
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anna Kilango Malecela
Na Mwandishi Wetu, RISASI Mchanganyiko
DAR ES SALAAM: Kitendo cha Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anna Kilango Malecela na Katibu Tawala, Abdul Dachi kwa kusema uongo kuwa mkoa huo haukuwa na wafanyakazi hewa, kimezua hofu kubwa miongoni mwa wateule wake katika nyanja mbalimbali nchini.
Hofu hiyo inatokana na ukweli kuwa watendaji wengi wa serikali wamekuwa na tabia ya kukubali bila kuchunguza taarifa wanazopewa na watu walio chini ya mamlaka zao, kitu ambacho kimemponza mbunge huyo wa zamani wa Same kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Kwa kweli hili jambo ni zito sana, sasa tutalazimika kufanya uhakiki sisi wenyewe kabla ya kukubali au kukataa taarifa tunazopewa, maana inavyoonekana bwana mkubwa (Rais Magufuli) anakuwa na taarifa zote kabla hajasikia kutoka kwako, kwa kweli ni hofu tupu,” alisema kiongozi mmoja mkubwa katika idara ya serikali aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Rais Magufuli ametengua uteuzi wa mwanasiasa huyo machachari ikiwa ni siku 26 tu tangu alipomuapisha yeye na wenzake Machi 15, mwaka huu katika Viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam. Kazi ya kwanza waliyopewa viongozi hao ni kuhakikisha ndani ya siku 15, kila mmoja anawatambua na kuwaondoa wafanyakazi hewa katika maeneo yao ya kazi.