×

Rais Auawa na Msanii Kwenye Jumba la Sinema

What-if-Abraham-Lincoln-Had-LivedHebu vuta picha, mheshimiwa rais amejumuika na familia yake katika uzinduzi wa filamu kwenye ukumbi maarufu nchini, wasanii mbalimbali wa filamu pamoja na watazamaji wamejumuika naye.

Wakati filamu ikiendelea kuoneshwa, ghafla unasikika mlio wa risasi na sekunde chache baadaye, rais anaonekana akiwa amelala chini, damu nyingi zikimwagika kichwani! Ni tukio la ajabu si ndiyo? Basi kwa taarifa yako, tukio kama hilo limewahi kumtokea aliyekuwa Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln.

Ilikuwaje? Aprili 14, 1865, Rais Lincoln akiwa na familia yake, walijumuika katika ukumbi maarufu wa filamu jijini Washington uitwao Ford’s Theatre nchini Marekani. Siku hiyo kulikuwa na uzinduzi wa filamu ya vichekesho ya msanii Laura Keene iitwayo Our American Cousin.

Hicho kilikuwa ni kipindi kifupi tangu kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, iliyodumu kwa kipindi kirefu. Licha ya kumalizika kwa vita, bado kulikuwa na makundi hasimu yaliyokuwa yakiupinga uongozi wa Rais Lincoln.

Msanii maarufu wa filamu enzi hizo, John Wilkes Booth, alikuwa miongoni mwa waliokuwa wakimpinga rais huyo ingawa hakuwahi kujionesha hadharani. Kwa kuwa alikuwa maarufu, hakuna mtu aliyemtilia mashaka Booth kwamba anaweza kuwa na dhamira ovu ndani ya moyo wake.
Wakati filamu ikiendelea kuoneshwa, Rais Lincoln akiwa katika chumba maalum ukumbini humo, akicheka kwa furaha na familia yake, Booth alitokeza kwa nyuma, akamchoma kisu mlinzi wa rais na kufumba na kufumbua, akafyatua risasi iliyompiga Rais Lincoln kisogoni, akapiga mayowe na kudondoka chini.

Mlio wa risasi na mayowe aliyoyapiga Rais Lincoln, viliwafanya watu wahisi kwamba ni sehemu ya filamu hiyo lakini kelele za mkewe, Mary aliyeanza kulia kwa sauti ya juu akiomba msaada pamoja na purukushani za mlinzi aliyechomwa kisu aliyekuwa akijitahidi kumdhibiti Booth, ndizo zilizofanya watu washtuke na kugundua kwamba kumbe kulikuwa na tukio la mauaji.

Licha ya ulinzi mkali uliokuwepo ukumbini hapo, Booth alifanikiwa kutoka bila kukamatwa mpaka nje ya ukumbi ambapo alitoroka kwa kutumia farasi kuelekea kusikojulikana.
Jitihada za kuokoa maisha ya Rais Lincoln ziligonga mwamba kutokana na eneo risasi hiyo ilipopiga, hatimaye akaaga dunia.

Zaidi ya wanajeshi 10,000 walisambazwa nchi nzima na kuanza kumsaka Booth na baada ya kazi nzito, hatimaye alikutwa akiwa mafichoni na rafiki yake, David Herold, Virginia. Askari wakawataka kujisalimisha lakini Booth aligoma, akapigwa risasi shingoni iliyomuua.

Wenzake wanne alioshirikiana nao katika njama hizo, akiwemo mwanamama Mary Surratt, walihukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Leave a Comment