, mwaka jana.

 

 

Eduardo Rodriguez, Mkurugenzi wa Programu ya kupandikiza uso, alisema: “Tulitaka kumpa siyo tu operesheni ambayo ilimfanya aonekane vizuri, lakini mwishowe ilibidi ifanywe kazi nzuri zaidi  hasa kwenye mikono.”

 

 

DiMeo alikaa siku 45 akiwa chini ya uangalizi baada ya upasuaji na miezi miwili zaidi hospitalini, ambapo alilazimika kujifunza jinsi ya kufungua vigubiko vya macho na kutumia mikono yake mipya.

 

 

Upandikizaji wa uso na mikono miwili uliwahi kufanyika hapo awali lakini  haukufanikiwa. Mgonjwa mmoja alikufa kutokana na changamoto na mwingine mikono yake iliondolewa baada ya kushindwa kufanya kazi, hospitali ilisema.

 

 

Rodriguez anasema DiMeo, ambaye hufanyiwa hadi saa tano za ukarabati kwa siku, ndiye “mgonjwa aliye na motisha zaidi” aliyewahi kukutana naye.

 

 

“Anataka kufanya kazi kwenye michezo, anapenda kucheza gofu, na anataka kurudi kwenye kozi. Ninavutiwa kila wakati na kiwango cha uzani ambao anaweza kuinua,” anaongeza Rodriguez.

 

 

DiMeo anasema sasa anaweza kufanya mazoezi mwenyewe na kutayarisha kifungua kinywa chake. “Hii ni zawadi ya mara moja katika maisha, na natumaini familia inaweza kupata faraja kujua kuwa sehemu ya wafadhili inaishi na mimi,” alisema na kuongeza: “Wazazi wangu na mimi tunashukuru sana kwamba nimepewa nafasi hii ya pili.”

Leave a Comment