×

Sitasahau Nilivyokumbana na Jini Mwanaume-14

ILIPOISHIA WIKIENDA
Tulipofika nyumbani ndipo nilipoeleza yaliyonikuta. Nilianzia yale ya Zanzibar, nikamalizia na ile simu aliyonipigia Smith.
Dada na mume wake wakashangaa.
“Ndiyo maana nikakukuta unalia?” Shemeji akaniuliza.
“Nisilie, unayaona hayo ni madogo?” nikamuuliza.
“Kwa kweli ni makubwa.”
“Lakini Enjo mdogo wangu, matatizo uliyataka mwenyewe, kwa nini mtu anakutongoza unamkubali wakati hamjuani?” Dada akaanza kunilaumu. SASA ENDELEA…


Sasa dada mimi nilijuaje kama ni jini? Utanilaumu bure. Mimi nilijua ni binadamu kama binadamu wengine, kumbe najiingiza kwenye matatizo nisiyoyajua. Tena ameniambia ameshika kivuli changu, sitaweza kumuepuka na nisipomkubali atanitia kwenye matatizo.”
Nilipowaeleza hivyo nikaanza tena kulia.
“Kwa matukio hayo ya Zanzibar, huyo jini tayari ameshakutia kwenye matatizo. Sasa kama unatafutwa na polisi, utasema kuna usalama hapo?” Dada akauliza.
Mimi niliendelea kulia nikiamini kuwa maisha yangu yalikuwa yamekwisha.
Kusema kweli nilijuta kukutana na jini yule.

“Lakini tusemeni huku na huku, hao polisi wa Zanzibar wanamtafuta, wanamjuaje au walimuona wapi?” Shemeji akahoji.
“Si huyo jini amemwambia kuwa anatafutwa na polisi,” dada akamjibu.
“Pamoja na kuambiwa na huyo jini na sisi tutafakari katika akili zetu. Polisi wanamkamata mtu wanayemfahamu, huyu hawamfahamu. Mimi sioni kama ni kitu cha urahisi kuja hapa Dar na kumkamata. Afadhali angekuwa yuko Zanzibar.”
“Na mimi sitaenda tena huko,” nikajisemea.
“Uende umfuate nani wakati unayemfuata ameshauawa?” dada akaniuliza.
“Ndiyo sitaenda.”
“Kutokana na haya mambo yalivyo, hapa shauri liliopo ni kutafuta mganga atakayemshughulikia Enjo,” Dada akatoa wazo.

“Hilo ndilo wazo nililonalo mimi,” nikamwambia na kuongeza:
“Hiyo kesi kama ipo tuiue na huyo jini afanyiwe kafara asinifuate tena.”
“Sasa mganga tutampata wapi?” Shemeji akauliza.
“Wanatoaga matangazo yao kwenye haya magazeti. Tena kwenye gazeti la leo niliona tangazo la mganga mmoja anatoaga majini na kuua kesi. Hebu ngoja nikalilete lile gazeti.”
Dada akainuka na kuingia chumbani. Alipotoka alikuwa ameshika nakala ya gazeti fulani akaja nalo sebuleni na kuketi. Alifungua ukurasa mmoja mmoja huku akivitupia macho kwa makini vichwa vya  habari. Ghafla akaliona hilo tangazo alilotuambia.
“Enhe tangazo lenyewe hili hapa.”
Mimi na shemeji tukalisogelea gazeti na kulitupia macho tangazo hilo.
Lilikuwa tangazo la mganga wa kienyeji aliyekuwa akitoa majini, kuua kesi na kutoa dawa za mvuto wa kimapenzi.
Aliweka picha yake. Alikuwa mtu mzima aliyevaa kanzu na kofia ya darizi na kuonekana kama ustadhi wa madrasa.
Alijitambulisha kama mganga wa majini kutoka Tanga na alikuwa akipatikana maeneo ya Tegeta jijini Dar.
Kwa vile alikuwa ameweka namba yake ya simu, dada alishauri tumpigie tumueleze lakini shemeji akasema isingekuwa vyema kumpigia simu usiku ule.
“Tusubiri asubuhi.”
“Basi tutampigia asubuhi,” dada akamkubalia.
Usiku ule kwa sababu ya hofu ilibidi nilale na dada  katika chumba nilichokuwa nikilala. Shemeji alilala peke yake. Nilijua kuwa alikasirika lakini hapakuwa na jinsi.

Kulipokucha baada ya kupata kifungua kinywa nilirudisha betrii kwenye simu yangu nikampigia yule mganga.
Alikuwa mswahili hasa kwani baada ya kupokea simu yangu aliniambia:
“Assalaam alaykum.”
Na mimi nikamuitikia kama mswahili.
“Waalayka salaam. Shikamoo.”
“Marahaba. Nani mwenzangu?”
“Mimi naitwa Enjo niko Sinza. Nina shida yangu.”
“Shida gani mama?”
“Kuna jini ananifuatafuata….”
Kabla sijamaliza kusema akadakia:
“Hiyo ndiyo kazi yangu mama. Mimi nafukuza majini wabaya, nazindika nyumba, natoa dawa za mvuto wa kimapenzi na nashughulikia matatizo mbalimbali.”
“Nimekuelewa. Sasa ngoja nikueleze vizuri.”
“Haya nieleze.”
“Huyo jini ananifuata waziwazi akiwa na umbo la kibinadamu na kunitaka kimapenzi….”
Mganga akang’aka:
“Kumbe ni majini wa aina hiyo! Hao wanasumbua sana mama.”
“Hutaweza kumfukuza?”
“Kwa nini nishindwe wakati ni kazi yangu. Mimi nafukuza jini hata akiwa mkubwa kama nyumba!”
“Sasa ameshanifanyia visa vingi sana na kutishia maisha yangu…”
“Usijali…usijali, mwisho wake ndiyo umefika. Wewe uje hii asubuhi nikushughulikie kabla watu hawajajaa.”
“Mengine nitakuja kukueleza huko huko.”
“Sawa. Sasa unakuja?”
“Ninakuja. Nichukue shilingi ngapi.”
“Hiyo kazi ni kubwa lakini kwanza uje na laki tano.”
Pesa alizonitajia zilikuwa nyingi lakini kutokana na tatizo lililokuwa limenikabili nilimkubalia.
“Sawa, ninakuja sasa hivi.”
“Nakusubiri.”
Nikakata simu.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.

1 Comment

Leave a Comment