×

Kuziba na kuvimba kwa mirija ya uzazi (hydrosalpinx)

Hdrosalpinx’ ni hali ambayo mirija ya uzazi ya mwanamke inakuwa inavimba kwa kujaa majimaji na inaziba upande wa mwishoni mwa mirija. Mirija hii inapovimba huwa na uvimbe kama soseji, uvimbaji huu wa mirija na kuziba huwa wa pande zote mbili, kulia na kushoto. Tatizo hili la kuvimba na kuziba kwa mirija husababisha ugumba kwa mwanamke.
Pamoja na kujaa maji pia mirija inaweza kujaa usaha au kujaa damu.

CHANZO CHA TATIZO
Kama tulivyokwishaona, tatizo hili huweza kumfanya mwanamke apoteze uwezo wa kuzaa yaani kuwa mgumba. Chanzo kikuu cha hali hii ni maambukizi katika viungo vya uzazi, ‘Pelvic Inflammatory Disease’ au kwa kifupi ni ‘PID’.
Maambukizi haya hupanda taratibu na huanzia ukeni. Kwa hiyo mwanamke anayesumbuliwa na tatizo la maambukizi ya mara kwa mara ukeni ni vema atibiwe vinginevyo baadaye anaweza kujikuta anashindwa kupata ujauzito.

Dalili za maambukizi ya mara kwa mara ukeni ambayo yanaweza kukufanya ukose uwezo wa kuzaa kwa kupata tatizo hili la ‘Hydrosalpinx’ ni kutokwa na uchafu au majimaji ukeni yenye harufu mbaya na muwasho, maumivu ukeni, maumivu wakati wa kujamiiana na kuhisi uvimbe ukeni kama gololi.

Vijidudu vya klamidia na ‘Gonorrhoea’ au kisonono au Gono kama wengi wanavyopenda kuita hutajwa kuwa chanzo kikuu cha tatizo hili la kuvimba na kuziba mirija ya uzazi.

Ingawa siyo kila maambukizi ya kizazi husababisha kuziba mirija, bali endapo mwanamke atawahi hospitali na kupata tiba sahihi anaweza kupona na asiwe mgumba.

Mwanamke mwenye tatizo hili hutokea mirija inapoharibika maana yake yai haliwezi kuchukuliwa na kuingizwa katika mirija ya mbegu za kiume kwani haliwezi kupenya.
Matatizo mengine yanayosababisha mirija ya uzazi ya mwanamke kuziba ni makovu kutokana na upasuaji wa awali wa kizazi au mirija, tabaka la ndani la kizazi kuwa nje ya kizazi na saratani ya mirija ya uzazi au vifuko vya mayai.

DALILI ZA TATIZO
Kwa ujumla dalili hutofautiana kati ya mwanamke na mwanamke lakini zipo dalili kuu za ugonjwa. Mgonjwa mwenye tatizo la kuvimba na kuziba kwa mirija ya uzazi hulalamika maumivu ya mara kwa mara ya tumbo chini ya kitovu na husambaa katika nyonga zote na kiuno, wapo wengine hawaoneshi dalili zozote ila wakipimwa ‘Ultrasoud’ au ‘HSG’ huambiwa mirija imevimba au imejaa usaha.
Mwanamke hulalamika kutoshika mimba kwa zaidi ya mwaka tangu aanze kutafuta, tumbo kuuma mara kwa mara hasa anapokuwa katika siku zake za hedhi, mzunguko wa hedhi huvurugika na kutoona ute wa uzazi, kupoteza hamu na raha ya tendo la ndoa, ingawa mwanaume akipimwa mbegu za uzazi huwa vizuri.

UCHUNGUZI
Uchunguzi hufanyika katika kliniki za madaktari bingwa wa akina mama katika hospitali za mikoa ambapo vipimo mbalimbali kama ‘Ultrasonography’, ‘Hysterosalpingogram’ au ‘Laparoscopy’ hufanyika ili kufahamu kama mirija tu au imeziba na kuvimba.
Vipimo vingine vitafanyika kadiri daktari atakavyoona inafaa, mfano vipimo vya damu kuangalia vichocheo na maambukizi, vipimo vya ukeni na shingo ya kizazi pia vitafanyika.
Kumbuka, ugonjwa huu hauhusiani na yutiai, si kila tatizo la ukeni na maumivu chini ya tumbo kwa mwanamke ni yutiai, inashauriwa umuone daktari katika hospitali kubwa ili kujua tatizo ni nini.

Leave a Comment