Morogoro: Maumivu! Msanii wa Bongo Fleva na Nyimbo za Asili mjini hapa, Paskali Linda almaarufu Batarokota anaishi maisha ya upweke kwa madai ya mchepuko kumtorosha mkewe aliyemtaja kwa jina moja la Sara na mwanaye, Theresia.
Akizungumza na Wikienda mjini hapa kwa masikitiko makubwa, msanii huyo alisema kuwa, mwaka 2011 alifunga ndoa na Sara katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Patrisi la Msamvu mjini hapa ambapo walipewa cheti cha ndoa namba B 0129392.
Batarokota alisimulia kwa uchungu: “Mwanzoni tuliishi vizuri hapa Msamvu. Mke wangu wa ndoa, Sara au mama Juliana alitoroshwa na mchepuko akiwa na mwanangu Theresia mwenye umri wa miaka miwili.
“Ameniachia mwanangu mwingine, Makrina mwenye umri wa miaka minne akiwa mgonjwa, sitaki niongee sana kwani inaniuma ila namuomba popote alipo arudi nyumbani au afike kwenye ofisi za Gazeti la Ijumaa Wikienda (Bamaga-Mwenge), mimi nitakuja Dar kumchukua kwani Dar na Morogoro siyo mbali.
“Hii ni mara ya pili mke wangu anatoroshwa na mchepuko. Mara ya kwanza alitoroshwa mwaka jana, akamwacha mtoto wetu, Theresia aliyekuwa akinyonya. Nilihangaika sana hadi nilipompata jijini Dar na kumrudisha nyumbani lakini sasa ametoroshwa tena na huyo mchepuko wake ambaye yupo Dar.”
Alisema kuwa namba ya simu ya mkewe huyo kwa sasa haipo hewani na hata alipompigia mbele ya mwanahabari wetu ilikuwa haipatikani.
Hata hivyo, gazeti hili lilimshauri kwenda kuripoti polisi ambapo alikubali kufanya hivyo ili kumpata mkewe na mwanaye.