STORI: Stephano Mango, Wikienda
Ruvuma: Jeshi la Polisi mkoani hapa, limewatia mbaroni waendesha bodaboda 20 wa Manispaa ya Songea ambao wamemshambulia Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) wa Kikosi cha 411 KJ cha Ruhuwiko kilichopo wilayani humo kwa kumjeruhi na kulivunja gari lake kwa mawe baada ya kumgonga mtembea kwa miguu.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilijiri mishale ya saa 3:00 usiku, mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya ‘mjeda’ huyo, Samweli Nginila (32) kudaiwa kumgonga mwanamke aliyefahamika kwa jina la Bahati Mbero, mkazi wa Majengo wilayani humo ambaye haikuelezwa aliumia kiasi gani.
Ilielezwa kuwa, baada ya tukio hilo, ilidaiwa mwanajeshi huyo aliwasha gari lake aina ya Nissan X-trail ili aondoke eneo la tukio kujisalimisha polisi ndipo bodaboda hao walimshambulia na kumjeruhi mwilini hivyo kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma (HOMSO) ambako amelazwa kwa matibabu.
Mbali na kujeruhiwa na gari lake kuvunjwa, mwanajeshi huyo alipoteza simu mbili, waleti iliyokuwa na vitambulisho vya kazi, kupigia kura, kadi za ATM na shilingi laki moja na ishirini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, ACP Zuberi Mwombeji alithibitisha kutiwa mbaroni kwa bodaboda hao huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.