ILIPOISHIA GZETI LA AMANI LA JANA:
“Wengi wao bwana Tolu wanakuwa ni majini na wanachanganyana na wanadamu. Ndiyo maana unaweza kukuta mtu anaogelea kila siku majini, lakini siku moja anatoweka katika mazingira ya kutatanisha, unadhani ni nini kama siyo kuchukuliwa na majini kwenda nao kwao,” alisema Nurdin, nikakumbuka swali moja la adhabu mbalimbali wanazopewa majini mara baada ya kushitakiana.
“Na vipi kuhusu adhabu Nurdin? Maana siamini kama majini wanaweza kushitakiana.”
SASA ENDELEA MWENYEWE…
“
Majini wana adhabu nyingi sana bwana Tolu. Wana adhabu ya kumtenga jini aliyetenda makosa, wana adhabu ya kumrudisha duniani jini aliyekosa na asirudi tena ujinini na pia wana adhabu ya kumfanya awe na matatizo ya akili ya kudumu.
“Kwa hiyo kuna watu wengine wana matatizo ya akili lakini hawaponi na wala hawajulikani makwao ni wapi, wapo kila siku mitaani na majalalani wakitafuta vyakula wale.
“Haya yote mimi niliambiwa na mtaalam wangu mmoja kule Mombasa ambaye mara kwa mara ndiyo amekuwa akinitengeneza ili kunikinga na madudu ya baharini,” Nurdini aliniambia hayo yote mpaka nikaogopa.
Tuliendelea na safari, tukafika eneo fulani ambapo jua lilionekana kuwa jekundu sana kama damu na likapoteza mng’aro wake. Hakukuwa na mionzi. Hali ya hewa ilipooza.
“Nurdin ni nini hii?”
Hapo tulikuwa tumekaa juu kabisa ya meli tukiangalia mazingira ya majini.
“Bwana Tolu hata mimi mwenyewe nashangaa hivi, sijui ni nini?”
Bwana mmoja wa Kizungu tuliyekuwa naye kwenye meli hiyo akasema kwa Kiingereza licha ya kwamba pia alikuwa anakijua Kiswahili, lakini tafsiri yake akimaanisha:
“Hapa bahari ipo juu. Ni ukanda wenye mvutano kati ya anga na majini. Binadamu hawezi kuishi na akiishi ngozi yake itapoteza rangi ya asili na kuwa kama ya kenge.”
“Kwa wanasayansi wanaokwenda mwezini, wanapoiangalia dunia wanaiona ina baka kubwa na ni hili eneo. Lina kilomita za mraba nyingi kidogo.”
Nilimwelewa yule Mzungu, anaitwa Kasha. Lakini naye alinipoteza aliposema wanasayansi waliokwenda mwezini wakiiangalia dunia, kwani mtu akiwa mwezini anaiona dunia!
Ili kujielimisha zaidi, niliamua kuuliza maana kuuliza si ujinga. Lakini nilishangaa kumbe hata Nurdin alikuwa hajui kama mtu akiwa mwezini anaweza kuiona dunia, Kasha akafafanua, safari hii akatumia Kiswahili safi kabisa:
“Jua, mwezi na dunia na sayari nyingine zipo sambamba. Kama machungwa yanavyopangwa chini. Mtu anapokwenda mwezini, anapaa lakini akivuka nguvu ya mvutano anaingia kwenye anga lingine kwa hiyo chombo kinachokwenda mwezini kinakuwa hakipai tena, kinakuwa kama ndege inayotoka nchi moja kwenda nchi nyingine na kutua.
“Akishatua, ili aione dunia, inabidi aangalie juu kama vile mtu aliyepo duniani anavyotaka kuuangalia mwezi. Na dunia huonekana hivyohivyo.
“Chombo kilichopo mwezini, kikitaka kurudi duniani, nacho kinapaa juu kwanza mpaka kuvuka nguvu ya mvutano na kujikuta kinatua duniani. Ni maajabu ya uumbaji wa Mungu lakini wanasayansi wao wanajua zaidi.
“Sasa unapokuwa mwezini, ukiiangalia dunia inakuwa na alama kama vile sisi tunavyouangalia mwezi. Miongoni mwa alama ni pamoja na eneo hili ambalo kitaalam inaonekana kama bahari ipo juu ndiyo maana jua linapoteza nuru, rangi nyekundu na pia kuna baridi sana.”
Niliuliza tena kwamba, kama bahari iko juu ina maana imekaribia jua, je ni kwa nini kuwe na baridi kiasi kile badala ya kuwa na joto zaidi?
“Unavyozidi kulifuata jua, baridi inakuwa kali sana. Hata makwenu, mikoa yenye baridi sana ni ile iliyo juu kutoka usawa wa bahari. Tolu hujasikia kwenu kwenye Mlima wa Kilimanjaro, kule juu kuna baridi sana wakati ni juu kutoka usawa wa bahari?”
“Ni kweli,” nilikubali haraka sana.
Basi, Mungu alitusaidia sana, tukapita salama eneo hilo lakini pia sikuona miongoni mwa wafanyakazi wenzangu waliokuwa wakiogopa ile hali. Nikajua ni jambo la kawaida kwao maana wamekuwa kwenye kazi ya ubaharia kwa muda mrefu.
Meli ilifika mahali ambapo kulia hakuna kilichoonekana, kushoto hakuna kilichoonekana, mbele na nyuma pia hakuna kilichoonekana. Ni maji tu yalikuwa yakichanjwa na mapanga ya meli. Hali ilikuwa ya utulivu kuliko wakati mwingine wowote ule.
Ghafla umbali wa mita kama hamsini kutoka kwenye meli tukawaona wanawake wakiwa wamevaa magauni meupe na wakitushangilia kwa kunyoosha mikono juu. Walikuwa kundi ambapo kwa mahesabu ni kama hamsini hivi.
Niliwaogopa maana nilipowakazia macho niliwaona kama wanatembea juu ya maji.
“Bwana Tolu usifanye kitu chochote kile. Usipunge mikono juu wala usishuke kwenda chini. Wewe waangalie tu. Basi, niliwaangalia kweli kwani wenzangu wote walitulia wakiwaangalia tu. Waliendelea kutupungia mikono kama vile watu wanavyofanya pale kiongozi fulani anavyotembea eneo akiwa ndani ya gari.
Je, ni kiliendelea? Usikose kusoma mkasa huu kwenye Gazeti la Amani, Alhamisi ijayo.