HABARI za leo wapendwa wasomaji wa safu hii ya kila wiki, ni matumaini yangu kuwa mnaendelea vizuri na kazi zenu za kila siku maana hata katika vitabu vya dini vimeandikwa, asiyefanya kazi na asile.
Kama tunavyojua, watu wote hatuwezi kuwa sawa, maana wapo miongoni mwetu walioamka wakiwa wagonjwa, hawa nawapa pole na Mungu ni mwema atawaponya na kwa wale wenye misiba nawaombea subra, ishallah mtakuwa sawa, maana mbele yake sote tutakwenda!
Leo nimekuja kuwasema nyie akina dada mnaojitoa ufahamu, mkaona mkiwa na dada wa kazi, ndiyo tiketi ya kutaka kufanyiwa kila kitu, mkijiona mmeukata halafu siku inatokea mnaanza kulia eti ooh ndoa zenu zimevunjika, mmerogwa.
Mwanamke mzima, unamuachia mwanamke mwenzio anafanya kazi zako zote? Aaah hapana shosti, kuna kazi nyingine hakuna kufanya mtu mwingine zaidi yako, kama hii ya kutandika kitanda chako unachotumia na mumeo.
Kulala na mume ulale wewe, halafu msichana aje akutandikie, kumbuka kuwa mwanamke kutandikiwa kitanda na mwanamke mwenzako tena ukiwa na mume ni tatizo kubwa.
Maadili ya mwanamke aliyekamilika, hawezi kumuachia mtu akamtandikia kitanda chake na mumewe kwa sababu kwanza chumbani kwako kuna uwezekano wa mambo mengi kutendeka, msichana akaona siri zako achilia mbali kukuibia vitu vyako vya thamani.
Inawezekana msichana wako wa kazi unaishi naye vizuri kwa hiyo huoni tabu kumwachia akutandikie kitanda chako, lakini binadamu hatufanani akili, hivi hamjawahi kusikia kuhusu baadhi ya wadada wa kazi washirikina? Ni bora apate kazi kuingia chumbani kwako kuliko kwa ruhusa yako.
Utasikia mtu anakwambia, mume wangu alirogwa ndiyo maana aliniacha, lakini mke anasahau kuwa yeye ndiye sababu ya yote hayo, anaweza kuwa hakutumia ushirikina, lakini alitumia ile nafasi uliyomuachia kukaa chumbani kwako.
Huenda siku moja wakati anatandika na kusafishasafisha mumeo alirudi nyumbani ghafla, akatumia ile nafasi, si unajua tena wanaume wengi walivyo dhaifu? Wanawake wenzangu, hapo ndipo tunapokosea.
Wapo wanaume ambao wanawatongoza wadada hao na kuwakaribisha chumbani, akiwa hana ruhusa ya kuingia huko, ataogopa, maana atajua ukimkuta huko imekula kwake, maana utamuuliza alichokifuata na atakosa majibu.
Lakini kama unamtuma afagie, akutandikie kitanda chako, siku ukimkuta na mumeo ni rahisi kujitetea, kwamba yeye alikuwa anafanya kazi ndipo baba akaingia.
Wanawake tuache kurahisisha mambo kwa sababu ya uvivu wetu, siku hizi kila mtu anatafuta pa kupumulia, maana maisha magumu, nawasihi muendelee kuheshimu maadili ya ndoa, maana ni muhimu sana.
Kutokana na matatizo yetu wenyewe tunajikuta tunanyang’anywa wanaume na kubaki tukilaumu, mwanaume akipata upenyo akaona huduma zimezidi upande fulani, anahamia hukohuko.