Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanatenganishwa wakiwa bado wadogo kufuatia tukio baya la kigaidi linalotokea wakiwa mapumzikoni na wazazi wao nchini Kenya, kwenye kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi.
Katika tukio hilo, baba wa watoto hao, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa wanapigwa risasi na magaidi hao na kupoteza maisha, wakiwaacha watoto wao wakiwa bado wachanga.
Kila mmoja anapitia maisha tofauti kabisa, Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango ambaye anaishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Arianna anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kuamua kumuoa. Baadaye, Arianna ananasa ujauzito wa Diego na wanapanga njama za kutoroka.
Msichana huyo anafanikiwa kutorokea nchini Kenya, jambo linalomfanya Msuya atangaze dau nono.
Hatimaye, pacha wa Arianna, Brianna anapatikana na kila mtu anaamini kwamba ndiyo Arianna na Diego anashiriki kuandaa mpango wa kumuaminisha Msuya kwamba huyo ndiye Arianna na tayari amefika nyumbani kwa Msuya lakini anaonesha tofauti kubwa ya kitabia na Arianna, jambo linalomshangaza kila mtu.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Baada ya kila mmoja kutulia, waliondoka hospitalini hapo na kwenda kwenye hoteli ya kifahari ya Crater View, iliyokuwa inatumiwa sana na watalii. Msuya akalipia kila kitu ikiwa ni pamoja na chakula cha mchana na usiku, wakaingia ndani ya vyumba vya kisasa vya hoteli hiyo.
Kama ilivyokuwa mara ya kwanza, Msuya alimkumbatia tena Brianna, akashindwa kumzuia zaidi ya kutulia huku mapigo ya moyo wake yakizidi kuongezeka kasi. Sekunde chache baadaye, msichana huyo alikuwa ni kama amezinduka kutoka usingizini, akamsukuma Msuya na kujitoa kwenye mikono yake na kukimbilia kwenye chumba kingine.
“Nahisi anahitaji nimtafutie mtaalamu wa saikolojia atakayemsaidia kuondokana na hali hii aliyonayo, hayupo sawa kabisa,” alijisemea Msuya, akashusha pumzi ndefu na kujilaza kwenye kochi, akatoa simu yake na kumpigia yule daktari waliyetoka kuonana naye muda mfupi uliopita.
“Hellow boss!” (Halo bosi)
“Hellow doctor! I need your help please!” (Halo daktari! Nahitaji msaada wako tafadhali).
“Im listening boss!” (Nakusikiliza bosi).
“It seems my wife has a serious psychological disorder! May be its because of what happened to her, she has been through a very dangerous trespass. Can you help me to find a qualified psychologist to treat her?)
(Inaonesha mke wangu ana matatizo makubwa ya kisaikolojia, pengine ni kwa sababu ya matukio yaliyomtokea, amepitia mapito hatari sana. Unaweza kunisaidia kumtafuta mtaalamu wa saikolojia aliyebobea ili amtibu?)
“Worry out boss, I will!” (Usihofu bosi, nitafanya)
“May God bless you doctor! I love her so much and I don’t want to see her suffering!” (Mungu akubariki daktari, nampenda sana, sitaki kumuona akiteseka)
alisema Msuya wakati akizungumza na simu na daktari huyo, Brianna aliyekuwa chumba cha pili akawa anasikiliza mazungumzo yote kati ya Msuya na daktari huyo. Kwa kuwa Kiingereza hakikuwa kikimpa taabu, alielewa kila kitu walichokuwa wanazungumza.
“Maskini! Alikuwa anampenda sana mke wake, hata sijui alikuwa anamuonesha mapenzi kiasi gani ambayo mimi nashindwa kumpa na kumfanya afurahi!
“Lakini nikikubali kufanya naye mapenzi si atagundua kwamba mimi ni bikra wakati mkewe tayari alishakuwa na ujauzito? Si uongo wangu wote utafahamika?” Brianna aliendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu, akaegamia ukuta huku machozi yakianza kumlengalenga. Alishindwa kuelewa afanye nini kumsaidia.
Hakuwa na habari kwamba Msuya alishamaliza kuzungumza na simu na kutoka mpaka jirani kabisa na pale alipokuwa amesimama, akiwa ameegamia ukuta.
“Mke wangu, nini kinakuliza jamani?” alisema Msuya kwa upole.
“Hamna kitu, najisikia tu vibaya,” alisema Brianna huku akifuta machozi na kugeukia ukutani. Msuya alimsogelea na kumkumbatia tena, akambusu kwenye paji la uso huku akitoa kitambaa na kuanza kumfuta machozi.
Akilini mwake, alihisi mwanamke huyo analia kwa sababu ya ujauzito wake kuharibika, akawa anamfariji kwamba kila kitu kilichotokea ni mipango ya Mungu na wanapaswa kumshukuru kwa kila jambo. Hakuwa na habari kwamba mwenzake alikuwa akilizwa na kitu kingine kabisa.
Siku hiyo walishinda pamoja ndani ya hoteli hiyo, Msuya akawa anajaribu kumpigisha stori za hapa na pale, muda mwingine akawa anafanikiwa kumfanya acheke. Kadiri alivyokuwa anazidi kukaa naye jirani, Brianna alianza kuhisi hali tofauti ndani ya moyo wake.
Ile hofu aliyokuwa nayo juu ya mwanaume huyo, ikaanza kupungua na kutokana na jinsi alivyokuwa akimfanyia mambo mazuri kila dakika, alianza kuhisi hali tofauti ndani ya moyo wake ambayo hakuwahi kuihisi.
Mpaka muda wa kulala unafika, Brianna hakuwa akimuogopa tena Msuya kama mwanzo ingawa bado ndani ya kichwa chake aliendelea kuteseka na mawazo ya juu ya kitakachotokea endapo mwanaume huyo akiujua ukweli.
Walipopanda kitandani, Msuya alimvutia Brianna kifuani kwake na kumkumbatia, tofauti na siku zote ambazo Brianna alikuwa akijitoa akiwa hataki kabisa kukumbatiwa, siku hiyo alitulia, na yeye akapitisha mkono wake mmoja kwenye shingo ya Msuya na kumkumbatia, jambo lililomfurahisha sana Msuya.
“Mke wangu!” alisema Msuya kwa sauti ya chini, mikono yake ikiwa inafanya utalii kwenye maeneo mbalimbali ya mwili wake, hali iliyomsisimua sana Brianna kwani hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kukumbatiwa na mwanaume akiwa katika hali hiyo.
“Abeee,” aliitikia Brianna kwa sauti ya kukatakata iliyokuwa inatokea kwenye pua, pumzi zikiwa zinamtoka kwa fujo mithili ya mtu aliyetoka kukimbia mbio za mita mia moja.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.