Wachezaji wa Yanga wakishangilia goli.
Na Hans Mloli, Dar es Salaam
YANGA imepunguza tofauti ya pointi kati yake na Simba baada ya jana Jumapili kushinda mabao 3-1 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 53 huku ikiwa imebakiwa na michezo miwili mkononi kuifikia Simba iliyo kileleni na pointi 57 ikiwa imecheza mechi 24. Azam FC bado ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 51 baada ya jana kutoka sare ya bao 1-1 na Toto Africans.
Katika mchezo wa jana ambao kuna wakati ulikosa ufundi kutokana na uwanja kuteleza, Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya 12 na pointi 25 kabla ya mchezo huo, ilianza vizuri lakini baadaye haikuweza kubaki katika kiwango chake.
Kagera ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tisa lililofungwa na Mbaraka Yusuph ambaye aliunganisha vizuri pasi ya beki wa kulia Salum Kanoni.
Baada ya kuingia kwa bao hilo, Kagera inayonolewa na Adolf Rishard ilionekana kutawala mchezo lakini Yanga ilisawazisha dakika ya 25 kwa bao safi la kichwa lililofungwa na Donald Ngoma akiunganisha krosi ya Juma Abdul.
Yanga ilikosa penalti dakika ya 34 baada kipa Andrew Ntala wa Kagera Sugar kudaka penalti ya Kelvin Yondani ambayo ilipatikana baada ya Ngoma kuangushwa na Shaaban Ibrahim ndani ya eneo la hatari. Timu hizo zilienda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa Kagera kupata pigo dakika ya 47 baada ya Ibrahim kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kisha nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu Ngoma.
Yanga ilionekana kutumia vizuri upungufu wa Kagera Sugar kwani ilipata mabao mawili kupitia kwa Amissi Tambwe dakika ya 62 akipokea pasi ya Simon Msuva na Haji Mwinyi aliyefunga kwa kichwa dakika ya 89 akimalizia kona ya Msuva.
Yanga ilikosa bao dakika ya 65 baada ya shuti kali lililopigwa na Juma Abdul akiwa nje ya 18 na kugonga mwamba likiwa limemshinda kipa wa Kagera, Ntala.
Kagera ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Martine Lupati, Yusuph na Paul Ngalyoma na nafasi zao kuchukuliwa na Ibrahim Job, Ramadhan Kiparamoto na Idd Kurachi, Yanga iliwatoa Deus Kaseke, Tambwe na Abdul na nafasi zao kuchukuliwa na Geofrey Mwashiuya, Paul Nonga na Pato Ngonyani.
Kutoka Mwanza, Johnson James anaripoti kuwa, Toto Africans imetoka sare ya bao 1-1 na Azam FC katika mchezo wa ligi hiyo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Katika mchezo huo, Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 23 lililofungwa na John Bocco lakini wenyeji Toto walisawazisha dakika ya 39 kupitia kwa Wazir Junior.
Kivutio kikubwa baada ya mchezo huo, Kocha wa Azam, Stewart Hall aligeuka mbogo na kutaka kumvaa mwamuzi Jimy Fanuel kutoka Shinyanga. Katika matokeo mengine, JKT Ruvu imeifunga African Sports bao 1-0 na Ndanda FC imetoka suluhu na Prisons