×

Njia rahisi ya kupunguza unene zingatia haya-3

Leo naendelea kuelezea njia rahisi ya kupunguza unene, fuatana nami katika elimu hiyo.

PENDEKEZO LA 3
Kula mbegumbegu za korosho, karanga (ziwe mbichi badala ya kukaanga na chumvi) katikati ya siku. Haya ni mafuta yenye rutuba mwilini kuliko nyama za mafuta.

5-MAZOEZI YA MWILI NA VIUNGO
Mazoezi ni mfalme wa kupunguza unene. Ukiwauliza wengi watakuambia wanafanya kazi ngumu za sulubu (wanachuruzikwa jasho) kwa hiyo hayo ni mazoezi. Ila kazi na mazoezi ni vitu viwili tofauti. Ingekuwa kufanya kazi ni mazoezi basi kusingekuwa na wastani mfupi wa maisha kwa maskini hasa sisi Waafrika.

Wengine watadai kwamba walipokuwa wadogo shuleni walifanya mazoezi sasa wamekuwa watu wazima (miaka 40 kuendelea) kwamba eti mazoezi ni suala la ujana; kumbe kadiri unavyokuwa ki-umri ndivyo unavyotakiwa kufanya mazoezi na kujitazama zaidi kiafya.

Mazoezi ni shughuli inayokufanya kwanza uheme (mapafu na moyo kwenda kasi), viungo na mifupa kujinyoosha (stretching), kutoka jasho na usafishaji wa damu.

Mazoezi yanayosaidia haya ni pamoja na kutembea kwa kasi, kukimbia, kuogelea, michezo mbalimbali ya riadha (kama mpira wa miguu, nyavu, kikapu, mikono, n.k); michezo ya kupigana na kujilinda (karate, kung fu, judo, capoeira, krav maga, jiu jitsu, systema, kickboxing, thai boxing, kempo, kalari payatu, aikido, nk.

Ni muhimu mwanadamu ufanye mazoezi makali ya viungo mara mbili tatu kwa juma. Si vizuri kufanya kila siku kwani misuli na mishipa inahitaji kupumzika na kukua.

Kama unapenda kuinua vyuma lazima uwe na mwalimu wa kukuelekeza; na si vizuri kufanya kila siku. Wastani wa mara mbili tatu kwa juma inatosha kabisa.

6-UPO UFANYAJI MAZOEZI WA AINA MBILI
Mazoezi ya nguvu ya kuhema niliyotaja hapo juu (cardio-vascular) na yale laini ya kujinyoosha yaani ambayo hutumia zaidi nguvu za ndani na pumzi. Haya ya pili ni kama Yoga (India), Tai Chi Chuan (China) na aina mpya ya mazoezi iliyoanza nchi za wenzetu miaka ya karibuni yaani Pilates (hutamkwa hivyo hivyo ilivyoandikwa Pilates).
Haya laini yanawafaa zaidi watu wazima na nchini China na Japan mathalan utawakuta wazee wa miaka 80 hadi 90 bado wanayafanya. Husaidia moyo, damu na akili.

Michezo na mazoezi ya mwili ni njia kuu ya kupunguza unene, kurefusha maisha, kuchangamsha ubongo, kupunguza ulevi, uvutaji sigara, dawa za kulevya, tabia mbaya za uvivu, ugomvi, n.k. Mataifa yenye watu wanaofanya mazoezi kama Japan, Brazili, India na China huwa na wachapakazi wengi na wananchi wanaoipenda jamii yao.
Itaendelea wiki ijayo.

7-KULA SANA CHUMVI SI VIZURI
Ulaji chumvi mwingi hutokana na suala la ladha. Kisayansi vyakula vyote vina chumvi asilia sema tu tumezoea kuongezea madini hii iitwayo Sodium. Sodium inachangia sana kufupisha maisha.

Huifanya mishipa ya damu ichoke; ni kama bomba lolote la maji ukilitazama baadaye hugeuka rangi kutokana na yale maji kupita pale kila siku.

Kwa wale tunaoishi nchi za joto na kutoka sana jasho kula chumvi ni muhimu. Ila tatizo letu ni kwamba hatunywi maji ya kutosha. Mtu ukiwa na kiu unakunywa soda au kinywaji cha sukari; inakuwa kama unaendelea kuutesa mwili.

Kwa vipi? Mishipa inayopitisha damu mwilini badala ya kusaidiwa kwa maji inawekewa kazi zaidi ya kusafisha sukari na chumvi. Ndiyo maana vifo vingi vinatokea mapema; wastani wetu wa maisha haupiti miaka 50.

Utafiti uliofanywa chuo kikuu cha California, Marekani mwanzoni mwa 2010, umethitibisha kwamba vifo vingi duniani husababishwa na maradhi ya moyo na saratani ambavyo hutokana na uvutaji sigara, unene, ulevi na ulaji sana wa chumvi na sukari. Tukipunguza ulaji wa chumvi tunasaidia pia kupunguza maradhi ya moyo, utafiti unasema.

SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

Leave a Comment