Kijana mdogo, Benjamin Semzaba, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye kesi iliyokuwa inamkabili inaelekea kufika mwisho na hukumu kutolewa.
Ushahidi wote umeshakamilika na hakuna shaka kwamba Ben ndiye aliyeua kwani ukiachilia mbali ushahidi huo, yeye mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikiri kwa kinywa chake kufanya mauaji hayo.
Hatimaye siku ya hukumu inawadia, Ben akiwa amedhoofika sana na kubadilika kutokana na mateso ya gerezani, anahukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia.
Upande wa pili, historia ya maisha ya Ben inaelezwa, tangu akiwa kijana mdogo kabisa, akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake, Mtaa wa Maporomoko kwenye mji mdogo wa Tunduma.
Licha ya maisha ya kifukara anayopitia, anaonesha uwezo mkubwa darasani, anafaulu kwa kiwango cha juu na baada ya kuhitimu kidato sita, anaenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akiwa chuoni hapo, anakutana na msichana mrembo, Gladness anayetokea kumpenda sana na baada ya kumficha kwa muda mrefu historia juu ya familia yake, msichana huyo anambana na anaeleza ukweli.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Simulizi hiyo iliugusa mno moyo wa Gladness, akashindwa kuzificha hisia zake, akawa analia kama mtoto mdogo huku akiwa amemkumbatia Ben kifuani. Ilibidi kijana huyo ndiyo aanze kazi ya kumbembeleza na kumtaka achukulie kawaida kila kitu.
“Nataka kwenda kuiona familia yako, wikiendi hii nitamuomba baba atukatie tiketi mbili za ndege, tutaenda Ijumaa na kurudi Jumapili,” alisema Gladness huku akifuta machozi.
Hakuna kitu kilichomuumiza moyo wake kama kugundua kwamba kumbe Ben alikuwa akimficha hayo yote kwa sababu aliamini kwamba atamdharau na kumkimbia, akaamua kumdhihirishia kwa vitendo kwamba anampenda kwa dhati kutoka ndani ya moyo wake.
Siku hiyo ilipita huku Gladness akiendelea kusisitiza kwamba ni lazima mwisho wa wiki hiyo wafunge safari mpaka nyumbani kwao, Tunduma mkoani Mbeya.
Japokuwa alijitahidi kumtoa wasiwasi kwamba kila kitu kitakuwa sawa na kamwe hawezi kumuacha kwa sababu ya umaskini wao, kila Ben alipokuwa akifikiria jinsi itakavyokuwa msichana huyo atakapoenda kuyaona maisha halisi ya familia yao, alijikuta akikosa kabisa amani.
Hatimaye Ijumaa iliwadia, kama alivyokuwa amemuahidi, Gladness tayari alikuwa na tiketi mbili za ndege mkononi za kwenda na kurudi Mbeya. Kwa kuwa siku hiyo walikuwa na kipindi kimoja tu, baada ya kumaliza walianza maandalizi na muda mfupi baadaye, waliondoka na kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Japokuwa alikuwa na mawazo mengi, hali ambayo haikujificha hata kwenye uso wake, kwa upande mwingine alikuwa na furaha kwa sababu katika maisha yake hakuwahi kupanda ndege hata mara moja na hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza. Shauku ya kutaka kujua usafiri wa ndege unakuwaje, kwa kiasi fulani ilimpunguzia mawazo.
“Unaonekana haupo hapa kimawazo, nini kinakusumbua jamani mume wangu mtarajiwa? Au unaogopa kupanda ndege,” Gladness alimtania wakiwa kwenye jengo la abiria kusubiria ndege, Ben akajikuta akicheka mwenyewe.
Msichana huyo mrembo akaendelea kumpigisha stori za hapa na pale ili kumchangamsha mpaka sauti ya mhudumu uwanjani hapo iliposikika ikiwataarifu abiria waliokuwa wakielekea jijini Mbeya kuanza kujiandaa kulekea kwenye ndege.
Dakika kadhaa baadaye, Ben na Gladness walikuwa tayari wameshaingia ndani ya ndege na kukaa kwenye siti zao sambamba na abiria wengine, msichana huyo akawa anaendelea kumtania Ben ili kumchangamsha. Taratibu ndege hiyo ilianza kujongea kuelekea kwenye njia za kurukia (run ways).
Ikazidi kuongeza kasi huku muungurumo wa injini nao ukizidi kuongezeka na muda mfupi baadaye, ilianza kuinuka upande wa mbele kuonesha kwamba ilikuwa ikipaa, Ben akawa na hofu kubwa moyoni mwake kwani ukweli ni kwamba hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kutumia usafiri huo.
Ndege iliendelea kuinuka upande wa mbele na baada ya dakika kadhaa, taratibu ilianza kurudi kwenye hali yake ya kawaida, Ben akashusha pumzi ndefu na kumgeukia Gladness ambaye muda wote alikuwa akimtazama kwa macho yaliyojaa ujumbe mzito.
“Nakupenda sana Ben lakini sijui kwa nini huniamini, nipo tayari kuwa na wewe kwa hali yoyote uliyonayo, tafadhali nakuomba utulize nafsi yako, mimi ni wako baba,” alisema Gladness kwa sauti ya chini kisha akajilaza kwenye kifua cha Ben wakati ndege ikiendelea kupasua mawingu kwa kasi kubwa.
“Nimekuelewa mpenzi wangu lakini narudia tena kukusisitiza kwamba ukubaliane na hali utakayoikuta nyumbani kwetu,” alisema Ben, wawili hao wakabusiana kwenye midomo na kukumbatiana, safari ikaendelea.
Baada ya safari ndefu, hatimaye sauti ilisikika kutoka kwenye vipaza sauti vilivyokuwa ndani ya ndege hiyo ikiwataarifu abiria kufunga mikanda kwani ndege ilikuwa ikikaribia kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe jijini Mbeya. Ben na Gladness ambao muda wote walikuwa wamegandana kama ruba, wakaachiana na kila mmoja akafunga mkanda kwenye siti yake.
Ndege ikainama upande wa mbele na kuanza kushuka kwa kasi, dakika chache baadaye, tayari ilishaigusa ardhi ya uwanja huo, ikakimbia na kuzunguka uwanja huo kabla ya kwenda kusimama kando ya jengo kubwa uwanjani hapo.
Wakashuka na kuelekea kwenye jengo la uwanjani hapo ambapo baada ya kukamilisha taratibu za kiusalama, walichukua mizigo ya zawadi mbalimbali walizonunua kwa ajili ya mama yake Ben na wadogo zake, wakatoka na kutembea umbali wa mita kadhaa mpaka walipoikuta Barabara Kuu ya Mbeya- Tunduma.
Wakapanda basi na safari ikaendelea kwani bado kulikuwa na umbali mrefu kutoka kwenye uwanja huo mpaka Tunduma, mji uliokuwa kwenye mpaka kati ya Tanzania na Zambia. Safari iliendelea na baada ya takribani saa moja, tayari walikuwa wamewasili Tunduma.
Wakashuka kwenye basi na kupanda Bajaj iliyowapeleka mpaka jirani kabisa na nyumbani kwa akina Ben. Kadiri walivyokuwa wanazidi kukaribia nyumbani kwao ndivyo Ben alivyokuwa anazidi kukosa amani ndani ya moyo wake.
Kila alipokuwa akivuta kumbukumbu ya maisha waliyokuwa wanaishi Gladness na wazazi wake, jinsi jumba lao lilivyokuwa la kifahari, ndani likiwa na vitu vingi vya thamani kisha akakitazama kibanda chao ambacho sasa kilikuwa mita chache tu mbele yao, alijikuta akipoteza kabisa furaha.
Gladness ni kama alikuwa anajua kinachoendelea ndani ya kichwa cha Ben, kwa jinsi alivyokuwa anampenda hakutaka ajihisi vibaya hata kidogo, akawa anaendelea kumchangamsha mpaka walipowasili nyumbani kwao.
Mama yake Ben aliyekuwa akipasua kuni nje ya nyumba yao, ndiye aliyekuwa wa kwanza kumuona mwanaye, akatupa shoka lake pembeni na kujikongoja kumkimbilia Ben kwani bado afya yake haikuwa imetengemaa.
“Beeeen!”
“Mamaaaaa!”
Aliitikia Ben huku akitupa mizigo aliyokuwa ameibeba na kumkimbilia mama yake, wakakumbatiana kwa nguvu huku machozi ya furaha yakiwatoka wote wawili.
“Umekuwa baba wa nguvu mwanangu, ooh ahsante Mungu kwa kumlinda na kumkuza mwanangu,” alisema mwanamke huyo kwa furaha huku akimkaguakagua mwanaye. Ben alikuwa amebadilika mno, tofauti kabisa na wakati anaondoka kwenda kuanza chuo. Usingeweza kuamini kwamba hapo ndiyo palikuwa nyumbani kwao na huyo ndiye mama yake mzazi.
Kwa muda wote huo Gladness alikuwa amesimama pembeni huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake. Bila hata kusubiri kutambulisha, alimtambua mama yake Ben kutokana na jinsi walivyokuwa wakifanana.
“Na huyu msichana mzuri hivi ni nani mwanangu,” alihoji mama yake Ben huku akimtazama Gladness, wakawa wanatazamana.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.
SOCIAL MEDIA ZETU:
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA
INSTAGRAM: @Globalpublishers
TWITTER: @GlobalHabari
FACEBOOK: @GlobalPublishers
SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers
GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz