Diamond akiwa na mama yake mzazi, Sandra.
SANURA Kassim ni jina la mama mzazi wa msanii nyota wa Muziki wa Kizazi Kipya, Diamond Platinumz ambaye naye ana a.k.a yake, akijulikana kama Sandra.
Ni aina ya mama ambaye baada ya mateso mengi ya kuhangaika na watoto akiwa peke yake, sasa amekaa kivulini akila matunda, kwani maisha anayoishi hivi sasa, hayakuwepo akilini mwake miaka sita iliyopita.
Historia yake na Diamond inaonesha ni watu waliopitia maisha wanayopitia Watanzania wengi, ya shida, manyanyaso na karaha za kila namna. Unapomsikiliza kijana huyu ambaye sasa ni mfano kwa wasanii wengi, unagundua jinsi gani mama yake alivyompa sapoti, kwani mojawapo ya simulizi zinasema, alikuwa akienda naye kwenye matamasha ya muziki enzi hizo na hata kudiriki kumuombea ili apate nafasi ya kuimba!
Alitembea kwenye ndoto za mwanaye, akakataa kuwa kama wale wazazi wanaotaka watoto wafuate ndoto zao, ambazo wao wenyewe walishindwa kuzitimiza. Mwanaye alipomwambia anataka muziki, akamuunga mkono kwa kila hatua licha ya kwamba kipato chake kilikuwa hakimtoshi hata kutimiza mahitaji yake binafsi.
Kwa kweli ni mama anayefaa kuwa mfano kwa wazazi wengine, kwa sababu muziki siyo kama kibarua cha kubeba zege, useme ukifanya asubuhi jioni unarudi na ujira wako. Sanaa hii inataka muda na uwekezaji. Mama alivumilia akijua ipo siku mambo yatakaa kwenye mstari, kama anavyoshuhudia hivi sasa.
Hivi sasa anaishi maisha ya daraja la kwanza kwa viwango vya Bongo. Hana hofu na maisha kwa maana ya atakula au kuvaa nini. Anapata anachohitaji, tena kwa wakati.
Lakini nyuma ya yote haya, kuna jambo ambalo kwa maoni yangu, naona haliko sawa, pale unapotazama maisha ya kimapenzi ya mwanaye na jinsi yeye mama, anavyojihusisha naye. Kuna mambo mengine, mama hapaswi kumpa sapoti kwa kiwango hicho.
Diamond anapenda warembo. Huenda wanajilengesha wenyewe kutokana na umaarufu wake au pengine yeye ndiye anayewatafuta. Tatizo langu ni pale mama anapomkubali kila mwanamke anayeshiriki mapenzi na kijana wake. Simaanishi awachukie, lakini mila na desturi zetu, haziwapi wazazi uhalali huo.
Msururu wa wasichana walioshiriki mapenzi na Diamond ni mrefu hasa wale wenye majina. Na wote hawa, walipata kukumbatiwa na mama yake kwa maana ya kuwapokea, Jokate, Wema, Penny na sasa Zari. Katika hali ya kawaida, hawa ni wapenzi wake tu, hawajawa wachumba bado.
Kama mama anayehitaji kijana wake kuwa na maadili mema, hii ni tabia ambayo angepaswa kuikemea ili kumlinda mwanaye. Angekataa kupelekewa wanawake tofauti kila siku hadi siku atakapoamua kumpeleka mchumba wake.
Angekataa tabia hii tangu zamani ili kumuonesha kuwa kubadilisha wanawake hakujawahi kuwa sifa nzuri kwa wanaume. Ninajua Zari hawezi kuwa mwanamke wa mwisho kwa Diamond kumpeleka kwa mama yake na pia, mama naye atampokea kwa kumkumbatia kama kawaida yake.
Inawezekana mafanikio ya Diamond kimaisha yamemfanya mama sasa awe mwoga, kwamba kila anachofanya anaona sawa tu. Hapana, Kiafrika fedha hazijawahi kuwa kubwa kuliko wazazi na inapotokea hivyo, wengi huishia pabaya.
Mama asimame katika nafasi yake, aache kujichanganya na kupiga picha kwa pozi kama msanii. Nafasi aliyofikia Diamond hivi sasa ni hatari zaidi kwa maisha yake kiafya kuliko ilivyokuwa awali. Kila mwanamke anamtaka na simulizi zake juu ya wanawake hao, zinaonesha hatumii kinga, maana anazungumza kuhusu mimba.
Awe mkali ili ‘uhuni’ wake ubakie huko huko nje, akija ndani abakie kuwa mtoto na kama anahitaji kumleta mwanamke ndani, awe mmoja na mwenye kueleweka, siyo kila akibadili anamleta nyumbani!